MOROGORO: WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, amesema Kada ya Maendeleo ya Jamii inapaswa kuwa injini ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuongoza mageuzi ya fikra, kuimarisha uchumi wa wananchi na kujenga jamii yenye maarifa, uzalishaji, ubunifu na uzalendo.
Dk Gwajima amesema hayo mjini Morogoro wakati akifungua kikao cha utendaji kazi kwa Wakuu wa Vitengo vya Maendeleo ya Jamii ngazi ya mikoa ambapo pia amegawaa kompyuta mpakato kwa mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
Amesema mafanikio ya Dira ya 2050 hayatategemea ukubwa wa bajeti au idadi ya miradi ya maendeleo, bali uwezo wa kubadilisha fikra na tabia za Watanzania katika kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Dk Gwajima amesema taifa lenye watu wenye maarifa, ubunifu, nidhamu, ujuzi wa teknolojia, uwezo wa kutatua changamoto na utamaduni wa uzalishaji ndilo litakaloongoza dunia.
“Mataifa makubwa duniani hayakujengwa kwa kuwekeza katika miundombinu pekee yalijengwa kwa kuwekeza kwa makusudi katika watu wake,” amesema Dk Gwajima.
Dk Gwajima amesema katika dunia ya leo, ushindani wa Mataifa hauamuliwi tena na ukubwa wa ardhi wala wingi wa maliasili pekee bali unaamuliwa na ubora wa watu wake.
Amesema kuwa barabara, reli, bandari, viwanda na teknolojia vinaweza kujengwa kwa muda mfupi, isipo kuwa kujenga jamii yenye maarifa, maadili, uzalendo, ubunifu na uwezo wa kushindana duniani.

“Kazi hii inayohitaji maono ya muda mrefu, uongozi madhubuti na taasisi imara na hapo ndipo taaluma ya Maendeleo ya Jamii inapopata nafasi yake ya kimkakati,” amesema Dk Gwajima .
Dk Gwajima amemtaka kila Ofisa Maendeleo ya Jamii awe kichocheo cha kuibua fursa za kiuchumi katika eneo lake ikiwa na kuwaunganisha wananchi na teknolojia, masoko, taasisi za fedha, mafunzo ya ujuzi, na huduma za Serikali.
“Lengo letu si kuongeza idadi ya vikundi pekee bali ni kujenga biashara endelevu, kuongeza thamani ya bidhaa na kuongeza kipato cha wananchi,”amesisitiza Dk Gwajima.
Dk Gwajima pia amewataka kuhamasisha mapinduzi ya fikra yatakayojenga utamaduni wa kuthamini kazi, uzalishaji, ubunifu, matumizi ya teknolojia, uwajibikaji na kujitegemea.

Waziri pia amesema ni wakati wa kuifanya taaluma ya maendeleo ya jamii itumie mifumo ya kidijitali ikiwa na kushiriki kikamilifu kujenga familia imara kwa sababu familia ndiyo kiwanda cha kwanza cha mtaji watu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi, amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji mabadiliko makubwa katika sekta ya maendeleo ya jamii ili iweze kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi.
Maswi amesema pamoja na Serikali kuendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya maendeleo, mafanikio yake yatategemea pia mabadiliko ya wananchi kupitia kazi ya maofisa wa maendeleo ya jamii.
Nao washiriki wa kikao hicho kupitia Mwenyekiti wa Wakuu wa Vitengo vya Maendeleo ya Jamii , Elice Simonile, amesema kikao hicho kimewapa fursa ya kujitathmini, kubaini changamoto na vikwazo vinavyoikabili Idara hiyo na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji ili kuleta mabadiliko ya tabia na kuimarisha uzalendo miongoni mwa wananchi.