Dar es Salaam. Wakati baadhi ya maeneo nchini Tanzania yakianza kushuhudia joto la chini kuwahi kutokea, madaktari wametoa tahadhari kwa wazazi wakishauri mbinu za kuwakinga wanafunzi wanaorudi masomoni kwenye maeneo yenye baridi kali.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Julai mwaka huu kunatarajiwa kuwa na vipindi vya baridi kali zaidi kuliko miezi mingine ya msimu wa kipupwe.

Hili linawahusu zaidi hususan wazazi wenye watoto wanaosoma katika mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi na baadhi ya maeneo ya Kilimanjaro na Arusha.

Kwa mujibu wa madaktari, mwanafunzi anayekwenda shule za bweni (boarding) mabadiliko haya ya hali ya hewa yanaweza kuwa changamoto kubwa ikiwa maandalizi hayajafanyika mapema, hasa kwa wale wanaotoa maeneo yenye joto watakaojikuta wakikabiliwa na mazingira tofauti.

Kwa mujibu wa kalenda ya masomo, shule zimeanza kufunguliwa kuanzia Julai 29 na nyingi zitafunguliwa Jumatatu Julai 6 huku shule za bweni tayari zimeanza kupokea wanafunzi.

Maji, mafuta

Wakati wa baridi watu wengi huhisi hawana kiu, hata hivyo wataalamu wanasema mwili bado unahitaji maji ya kutosha. Upungufu wa maji mwilini unaweza kutokea hata wakati wa baridi na kuathiri uwezo wa mwanafunzi kujifunza na kuzingatia masomo.

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji kutoka Hospitali ya Aga Khan, Alex Masao anasema maji ni muhimu sana kwa mtu anayeishi maeneo yenye baridi kali.

“Ni vema wazazi wakawashauri watoto wanywe maji kwa wingi wawapo shuleni. Hawezi kusikia kiu, lakini anatakiwa mwili wake kunywa maji ya kumtosha ndiyo njia pekee ya kupambana na baridi,” anasema.

Pia anasema mafuta ya mgando ni muhimu kwa kuwa hufanya kazi kwa kuunda tabaka juu ya ngozi ambalo huzuia upotevu wa unyevu. Hii husaidia kupunguza ukavu, kupasuka kwa ngozi na michubuko inayoweza kusababishwa na hewa ya baridi.

Hata hivyo, Dk Masao ametaja changamoto yake ni kwamba mafuta ya mgando hayatoi unyevu moja kwa moja kwenye ngozi, bali hufunga unyevu uliopo tayari.

“Wanasema ukitumia mafuta ya mgando mwili unashindwa kupumua vizuri, vinyweleo vinashindwa kutoa hewa vizuri.

“Ikiwa ngozi imekauka sana, kupaka mafuta ya mgando pekee kunaweza kusiwe na manufaa makubwa. Mara nyingi hupendekezwa kutumia losheni au krimu yenye uwezo wa kuongeza unyevu kwanza, kisha kupaka mafuta ya mgando juu yake ili kuzuia unyevu huo usipotee,” anasema.

Anafafanua kuwa kwa wanafunzi wanaokwenda shule za bweni katika mikoa yenye baridi kali kama Njombe, Iringa au Mbeya, mafuta ya mgando yanaweza kusaidia kulinda ngozi dhidi ya ukavu.

Hata hivyo, yanapaswa kutumiwa kwa kiasi kinachofaa kwa sababu yakipakwa mengi yanaweza kufanya ngozi kuwa nzito, kuziba baadhi ya vinyweleo au kusababisha usumbufu kwa watu wenye ngozi inayopata chunusi kirahisi.

Kwa hiyo, yanaweza kuwa msaada mzuri wa kulinda ngozi dhidi ya ukavu unaosababishwa na baridi, lakini matokeo bora hupatikana yanapotumiwa sambamba na bidhaa zinazoongeza unyevu wa ngozi na kwa kuzingatia aina ya ngozi ya mtumiaji.

