
BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imeitoza Klabu ya Yanga faini ya Sh100 milioni baada ya kubainika kuwa wachezaji na benchi la ufundi walitumia nyumba iliyo nje ya uwanja badala ya chumba rasmi cha kuvalia katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya JKT Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB iliyotolewa leo Julai 3, 2026, adhabu hiyo inatokana na ukiukwaji wa Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mechi, baada ya tukio hilo kutokea katika mchezo namba 233 uliochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, ambapo Yanga ilishinda mabao 3-0.
TPLB imesema adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 27:7 ya Ligi Kuu kuhusu vyombo vya maamuzi.
Mbali na faini hiyo, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imewapeleka kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Rais wa Yanga, Hersi Said na Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Andre Mtine, kwa tuhuma za kutoa maelezo yanayodaiwa kuwa ya msingi usiokubalika na makosa ya kujirudia kuhusu matumizi ya vyumba rasmi vya kuvalia.
TPLB imeeleza kuwa si mara ya kwanza kwa Yanga kuadhibiwa kwa kosa hilo, ikikumbusha kuwa Mei 2026 klabu hiyo ilitozwa faini ya Sh30 milioni kwa ukiukwaji wa kanuni hiyo hiyo baada ya kutumia nyumba iliyo nje ya uwanja badala ya chumba rasmi cha kuvalia.
Nyumba hiyo ambayo Yanga imeitumia mara mbili ilipokwenda kuchezwa Meja Jenerali Isamuhyo, wamekuwa wakiita Jumba la Maajabu wakidai kwamba imewasaidia kutopoteza dhidi ya Simba zilipotoka 2-2 na ushindi wa mabao 3-0 JKT Tanzania uliopa timu hiyo ubingwa wa tano mfululizo wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu wa 2025-2026.