
Wanajeshi wa Israel wameuuwa shahidi kwa risasi kipa wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza, na hivyo kuifanya idadi ya wanamichezo waliouliwa shahidi na jeshi la Israel kufikia 1,009.
Shirikisho la Soka la Palestina (PFA) limearifu kuwa wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel mapema wiki hii walimuuwa shahidi kwa kumpiga risasi Salim Al-Ashqar aliyekuwa na umri wa miaka 32 katika mji wa Al-Qarara, kaskazini-mashariki mwa Khan Yunis katika Ukanda wa Gaza.
PFA imesema kuwa Al- Ashqar ni kati ya mamia ya watu mashuhuri katika sekta ya michezo ya Palestina waliouawa shahidi tangu jeshi la Israel lilipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Palestina wakazi wa Gaza mnamo Oktoba 2023.
Shirikisho la Soka la Palestina limeeleza kuwa, wanamichezo wa Kipalestina 1,009 wameuawa tangu kuanza vita na mauaji ya kimbari ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Gaza wakiwemo wanasoka 567 wa Palestina.
Taarifa ya PFA imeongeza kuwa kumekuwa na wimbi la majonzi kutoka kwa ndugu, wachezaji wenzake, pamoja na jamii kubwa ya michezo ya Palestina na dunia nzima tangu kuuawa kipa Salim Al-Ashqar.
“Tunaomboleza kwa masikitiko makubwa mauaji ya kusikitisha ya kipa Mpalestina mwenye umri wa miaka 32, Salim Al-Ashqar. Aliuawa na jeshi la Israel. Tunasikitishwa sana na kuendelea matukio ya namna hii. Tunatoa wito wa kupatikana haki na amani,” klabu ya soka ya Chile kwa jina la Deportivo Palestino, ilisema katika taarifa yake siku ya Jumatano.
Kabla ya kuuawa shahidi, Al-Ashqar alikuwa akicheza katika Klabu ya Khan Yunis Service. Pia aliwahi kucheza katika klabu za Al- Aqsa na Al-Musaddar katika Ukanda wa Gaza.
Alifunga ndoa miezi mitano iliyopita, na mkewe anatarajia mtoto wao wa kwanza karibuni.