TMA pia imeonya kuwa msimu huu wa kipupwe unaweza kuambatana na ongezeko la magonjwa yanayohusiana na mfumo wa upumuaji, mafua, homa ya mapafu pamoja na magonjwa ya macho yanayochangiwa na vumbi kutokana na upepo.

Hivyo, tahadhari binafsi na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ni muhimu katika kipindi hiki.

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji, Elisha Osati anasema baridi kali linaweza kusababisha wadudu na bakteria wakahama kutoka kwenye mdomo na kuingia katika njia ya hewa na kusababisha ugonjwa.

“Kama mtoto ana historia ya pumu, mzio, sinusitis au magonjwa ya mara kwa mara ya mfumo wa upumuaji, ni vyema mzazi awasiliane na uongozi wa shule pamoja na wahudumu wa afya kabla ya muhula kuanza.

“Dawa anazotumia kwa kawaida zinapaswa kuwepo kwa kiasi cha kutosha, pamoja na maelekezo ya matumizi,” anasema na kushauri kuwa watoto wapewe chakula cha moto, mazoezi na mchakamchaka na usafi wa mwili nao ni muhimu licha ya baridi.

“Watoto wengi hupunguza kuoga kutokana na maji kuwa baridi, jambo linaloweza kuongeza hatari ya magonjwa ya ngozi na maambukizi mengine. Endapo shule ina maji ya moto ni vizuri kuyatumia, na kama hakuna, kuoga kwa haraka huku mwili ukifunikwa vizuri baada ya kuoga kunaweza kusaidia.”

Mbali na afya ya mwili, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Pedro Pallangyo anasema maandalizi ya kisaikolojia ni muhimu kwa wanafunzi wanaoanza maisha ya bweni kwa mara ya kwanza au wanaorejea kipindi hiki cha baridi.

“Wazazi wanapaswa kuwaeleza mapema kuhusu hali ya hewa watakayokutana nayo ili wasishtuke. Pia wawafundishe umuhimu wa kuvaa nguo za joto kila mara, kutoruhusu viatu au nguo kubaki na unyevunyevu na kutoa taarifa mapema kwa walimu wanapojisikia kuumwa,”amesema Pallangyo.

Anasema mzazi lazima amtafutie mtoto sare za kumkinga na baridi, mavazi ya ndani ya joto ili yasaidie kuhifadhi joto la mwili, sweta nzito angalau mbili ili awe na ya kubadilisha, soksi nene za pamba au sufu hasa wakati wa kulala au asubuhi.

“Mzazi anaweza kumtafutia kofia ya sufu na glovu ili kulinda kichwa, mikono na masikio pamoja na viatu vyenye joto na visivyopitisha maji ili kulinda miguu dhidi ya baridi na unyevunyevu, hasa nyakati za kujisomea usiku darasani,” anasema na kuongeza kuwa ni muhimu kuwatafutia mavazi ya kulalia yenye joto.

Wanafunzi wa kutwa

Mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la World Vision, David Gambo anasema kwa watoto wanaotokea nyumbani, ni muhimu mzazi kuhakikisha mtoto anaondoka nyumbani akiwa ameshiba, akipewa vyakula vya joto kama uji wa lishe, uwele au uji wa viazi vitamu.

“Mfunze kubeba chupa ya maji ya moto au thermos ikiwa inaruhusiwa shuleni. Lishe yake iwe na vyakula vinavyoongeza nguvu na kinga ya mwili kama vile ndizi, viazi, mboga za majani, maziwa na protini,” anasema.

“Kwa kundi hili changamoto si ndogo, wengi huondoka nyumbani alfajiri wakati joto likiwa chini sana,” anasema Dk Pedro na kuongeza kuwa ni muhimu kuvaa mavazi yanayofaa, kula kifungua kinywa cha moto inapowezekana na kubeba chupa ya maji kwa matumizi ya siku nzima.

Kwa jumla, mafanikio ya mwanafunzi hayategemei vitabu na walimu pekee. Maandalizi mazuri ya kukabiliana na mazingira ya baridi yanaweza kumsaidia kuwa na afya njema, kuhudhuria vipindi bila usumbufu na kuzingatia masomo yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *