Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetahdharisha kuwa mji wa El-Obeid nchini Sudan, ambao ni makao makuu ya Jimbo la Kordofan Kaskazini, unaweza kukumbwa na hatima sawa na ile iliyoupata mji wa El Fasher katika jimbo jirani la Darfur Kaskazini iwapo mashambulizi yanayofanywa na wanamgambo wa kikosi cha Msaada wa Haraka, Rapid Support Forces (RSF) yataendelea.

IOM imetoa indhari hii jana Jumapili katika ujumbe wa video uliowekwa na shirika hilo kwenye mtandao wa kijamii wa X, ukimwonyesha Mohamed Refaat, Mkuu wa yjumbe wa shirika hilo nchini Sudan.

“Sote tuna wasiwasi kwamba El Obeid inaweza kuwa kama El Fasher… Tusipochukua hatua sasa, tutashuhudia El Fasher nyingine,” alisema Refaat.

Ameongeza kuwa zaidi ya watu 500,000 katika mji wa El-Obeid wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Mkuu wa Ujumbe wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji nchini Sudan amesema kuwa kundi la makao ya wakimbizi nchini Sudan, linaloongozwa na IOM, ni “mojawapo ya makundi yenye ufadhili mdogo zaidi nchini Sudan,” suala linalopelekea kupungua uwezo wake wa kutoa msaada kwa familia zilizoathiriwa.

Kwa takriban mwezi mmoja sasa mji wa, El-Obeid umekumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani za wanamgambo wa RSF dhidi ya kituo kikuu cha umeme cha mji huo, vituo vya mafuta na maeneo mengine ya raia, na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *