
Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania, imesema imewekeza zaidi ya Sh1 trilioni katika kupanua na kuboresha miundombinu ya mawasiliano nchini, hatua inayolenga kuharakisha ushirikishwaji wa kidijitali na kuongeza fursa kwa Watanzania kushiriki katika uchumi wa kidijitali.
Uwekezaji huo umewezesha kampuni kujenga zaidi ya minara 4,800 ya mawasiliano, hatua iliyopanua huduma za intaneti katika maeneo mengi ya vijijini na yale yaliyokuwa hayafikiwi na huduma hizo.
Akizungumza leo Jumamosi, Julai 4, 2026, kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yas Tanzania, Pierre Canton amesema kampuni hiyo inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma bora za kidijitali.
“Hatuwekezi kwenye miji mikubwa pekee. Dhamira yetu ni kupeleka ulimwengu wa kidijitali katika kila kona ya Tanzania kwa sababu mawasiliano yanafungua fursa kwa watu binafsi, biashara na jamii,” amesema Canton.
Amesema pamoja na kuimarisha mtandao, Yas imeanzisha mpango wa kuwawezesha wananchi kumiliki simu janja kwa kulipa kiasi kidogo cha awali na kukamilisha malipo kwa awamu za kila siku, zinazojumuisha huduma za sauti na intaneti.
Kwa mujibu wa Canton, hatua hiyo imechukuliwa baada ya kubaini kuwa gharama za simu janja bado ni kikwazo kikubwa kinachowazuia Watanzania wengi, hususan waishio vijijini, kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
“Pamoja na Tanzania kupiga hatua katika upanuzi wa huduma za 4G, umiliki wa simu janja bado uko chini ya kiwango kinachohitajika ili wananchi wengi wanufaike na huduma za kidijitali,” amesema.
Amesema changamoto hiyo imeongezeka kutokana na kupanda kwa bei za vifaa vinavyotumika kutengeneza simu duniani, hususan chipu za kielektroniki, kufuatia kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia za akili unde (AI).
Kutokana na hali hiyo, amesema kampuni hiyo pia inatafuta suluhisho kwa wakazi wa maeneo yasiyo na umeme, ikiwemo matumizi ya ‘power bank’ na vifaa vya kuchaji vinavyotumia nishati ya jua ili kuwawezesha wateja kutumia simu zao kwa urahisi.
Mbali na uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano, Yas imeendelea kupanua huduma zake za kifedha kidijitali, zikiwemo kuweka akiba, mikopo na vikundi vya kuweka na kukopa, pamoja na huduma za mawasiliano kwa biashara kupitia teknolojia za kisasa.
Katika hatua nyingine, kampuni hiyo imezindua awamu ya pili ya programu ya Anzia Ulipo, inayowapa fursa wajasiriamali na wabunifu wa teknolojia kuonyesha bidhaa na huduma zao, huku wakiunganishwa na masoko mapya.
Akizungumzia programu hiyo, Mkurugenzi wa Kanda ya Dar es Salaam Kusini wa Yas, Robert Kasulwa amesema lengo ni kuwawezesha vijana kutumia fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Amesema maboresho ya mtandao yamewawezesha wafanyabiashara wengi kutumia majukwaa ya kidijitali kufanya biashara saa 24 kwa siku, huku yakirahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na mawasiliano kwa wananchi.
Mmoja wa wanufaika wa awamu ya pili ya programu hiyo, Jerius Enrico kutoka Swahili Spark amesema ushirikiano na Yas umeongeza mwonekano wa kampuni yao na kuijengea uaminifu miongoni mwa wateja.
“Kupitia Yas tumepata nafasi ya kuonyesha ubunifu wetu katika maonesho ya Sabasaba, jambo ambalo limetupa fursa ya kufahamika na watu wengi zaidi. Pia jina la Yas linaaminika, hivyo hata sisi tunapata uaminifu zaidi kutoka kwa wateja,” amesema Enrico.