
ILIPOISHIA
Nikakaa kwenye jamvi. Kimoyomoyo nilikuwa najiuliza kwanini hawa waganga wa kienyeji hawaboreshi mazingira yao wakati wanapata pesa nyingi. Kila siku tunakaa chini tu.
Mganga alikuwa amekaa mbele yangu.
“Haya niambie umefanya zile dawa?” mganga huyo akaniuliza.
“Nimefanya”
“Umemtilia kwenye chakula?”
“Nimemtilia kwa siku tatu kama ulivyoniagiza”
“Na wewe umekula hicho chakula?”
“Ilibidi nile ile siku ya kwanza. Unajua niliitia kwenye mchuzi. Akaniambia mchuzi mchungu, hebu uonje. Nikauonja”
“Lakini haina madhara hata kama umeuonja”
“Na siku ya pili nilimtilia kwenye juisi akanywa kidogo kisha akaninywesha na mimi.”
SASA ENDELEA…
“SAWA kabisa. Maana yake ni kuwa anakupenda”
“Kweli eh?”
“Kweli kabisa. Anachokula yeye anataka ule na wewe”
“Tuseme hivi sasa ananipenda?”
“Wewe ndio uniambie kwa sababu ndiye unayeishi naye”
“Mimi naona bado kidogo. Jana nimemuomba pesa ameniambia mpaka mwisho wa mwezi”
“Sasa wewe ulitakaje?”
“Nilitaka anipe hapo hapo”
“Sasa kama hana atakupa nini?”
“Sio kama hana. Pesa anazo isipokuwa anajishauri tu kuwa anipe au asinipe”
“Hana ujanja, tutashughulika naye mpaka tutamuweka sawa”
“Mimi nataka vile nikimuomba pesa anipe hapo hapo”
“Huko ndiko unakoelekea, usiwe na wasiwasi. Wewe kidogo una nuksi ya jini, tukiiondoa tu, atakuona kama kioo”
“Kumbe nina nuksi eh?”
“Unayo nuksi ya jini dume, itabidi leo twende huko mzimuni tukaiondoe”
Hata sikumuuliza huko mzimuni ni wapi na kama ni lazima twende huko, nikajikuta nikimjibu.
“Haya twende”
“Subiri niandae dawa zangu”
Baada ya robo saa hivi akaniambia.
“Tayari, sasa tunaweza kwenda”
Alikuwa ameshika mfuko wake uliokuwa na dawa.
Tukatoka. Aliwambia wale wanawake kwamba tulikuwa tunakwenda mzimuni.
Tukaanza safari ya kuelekea huko mzimuni. Tulitembea kwa miguu nikidhani palikuwa karibu. Kumbe palikuwa na kipande kirefu cha mwendo.
Palikuwa ni kwenye pori. Hakukuwa na barabara isipokuwa njiaza kupita kwa miguu.
Tulitokea mahali ambapo palikuwa na mibuyu mitatu iliyoota pamoja na kuunda alama ya V huku ikiwa imezungukwa na kichaka. Kando ya ile mibuyu palikuwa na nyumba ndogo iliyojengwa kwa miti na udongo na kuezekwa kwa makuti ya mnazi.
“Tumeshafika. Mzimu wetu ndio huu hapa” Mganga akaniambia.
Palikuwa na kijinjia chembamba kilichoelekea ndani ya kile kichaka kilichoundwa na ile mibuyu. Mganga akasimama mbele ya kile kichaka kisha akapiga hodi.
Baada ya kupiga hodi akaingia ndani ya kichaka hicho.
“Na mimi nije?” nikamuuliza.
“Nisubiri hapo hapo halafu nitakwambia uje”
“Sawa” nikamjibu.
Mganga aliingia kwenye kile kichaka na kupotea. Akiwa humo ndani ya kichaka niliisikia sauti yake akizungumza. Sikuweza kujua alikuwa akizungumza na watu au na majini.
Nilimsikia akisema.
“Nyinyi watawala wa mzimu huu. Nimewaletea mgeni mwenye shida zake. Nawaomba musaidie kutatua matatizo yake na mumewe”
Sauti ya mganga ikapotea kidogo kisha nikaisikia tena ikisema.
“Shida yake, hasikizani na mume wake. Nimeona ana nuksi inayosababisha mume wake asimpe pesa na pia asiwe na mapenzi naye”
Sauti ya mganga ikapotea tena. Baada ya sekunde chache ikasikika tena.
“Mnasema nuksi yake haiwezi kuondoka mpaka kwa kitendo mashuhuri?” sauti ya mgana ilikuwa kama inayouliza.
Nikahisi huenda alikuwa akisemeshana na majini wa mzimu huo. Lakini sauti za majini hao alikuwa akizisikia yeye mwenyewe.
Sauti yake Ikasikika tena.
“Kitendo mashuhuri kama kitendo gani?”
Pakapita ukimya mwingine wa sekunde chache kabla ya sauti ya mganga huyo kusikika.
“Yaani mimi nifanye naye tendo la ngono hapa hapa kwenye mzimu?” alikuwa kama anauliza.
Halafu baadaye akasema.
“Nimeelewa” Akaongeza tena.
“Basi nitamwambia mlivyoniambia. Hakuna tatizo. Nyinyi ndio waganga”
Baada ya hapo sikuisikia tena sauti ya mganga huyo. Nilikuja kumshitukia mganga huyo ametokeza pale kwenye kinjia.
“Njoo” akaniambia huku akirudi alikotoka.
Nikamfuata. Mwili wangu ulikuwa umejaa baridi ya hofu. Yale maneno ambayo alikuwa akisemeshana na hao majini wake niliyaelewa. Alitakiwa afanye tendo la ngono na mimi. Hilo peke yake likanitia baridi.
