
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amewatolea wito wananchi kuhudhuria shughuli zijazo za mazishi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, na kutaka kulipizwa kisasi damu safi ya Kiongozi huyo aliyeuawa shahidi.
Katika ujumbe wake kwa taifa la Iran leo Alkhamisi, Muhammad Baqer Qalibaf amesema kuwa shughuli ya mazishi ya Ayatullah Sayyid Ali Khamenei yaliyopangwa kufanyika kuanzia tarehe 4 hadi 9 mwezi huu wa Julai si shughuuli ya kuaga mwili pekee, bali ni tukio ambamo ndani yake Wairani wanatangaza tena utiifu wao kwa njia tukufu ya mashahidi na tunu za Mapinduzi ya Kiislamu.
“Leo, macho ya historia yanaelekezwa Iran. Mkusanyiko mkubwa na wa kihistoria wa mamilioni ya wananchi; nyie ni watu adhimu, muungano huu utakuwa dhihirisho la upendo na uaminifu; ni mahudhurio ambayo, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, yatageuza tukio hili la mazishi kuwa tukio kubwa na la kudumu katika historia ya mwanadamu,” ameongeza kusema Spika wa Bunge la Iran.
Qalibaf ambaye pia ni kiongozi wa timu ya mazungumzo ya Iran amewataka wananchi kuandika ukurasa mtukufu katika historia ya Iran kupitia mwitikio wao wa hamasa katika mazishi ya Imam shahidi, na kwa mara nyingine tena kudhihirisha kuwa taifa la Iran limeungana na kusimama imara katika kutimiza ahadi yake wakati wa matukio muhimu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliuawa shahidi pamoja na baadhi ya wanafamilia wake, tarehe 28 Februari mwaka huu, siku ya kwanza kabisa ya vita haramu vya siku 40 vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Israel dhidi ya Iran.
Shughuli ya mazishi na kuaga mwili wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu zitafanyika Tehran, Qum, Mash’had na katika miji mitakatifu ya Iraq.