Abbas Salehi Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu wa Iran amesema kuwa takriban waandishi habari na wawakilishi wa vyombo vya habari 600 kutoka nje ya nchi wataripoti shughuli ya mazishi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, yaliyopangwa kufanyika kuanzia tarehe 4 hadi 9 mwezi huu wa Julai.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatano, Salehi alifafanua maandalizi makubwa ya wizara yake kwa ajili ya mazishi hayo, ikiwa ni pamoja na mfululizo wa matangazo ya vyombo vya habari, sinema na vipindi vya utamaduni vinavyohusiana na tukio hilo.

Ameongeza kuwa: “Katika sekta ya habari, takriban waandishi wa habari 600 na wawakilishi wa vyombo vya habari vya kigeni, pamoja na vile vya ndani, wataripoti shughuli ya mazishi hayo ili sura mbalimbali za tukio hilo ziweze kufikishwa kwa walimwengu duniani kote.

Waziri wa Utamaduni na Miongozi ya Kiislamu wa ya Iran amesema shughuli ya mazishi ya Shahidi Ayatullah Khamenei si kitendo cha taifa kutoa cha heshima kwa Kiongozi wake tu, bali ni “dhihirisho la nguvu ya taifa, mshikamano wa kijamii, na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuzuia uchokozi wa maadui zake.”

Wakati huo huo, wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 90, pamoja na viongozi wa kidini, wasomi na watu mashuhuri kutoka kote duniani, wametangaza utayarifu wao wa kuhudhuria mazishi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumanne, Ali Akbar Pourjamshidian, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran anayeshughulikia masuala ya Usalama na katibu wa kamati ya maandalizi ya mazishi, amesema kwamba zaidi ya nchi 30 tayari zimewasilisha maombi rasmi ya kutuma wajumbe wa ngazi za juu kwenye mazishi hayo.

Shughuli ya mazishi na kuaga mwili wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu zitafanyika Tehran, Qum, Mash’had na katika miji mitakatifu ya Iraq.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, mwili wa Ayatullah Ali Khamenei utapelekwa Iraq mnamo Julai 8, ambapo mapokezi rasmi yanatarajiwa kufanyika katika uwanja wa ndege wa Baghdad au Najaf yakishirikisha maafisa wakuu wa Iraq. Shughuli ya mazishi imepangwa kufanyika katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala.

Siku inayofuata, Julai 9, Swala ya Maiti na mazishi yamepangwa kufanyika katika mji mtakatifu wa Mash’had, ambapo kiongozi aliyeuawa shahidi wa Iran na familia yake wanatarajiwa kuzikwa karibu na Haram ya mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (SAW), Imam Reza (AS).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *