TANGA: SERIKALI imepokea mradi wa usambazaji wa maji katika mtandao wa bomba wa Kwamaizi, uliotekelezwa katika Kata ya Kideleko, Halmashauri ya Mji Handeni mkoani Tanga, kwa gharama ya Shilingi milioni 465.1.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo, yakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, ambaye amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji safi na salama.
Mradi huo umetekelezwa na shirika la WaterAid Tanzania kwa ufadhili wa OKF.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhandisi Mwajuma Waziri amesema kukamilika kwa mradi huo ni hatua kubwa katika kuboresha afya na ustawi wa wananchi wa maeneo husika.
“Serikali imejipanga kikamilifu kuendeleza ushirikiano na wadau ili kuboresha huduma za maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi. Ni wajibu sasa kwa Mamlaka ya Majisafi Handeni (HTM), RUWASA, viongozi wa Serikali za Mitaa na wananchi wenyewe, kulinda na kutunza miundombinu hii ili iwe na tija kwa muda mrefu,” alisema Mhandisi Waziri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga, amebainisha kuwa mradi huo umetumia jumla ya Sh milioni 465.1 na unatarajiwa kunufaisha wakazi 6,037 wa maeneo ya Kideleko, Kampene, Muungano, Ndekai na Bangu.

“Usimamizi bora wa miundombinu hii ndio utakaohakikisha kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa unaendelea kuleta matokeo chanya na kupunguza changamoto ya maji kwa wananchi wetu kwa kipindi kirefu,” alisema Mzinga.