La pili lililokuwa llimenitia hofu ni lile aeneo tuliloingia, lilikuwa linatisha. Baada ya kupiga hatua chache tu tukatokea mahali pa wazi. Ukiwa mahali hapo unakuwa kama upo ndani ya kibanda cha nyasi. Kutaza kibanda hicho ni mashina ya ile mibuyu mitatu.
Ile mibuyu ilikuwa imetundikwa kila kitu kinachotisha. Ilikuwa imetundikwa mafuvu ya watu na wanayama. Mifupa ya mikono na miguu, ilikuwa ikining’inia kilaupande.
Ngozi za wanyama, shuka za rangi mbali mbali na tunguri, vilikuwa vimening’inizwa kwenye mibuyu. Kulikuwa na makorokoro mengine ambayo sikuyaelewa yakiwemo majongoo makubwa yaliyozagaa katika eneo lote.
Katikakati ya eneo hilo palikuwa na kitu kama kichanja kilichotemgezwa kwa miti. Juu ya kichanja hicho palitandikwa ngozi iliyokuwa imewambwa kamangoma.
Mganga aliponiingiza katika eneo hilo aliniambia.
“Sasa unatakiwa uvue nguo zako zote, ulale hapa juu ya ngozi ushughulikiwe”
Nilishindwa hata kuuliza nishughulikiwe nini, nikajikuta ninavua nguo bila kupenda nikabaki uchi wa mnyama! Mganga aliniona kila kitu bila kificho. Nikamuona na yeye anavua nguo zake na kubaki uchi wa mnayama!
Alichukua ule mfuko aliokwenda nao akatoa tunguri na kujipaka dawa sehemu yake ya siri kisha akairudisha ile tunguri kwenye mkoba.
“Sasa lala kichalichali hapa juu ya ngozi, tuondoe matatizo yako”
Nikapanda pale kwenye kichanja na kulala kichalichali. Mganga naye akapanda. Kilichofuatia hapo umeshakijua. Naona aibu hata kukieleza. Baada ya hapo mganga akaniambia nivae nguo zangu nikavaa, na yeye akavaa nguo zake. Akaniambia.
“Shika huu mfuko, twendezetu”
Nikaushika ule mfuko wake wenye vifaa vya uganga tukatoka katika lile eneo na kuanza mwendo mwingine wa kurudi.
Tulirudi mpaka nyumbani kwa mganga. Tulipofika ndio sikutaka kuondoka tena nyumbani kwake.. Nikabaki hapo hapo. Sikukumbuka tena kule kwa mume wangu.
Amini usiamini nilihshinda pale hadi jioni nikala ugali na wale wanawake ninaowakuta pale nyumbani.
Kile kitendo tulichokwenda kukifanya kule, kilibadili mawazo yangu kabisa. Nikajiona nimekuwa mke wa mganga.
Yule mganga kwa kujua alichokifanya, hakuniuliza ni kwanini siondoki pale nyumbani kwake.
Ajabu ni kwamba baada ya kula ugali, nilichukua vyombo na kuuliza mahali pa kuoshea vyombo. Nilipooneshwa nikaenda kuviosha.
Ilipofika usiku mganga aliwaita wale wanawake ninaowakuta pale nyumbani. Siku za kwanza nilipokuwa nakuja pale nyumbani nilikuwa ninakuta wanawake watatu. Lakini baadaye nikawa nawakuta wanawake wawili.
Wanawake hao walipoitwa na mganga, wakaambiwa wakae chini pamoja na mimi. Tukakaa. Mganga akanitambulisha kwamba wale walikuwa ni wake zake. Mke mkubwa na mke mdogo.
Aliniambia mke mkubwa alikuwa anitwa Mwanasozi. Mke mdogo aliitwa. Mwadawa.
Mganga baada ya kunitambulisha wale wanawake,na wao akawatambulishakwangu. Aliwambia mimi nilikuwa mke wake wa tatu.
“Pale mlipoona tunaondoka. Tulikwenda kufunga ndoa mzimuni. Niliambiwa na mzimu nimuoe. Kwa hiyo mtakuwa mnakaa naye hapa”
Yale maneno yalikuwa ya uongo lakini ajabu ni kuwa yule mganga alipokuwa akiwaeleza wake zake uongo huo, nilikuwa nacheka cheka kwa furaha.
Majina ya wanawake hao sukuwahi kuyasikia popote maishani mwangu. Baada ya mganga kumaliza maelezo yake, Mwanasozi mke mkubwa wa mganga huyo akanikaribisha kwa kuniambia.
“Tunakukaribisha kwa mikono miwili mwenzetu. Kama ulivyofahamishwa sisi ndio wake wenzako. Tutakuwa pamoja, tutashirikiana na kusaidiana na mume wetu katika kazi zake ikiwemo kumhudumia yeye”
Akaendelea kuniambia.
“Kwa sasa hivi wewe ni mgeni. Unaweza kuona taabu kuishi hapa lakini baadaye utazoea kwani hata sisi tulikuwa hivyo hivyo lakini baadaye tumezoea, tunajiona tuko nymbani”
Aliponiambia hivyo nikamshukuru na kumuahidi kuwa nitashirikiana nao katika raha na taabu.
“Sitamuheshimu mume wangu peke yake, nitawaheshimu hata nyinyi wake wenzangu mlionitangulia” nikamwambia.
Mke mdogo naye akanikaribisha na kuniambia amefurahi kuona wamepata mwenzao tena msichana. Naye akaahidi kushirikiana na mimi na kunipa muongozo nitakaouhitaji.