Dar es Salaam. Chama cha National League for Democracy (NLD) kimeanza kikao chake cha siku mbili cha Kamati Kuu jijini Dar es Salaam, leo Jumatano, Julai 1, 2026, kikijikita katika kujadili hali ya siasa nchini, mwelekeo wa chama na mikakati ya muda mrefu kuelekea uchaguzi wa 2030.

Kikao hicho kinachofanyika Buguruni, Wilaya ya Ilala, kimehudhuriwa na wajumbe wa Kamati Kuu, viongozi wa chama pamoja na Msajili msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahozya.

Akizungumza leo Jumatano, Julai 1, 2026 na waandishi wa habari kuhusu kikao hicho, Katibu Mkuu wa NLD na aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, Doyo Hassan Doyo, ameeleza wasiwasi wa chama kuhusu kile alichokiita kampeni za uchochezi zinazoendelea mitandaoni.

“Tunachokiona kwenye mitandao ya kijamii ni kampeni zinazoweza kuathiri utulivu wa nchi. NLD kama chama kinachoheshimu sheria na Katiba, tunalaani vikali mwendelezo wa watu wanaochochea vurugu na kuhamasisha maandamano yasiyo na misingi ya kisheria,” amesema Doyo.

Kauli hiyo inakuja wakati hali ya ulinzi ikiimarishwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na miji mingine, kufuatia tahadhari za kiusalama.

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza (kushoto), akisalimiana na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha National League for Democracy (NLD), wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichofanyika Buguruni, jijini Dar es Salaam, Jumatano, Julai 1, 2026.

Jeshi la Polisi limekuwa likionekana kuongeza doria na ukaguzi katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu, huku katika nyumba za kulala wageni wakitakiwa kuwa na vitambulisho kikiwamo cha Nida ili kuweza kutambulika wanapotaka kuduma.

Aidha, Serikali wiki iliyopita ilitangaza kusitisha kwa muda mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, ikieleza hatua hiyo inalenga kulinda amani na kuzuia uvunjifu wa utulivu unaoweza kuchochewa na taarifa za mitandaoni.

Akizungumzia msimamo wa NLD kuhusu uamuzi huo, Doyo amesema chama chake hakioni zuio hilo kama kikwazo cha shughuli za kisiasa.

“Zuio la mikutano ya hadhara halijazuia siasa nchini. Linahusu mikutano tu, lakini shughuli za vyama zinaendelea. Ndiyo maana tuko hapa, tunafanya kikao chetu kama kawaida. Hata vyama vingine vinaendelea na vikao vyao vya ndani,” amesema.

Doyo amesisitiza NLD inaunga mkono hatua zinazolenga kulinda amani, akisema siasa lazima zifanyike kwa kuzingatia utulivu wa Taifa.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Pogora Ibrahim, kikao hicho pia kinaangazia tathmini ya uchaguzi uliopita, hali ya kisiasa nchini na ujenzi wa chama kuelekea ushindani wa kisiasa wa siku zijazo.

Taarifa hiyo imeeleza NLD imepanga kuimarisha uongozi wake kupitia mafunzo maalumu kwa viongozi na watendaji wake ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kuimarisha mshikamano wa ndani.

“Kikao hiki kitatoa mwelekeo mpya wa chama, ikiwemo maazimio yatakayosaidia kukiimarisha katika nafasi ya ushindani wa kisiasa na kuongeza uwezo wa kuwahudumia wananchi,” ameeleza Pogora.

Mkurugenzi huyo pia amebainisha kuwa ajenda zingine za kikao hicho ni maandalizi ya muda mrefu kuelekea uchaguzi wa 2030, ambapo chama kinatarajia kujipanga upya kimkakati ili kuongeza ushawishi wake kisiasa.

Kilele cha kikao hicho kinatarajiwa kufanyika kesho Alhamisi, ambapo maazimio rasmi ya Kamati Kuu yatatangazwa, yakihusisha mwelekeo wa kisiasa wa chama, tathmini ya ndani na mikakati ya uimarishaji wa chama hicho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *