
TORONTO, CANADA. Timu ya taifa ya Ureno, imefuzu hatua ya 16 bora baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Croatia katika mechi kali na ya kuvutia iliyopigwa Kwenye Uwanja wa BMO, uliopo huko Toronto, Ontario, Canada.
Katika mechi hiyo, Croatia ilianza kupata bao dakika ya 53, kupitia winga, Ivan Perisic kisha nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo akarejesha matumaini ya kikosi hicho dakika ya 68, baada ya kusawazisha kwa penalti.
Hata hivyo, mshambuliaji, Goncalo Ramos aliihakikishia Ureno kufuzu hatua ya 16 bora baada ya kufunga bao la pili dakika ya 90+4, akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Rafael Leao.
Ushindi huo kwa Ureno unaifanya kufuzu hatua ya 16 bora, ambapo sasa itakutana na Hispania iliyofuzu pia baada ya kuifunga Austria mabao 3-0.
Macho ya mashabiki wa soka duniani sasa yataelekezwa kwenye pambano la hatua ya 16 bora litakalowakutanisha Ureno na Hispania, huku mvuto mkubwa ukiwa kwenye tofauti kubwa ya umri kati ya nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo na nyota chipukizi wa Hispania, Lamine Yamal.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, ataingia uwanjani akiwa mmoja wa wachezaji wenye uzoefu mkubwa zaidi katika historia ya Kombe la Dunia, huku Yamal, mwenye umri wa miaka 18, akiendelea kuandika historia kama mmoja wa vipaji vinavyotikisa soka la dunia.
Tofauti ya miaka 22 kati ya nyota hao wawili imeifanya mechi hiyo kutazamwa kama pambano la vizazi viwili tofauti; Ronaldo akiwa alama ya enzi iliyotawala soka kwa zaidi ya miongo miwili, wakati Yamal akiwakilisha kizazi kipya kinachoanza kutawala.
Timu ya taifa ya Ureno imekuwa na historia mbalimbali nzuri katika Kombe la Dunia, ingawa haijawahi kuchukua taji hilo, licha ya kushiriki kwake mara tisa tangu ilipoanza mwaka 1966, 1986, 2002, 2006, 2010, 2014, 2018, 2022 na sasa 2026.
Ushiriki wa kwanza wa fainali za mwaka 1966, huko England, Ureno ilipata mafanikio makubwa kwa kumaliza nafasi ya tatu baada ya kuifunga Umoja wa Kisovieti (USSR) mabao 2-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Goodison Park, Julai 28, 1966.
Mafanikio mengine ni kufika nusu fainali Kombe la Dunia mwaka 2006, lililofanyika Ujerumani, ambapo Ureno ilichapwa na Ufaransa bao 1-0 kwa penalti ya dakika ya 13, ya Zinedine Zidane, kwenye mechi iliyopigwa Allianz Arena, Julai 5, 2006.
Pia, Ureno ilifika robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022, lililofanyika Qatar ambapo kikosi hicho kilichapwa bao 1-0 na Morocco, mfungaji akiwa Youssef En-Nesyri dakika ya 42, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Al Thumama, Desemba 10, 2022.
Kwa upande wa Croatia, inashiriki mara saba michuano ya Kombe la Dunia tangu ilipoanza kushiriki mara ya kwanza mwaka 1998 huko Ufaransa na kushangaza mashabiki wengi wa soka duniani, baada ya kikosi hicho kumaliza nafasi ya tatu.
Katika michuano ya mwaka 1998, aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Davor Suker aliyetamba na timu za Real Madrid na Sevilla za Hispania na Arsenal ya England, alikuwa mfungaji bora wa Kombe la Dunia baada ya kumaliza kwa kufunga mabao sita.
Mafanikio makubwa kwa Croatia ni ya Kombe la Dunia mwaka 2018, lililofanyika Urusi, ambapo ilifika fainali kwa mara ya kwanza kwenye historia yake, japo ilichapwa na Ufaransa mabao 4-2, Julai 15, 2018 na kumaliza ikiwa nafasi ya pili.
Katika Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar, Croatia ikaendeleza kiwango bora na kuishia nusu fainali baada ya kuchapwa na mabingwa Argentina mabao 3-0, Desemba 3, 2022, ikamaliza nafasi ya tatu kwa kuifunga Morocco mabao 2-1, Desemba 17, 2022.