VIONGOZI wa dini nchini wametakiwa kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na wananchi kwa kuhamasisha umuhimu wa kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa ili kuzuia vitendo vya vurugu vinavyoweza kukwamisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Dk. Evaline Munisi, wakati wa kikao chake na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali nchini.

Dk. Munisi amesema viongozi wa dini wana nafasi ya kipekee katika kujenga jamii yenye maadili, uwajibikaji na mshikamano, kutokana na ushawishi wao mkubwa kwa waumini na jamii kwa ujumla. Amesema pamoja na kuhubiri amani, viongozi hao wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kuijenga Tanzania yenye uchumi imara na maendeleo jumuishi.

“Viongozi wa dini ni nguzo muhimu ya amani na maendeleo ya taifa. Tunawaomba waendelee kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa umoja, uvumilivu na mshikamano, pamoja na kuwahamasisha vijana kujituma katika uzalishaji mali, kujiajiri na kutumia fursa zilizopo kuchangia maendeleo ya nchi,” amesema Dk. Munisi. SOMA: Vijana mikoa 4 kunufaika na mradi Dumisha Amani

Kwa upande wao, viongozi wa dini walioshiriki kikao hicho waliipongeza Serikali kwa kuendelea kuwashirikisha katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya taifa, huku wakisisitiza umuhimu wa ushirikiano huo kuendelezwa ili kuimarisha umoja wa kitaifa na mshikamano wa Watanzania.

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Alhaj Nuhu Jabir, alisema viongozi wa dini wako tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha amani, maadili mema na maendeleo endelevu. Naye Askofu wa Christian Council of Tanzania (CCT), Kanali Joseph Mutorela, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kujenga maadili kwa vijana ili kulinda mustakabali wa taifa.

Kwa upande wake, kiongozi wa dini Azza Nyamkababi alipendekeza somo la dini lipewe nafasi zaidi katika ngazi za awali za elimu ili kusaidia kujenga maadili mema kwa watoto na vijana tangu wakiwa shule za msingi. Viongozi hao walieleza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na taasisi za dini utachangia kuimarisha amani, mshikamano wa kitaifa na utekelezaji wenye mafanikio wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *