
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kimkakati, kisiasa na kibunge kati ya Tehran na Beijing.
Kwa mujibu wa Pars Today, Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema hayo hapa mjini Tehran katika mkutano wake na He Wei, Naibu Mwenyekiti wa Bunge la Watu la China, na kubainisha kwamba, kuna ulazima wa kuimarisha uhusiano wa kimkakati, kisiasa na kibunge kati ya Tehran na Beijing.
Aliongeza kuwa, hali ya eneo baada ya vita vya hivi karibuni na matukio mapya ya kisiasa imefanya uratibu wa karibu zaidi kati ya Iran na China kuwa muhimu zaidi kuliko hapo awali. Pia alisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaruhusu aina yoyote ya uingiliaji wa Marekani katika Mlango wa Hormuz.
Katika mkutano mwingine wa siku hiyo na Igor Sergeyenko, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Belarus, Qalibaf alitoa shukrani kwa msimamo wa Belarus wa kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya mashambulizi ya utawala wa Kizayuni na Marekani.
Qalibaf alisema kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni hazikufanikisha malengo yao yoyote katika vita vya siku 12 dhidi ya Iran, na kwamba sasa wengi wamefikia hitimisho kuwa hatua ya kijeshi dhidi ya Iran imeshindwa na kugonga mwamba.
Aidha, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika mkutano wake na Mohamed al-Halbousi, mwenzake wa Iraq ambaye amesafiri kuja Tehran kuhudhuria mazishi ya kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, alisisitiza uhusiano wa kina uliopo kati ya mataifa ya Iran na Iraq.
Qalibaf aliishukuru serikali na wananchi wa Iraq kwa mshikamano na uungaji mkono wao wakati wa vita vya hivi karibuni, akisema kuwa ushirikiano wa Tehran na Baghdad katika nyanja za usalama, uchumi na usafirishaji wa bidhaa (transit) utakuwa msingi muhimu wa kuimarisha usalama na kuwa chache ya maendeleo ya eneo zima.