GEITA: BARAZA la Wazee Halmashauri ya Manispaa ya Geita limelalamikia kukithiri kwa kasumba ya vijana kuzaa watoto na kisha kuwatelekeza kwa wazazi wao pasipo kutoa huduma ya malezi.
Wazee hao wamewasilisha malalamiko yao mbele ya waandishi wa habari mjini Geita na kueleza kuwa kasumba hiyo inawaongezea mzigo wa malezi wazee ingali wengi hawana vipato vikubwa.
Akizungumzia changamoto hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Manispaa ya Geita, Manoni Mgema amesema hoja hiyo inakuja kutokana na vijana wengi kutowajibika kulea watoto waliowazaa.
Amesema tathimini ya Baraza la Wazee imebaini vijana wengi wanapata watoto na kuwatelekeza kwa wazee huku wakikwepa majukumu yao ya msingi ya malezi, mavazi, makazi na chakula.
“Hatusemi kwamba tunawakataa wajukuu, lakini bado tunawakubali kwa uataratibu. Sisi inatuathiri katika kuwahudumia, hatuwezi kuwahudumia kwa sababu nguvu zetu zimekwisha”, amesema.
Amesema changamoto imekua kubwa zaidi kwani baadhi ya vijana hawawajibiki japo kutoa pesa ya matumizi ya watoto wao ili kuwapunguzia mzigo wazee ambao wengi ni wategemezi.
Katibu wa Baraza la Wazee mjini Geita, Marceline Magayane amesema kinachosikitisha ni kuona baadhi ya vijana wameajiriwa ama kujiajiri lakini hawataki kuhudumia au kukaa na watoto wao.

“Mtoto wako umemzaa ana kazi ama ana shughuli nyingine lakini bado anazaa watoto analeta kwako ili uzae upya, yeye yupo anastarehe, huu ni ukatili mbaya sana ambao tumeuona”.
Naye mjane na bibi wa wajukuu wanne, Asteria Buseng’wa amethibitisha uwepo wa changamoto hiyo akidai kuwa anaishi na wajukuu zake baada ya binti zake kutengana na waume zao.
“Waligombana na waume zao, wakaja na watoto, tukakaa nao, kidogo wakasema mama tukatafute hela huku hela hamna, wakaenda, lakini sasa hata kutuma hela hakuna”, amesema.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Geita, Cathbert Byabato amekiri kupokea malalamiko hayo ya kueleza kuwa vijana wanapopata watoto wanawajibika kulea na siyo kukimbia majukumu.
Amesema tabia ya kuwaachia wazee mzigo huo ni kinyume na maadili ya jamii na kunaweza kuchangia kuongezeka kwa changamoto za kijamii na kiafya kwa wazee na watoto.
“Unakuta watoto wengi wanaishia mtaani, pasipo kupata haki zao za msingi kama elimu, kwa hiyo tunaendelea kutoa rai kwa vijana ambao wanakuwa na watoto, watimize wajibu wao” amesema.