KATIKA safari ya utafutaji, suala la kukutana na changamoto ni la kawaida. Waswahili husema changamoto ndizo humkuza mtu.

Mchezaji, kocha au timu inayofanikiwa, ndani yake kuna milima na mabonde, hivyo bila ya uvumilivu, kujifunza na kuendelea kupambana kila kikwazo kinapotokea, suala la mafanikio utalisikia kwa wenzako.

Msemo huo unathibitishwa na mshambuliaji kutoka Zanzibar, Abdallah Iddi Mtumwa ‘Pina’ aliyewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2024-2025 akitupia mabao 21.

Pina ambaye msimu ujao anatarajia kuvaa jezi ya JKT Tanzania inayoshiriki Ligi Kuu Bara, amepiga stori na Mwanaspoti akizungumzia safari yake ya soka huku kubwa zaidi akifichua tukio ambalo hawezi kulisahau alipokwenda DR Congo kupambania ndoto zake.

Mshambuliaji huyo ambaye mwanzoni mwa msimu wa 2025-2026 alisajiliwa na Pamba Jiji ya Mwanza, lakini hakufanikiwa kucheza mechi hata moja ya mashindano baada ya kuumia, akalazimika kurudi Zanzibar kuitumikia Muembe Makumbi kabla ya sasa kupata dili jipya.

Mahojiano ya Mwanaspoti na Pina, yalifanyika nyumbani kwake maeneo ya Kwa Mchina, Unguja, Zanzibar ambapo anaanza kwa kufichua jina lake maarufu lilipoanzia.

“Zamani kulikuwa na mchezaji anaitwa Pina (Steven Pienaar, nyota wa zamani wa Afrika Kusini), mama yangu alikuwa anacheza mpira, baada ya kuacha, akaendelea kufuatilia.

“Sasa hilo jina la Pina, wakati nipo mdogo nilikuwa ninamuonekano kama wa huyo mchezaji. Kwahiyo jina lilianzia kwa mama yangu kuniita Pina na limekua hadi leo,” anaanza kusimulia nyota huyo.

Steven Pienaar ni kiungo aliyestaafu kucheza soka Machi 2018, mbali na kuitumikia timu ya taifa ya Afrika Kusini, pia amecheza klabu mbalimbali nchini humo ambazo ni Ajax Cape Town na Bidvest Wits.

Pia alicheza soka Ulaya katika timu za Ajax (Uholanzi), Borussia Dortmund (Ujerumani), kisha akaweka mizizi pale England akicheza Everton, Tottenham Hotspur na Sunderland. 2017 ndipo akarejea Afrika Kusini alipoichezea Bidvest Wits hadi anastaafu. Kwa sasa ana taaluma ya ukocha.

ALICHOKUTANA NACHO DR CONGO

Pina anasema, wakati anaichezea timu ya Chaux Sport ya DR Congo mwaka 2022, alishikwa bega na mchezaji mwenzake wakati wa mazoezi, baada ya hapo, alijikuta kwenye hali mbaya na kushindwa kuendelea kucheza hadi akarudi Zanzibar.

Anasema, awali hakuwa na wasiwasi wowote zaidi ya kuchukulia jambo la kawaida mnapokuwa mazoezini kugusana inatokea, lakini baada ya hapo, alikuja kugundua mwenzake huyo hakuwa na nia nzuri.

“Baada ya kuona nakuja kwa kasi mazoezini na kumfanya akose nafasi ya kucheza, alikuja kwa njia nyingine ambayo alinishika bega mara kwa mara ninapokuwa na mpira, kumbe mkononi mwake alikuwa na sumu ambayo ilibaki kwenye bega langu baadaye ilisambaa mwilini nilivyokuwa najifuta jasho,” anasema Pina.

“Nilikuwa nashangaa siku ile kila muda alikuwa ananishika mabegani anapokuja kupambania mpira hadi wachezaji wengine walikuwa wananiambia nisikubali anishike bega,” anasema.

Anafafanua kuwa, baada ya kufika usiku alianza kuharisha na kutapika, hapo alichukuliwa hadi hospitali na ndipo ilipogungulika kuwa amewekewa sumu.

“Daktari aliniambia nimewekewa sumu, walionipeleka hospitali akiwemo kocha King ambaye nilikuwa ninakaa naye karibu pale ninapoishi akashangaa. Nikaanza kujiuliza nimekula wapi chakula chenye sumu.

“Lakini yule daktari akasema kule Congo kuna dawa hiyo mtu anaweza kuipaka mkononi na kukushika, wewe ukiinusa tu, unakutana na hiyo shida, hapo ndipo nikakumbuka wakati tupo mazoezini kuna mchezaji alikuwa akinishika sana mabegani,” anasimulia.

Anasema hiyo ni miongoni mwa changamoto kubwa aliyowahi kukutana nayo katika safari yake ya soka hadi kufikia sasa, huku akibainisha kwamba, mchezaji aliyemfanyia hivyo, aliamini kwamba uwepo wa Kocha Othman King ambaye naye anatokea Zanzibar, angekuwa ananipa sana mimi nafasi kuliko yeye, ndiyo maana akachukua uamuzi huo wa kunipunguza kasi.

Kwa wale wasiomfahamu vizuri Pina, ni mshambuliaji aliyetokea kwenye familia yenye damu ya soka kuanzia baba, mama na hata mdogo wake Mrisho Iddi Mtumwa anayecheza namba sita mwenye umri wa miaka wa 14, anapita katika njia hiyohiyo.

Anasema kuwa, mdogo wake huyo ni miongoni watoto wanaokuja kwa kasi zaidi kutokea kwao kwa sababu anajua mpira kumzidi yeye.

“Sisi ni familia ya soka, mama yangu amecheza, baba yangu pia, kwa sasa yupo mdogo wangu na huyo anacheza mpira vibaya mno, nafasi yake ni namba sita anaitwa Mrisho, bado mdogo kama miaka 14 hivi.

USHAURI WA BABA UNAVYOMBEBA

“Nakumbuka zamani, sio zamani sana ni hivi karibuni wakati tayari nimerudi Zanzibar kutoka Congo, baba yangu anaitwa Idd Mwarabu ambaye naye alikuwa mchezaji mkubwa wa soka hapa Zanzibar, yeye ndiye aliyenijenga mimi kwa kuniambia ili niwe mshambuliaji mzuri lazima niwe na uamuzi wa haraka na sio kukaa sana na mpira.

“Aliniambia nikiwa ndani ya boksi niwe na first touch nzuri, nisiwe na mambo mengi, nikituliza moja au mbili nipige golini, niwe na uamuzi wa haraka na hiyo ndiyo imekuwa ikinisaidia katika kufunga kwangu.

RATIBA YAKE YA KULA SIKU YA MECHI

Mshambuliaji huyo anatueleza ratiba yake ya kula siku ya mechi akisema: “Asubuhi mapema nikiamka nakula matunda, ikifika mida ya saa tano au sita mchana, nakula chakula iwe ugali kidogo au wali kidogo, kisha muda mchache kabla ya mechi, nakula tena matunda ndiyo naingia uwanjani. Huwa napenda kula hivyo siku ya mechi.”

KILICHOMUONDOA PAMBA JIJI

Anasema, wakati anatokea Mlandege na kusajiliwa na Pamba Jiji msimu wa 2025-2026, timu hiyo iliamini atafanya makubwa zaidi ya alichokifanya Ligi Kuu Zanzibar.

Matarajio yalikuwa tofauti kwani licha ya kuonesha kiwango kizuri mazoezini, lakini majeraha yalizima ndoto zote.

Anasema, siku moja wakati wapo mazoezini na kikosi cha Pamba Jiji, kuna beki aliyemtaja kwa jina la Chuma alikuwa akipambana naye, sasa yeye alifanya kumtamanisha mpira baada ya kufunga mabao mengi kwenye mechi ya ushindani kati yao.

“Wakati namtamanisha yule jamaa alikuja kwa kasi kuwahi mpira, nikawahi kuuondoa lakini ukabaki mguu ndipo aliponikanyaga na hapo ndipo nilipoumia mguu.

“Mguu ulilia kabisa nikadhani umevunjika, nikakaa chini nikaanza kutibiwa, tangu hapo sikucheza mecho yoyote,” anasema.

Anaeleza kuwa hiyo ndio sababu iliyomfanya kukaa nje ya uwanja muda mrefu na asipate nafasi ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2025-2026. Licha ya kuumia, Pina anasema Kocha Francis Baraza alikuwa hakuachi kwenye safari, timu inapokwenda kucheza mechi naye yupo, anaishia kukaa jukwaani.

Anasema kilipofikia kipindi cha usajili wa dirisha dogo, aliamua kuwaomba viongozi kumpa nafasi ya kurudi Ligi Kuu Zanzibar kwa lengo la kujiweka imara zaidi.

Anafafanua kuwa, uongozi wa timu hiyo haukusita, ulimruhusu na hapo ndipo aliposajiliwa Muembe Makumbi na kupata nafasi ya kucheza Kombe la Mapinduzi 2026, Ligi Kuu Zanzibar na Kombe la Muungano 2026.

Anasema hata hivyo, hakupata nafasi kubwa ya kuonesha ambacho alijipangia kukifanya kwa kipindi hicho cha mkopo wa miezi sita.

Pina, amesisitiza kuwa, hajaachwa na Pamba Jiji kama inavyosemekana, badala yake aliomba kutolewa kwa mkopo na mkataba wake umebaki mwaka mmoja kwa timu hiyo.

“Kama ningekuwa na matatizo, Pamba isingekuwa tayari kutoa barua wala kukubaliana na kile ambacho nilikiomba kutoka kwao,” anasema.

49 NAMBA YA BAHATI

Pina anasema, wakati anajiunga na Mlandege akitokea Kundemba, alikuwa anavaa jezi namba tatu ila baada ya kufika hapo ilikuwa inavaliwa na nahodha wa timu hiyo, hivyo hakuweza kumvua.

Baada ya hapo, kuna shabiki nguli wa timu hiyo anayeitwa Bilali Ander Herera ndiye aliyemshauri kuvaa jezi namba 49 akiamini itakuwa yenye bahati kwake.

Naam! Namba hiyo ilikuwa na bahati zaidi kwani alifanikisha kuwa mfungaji bora wa msimu huo wa 2024-2025 na kuipa ubingwa Mlandege.

Hivyo, anasema kuanzia hapo hiyo ndio ikawa jezi pendwa kwake na hata alipofika Pamba Jiji aliipata jezi hiyo na msimu ujao anapokwenda, ataangalia kama haina mtu, ataivaa, lakini ikiwa na mtu, atamuomba.

RIJKAARD KOCHA MWENYE MCHANGO

Pina amemtaja Mohammed Salah ‘Rijkaard’ kuwa miongoni mwa makocha wenye mchango mkubwa kwake kisoka hadi kufikia kujulikana.

MECHI YA HISTORIA

Pina anasema mechi kati ya Mlandege na Muembe Makumbi msimu wa 2024-2025 ni miongoni mwa mechi zilizompa furaha na maumivu kwa wakati mmoja baada ya mzunguko kwanza kutoka sare ya mabao 2-2 huku marudio wakitoka 2-1 ambapo yeye alifunga mabao manne kwenye mechi hizo.

Mshambuliaji huyo anasema mechi nyingine ni Mlandege dhidi ya Tekeleza msimu wa 2024-2025 ambapo Mlandege ilishinda mabao 11-1, huku yeye akifunga mabao saba na kuwa gumzo.

Anasema, matokeo hayo yalikuja tofauti na matarajio ya wengi kwani ilikuwa mechi ya maelekezo ya kuikazia Mlandege na wapinzani walitakiwa kumkaba yeye.

USHINDANI WA LIGI BARA NA ZANZIBAR

Anasema: “Ligi Kuu Bara ina ushindani mkubwa zaidi ikilinganishwa na Zanzibar kwa sababu ya kila mechi kwao ni fainali tofauti na visiwani hapa.

“Zanzibar ushindani uliopo ni kwa timu chache na sio zote kama ilivyo upande wa Bara na ndio sababu ya Ligi hiyo kukua kutokana na ushindani uliopo,” anamaliza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *