Shirikisho la Soka la Ubelgiji limeonyesha ghadhabu kubwa kufuatia uamuzi wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA,  kumruhusu mshambuliaji wa Marekani, Folarin Balogun, kushiriki katika mechi muhimu ya hatua ya 16 bora dhidi ya Ubelgiji siku ya Jumatatu, licha ya mchezaji huyo kuonyeshwa kadi nyekundu katika mzunguko uliopita.

Shirikisho la Soka la Kifalme la Ubelgiji (RBFA) lilisema siku ya Jumapili kuwa “limeshangazwa mno” na uamuzi huo, huku kocha mkuu wa Ubelgiji, Rudi Garcia, akimwaga lawama nzito dhidi ya chombo hicho kinachosimamia soka duniani.

Garcia ameashiria Julai  sherehe za ‘siku ya uhuru’ Marekani na kusema:  “Sikujua kuwa tarehe 5 Julai ndiyo Siku ya Wajinga (April Mosi) kwenye Kombe la Dunia. Ametoa kauli hiyo baada  FIFA kutangaza kuwa adhabu ya Balogun ya kukosa mechi moja imesimamishwa kwa muda wa majaribio wa mwaka mmoja.

Uamuzi huo unamfanya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 kuwa huru kucheza mechi hiyo ya mtoano ya Kombe la Dunia mwaka huu itakayopigwa Seattle siku ya Jumatatu.

RBFA imeeleza kuwa FIFA imejikita kwenye Kifungu cha 27 cha Kanuni za Nidhamu za FIFA kufanya uamuzi huo, lakini imesema kuwa Kifungu cha 66.4 cha kanuni hizo hizo kinaeleza wazi kuwa kadi nyekundu inamzuia mchezaji moja kwa moja kushiriki mechi inayofuata ya timu yake.

Vilevile, Wabelgiji wametaja Kifungu cha 10.5 cha Kanuni za Mashindano ya Kombe la Dunia la FIFA la 2026, kinachosema mchezaji yeyote anayetolewa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja au ya kadi mbili za manjano anakosa “moja kwa moja” mechi inayofuata.

RBFA imebainisha kuwa msisitizo huo wa kukosa mechi moja kwa moja ulithibitishwa tena katika Waraka Na. 16 wa Kombe la Dunia la FIFA 2026 uliosambazwa kwa mashirikisho yote wanachama mnamo Mei 12, na kurudiwa tena kwenye vikao vya maandalizi ya mechi na warsha za mashindano.

Shirikisho hilo lilieleza: “Ili kulinda haki za kisheria za timu zote zinazoshiriki na kulinda misingi mikuu ya mchezo wa kiungwana (fair play) katika mchezo wetu, iwe kwenye Kombe hili la Dunia la FIFA au kwenye mashindano yajayo, RBFA inachunguza njia zote zinazoweza kuchukuliwa.”

Gazeti la The New York Times limeripoti kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, alimpigia simu Rais wa FIFA, Gianni Infantino, siku ya Jumatano kuomba mapitio ya adhabu ya Balogun, likinukuu vyanzo vitatu vyenye uelewa wa mazungumzo hayo.

Baada ya Infantiono kumtii, Trump aliupongeza uamuzi huo wa FIFA kupitia mtandao wake wa Truth Social, akikaa na kuandika: “Asante kwa FIFA kwa kutenda haki, na kubatilisha dhuluma kubwa!”

Ikulu ya Marekani haijathibitisha iwapo Trump aliwasiliana na Infantino wala kujinasibu kuhusika na uamuzi huo.

Baadaye, mtandao wa Politico uliripoti kuwa Katibu wa Biashara wa Marekani, Howard Lutnick, alihusika kwenye mazungumzo ya chinichini na FIFA ili kusitisha adhabu ya kadi nyekundu ya Balogun, ukinukuu vyanzo viwili vilivyo karibu na suala hilo vilivyoomba hifadhi ya majina yao ili kuzungumzia masuala hayo ya faragha. Imedokezwa kuwa Lutnick amejenga uhusiano wa karibu sana na uongozi wa juu wa FIFA.

Uamuzi huu unaweka historia ya kuwa mara ya kwanza tangu mwaka 1962 kwa FIFA kumruhusu mchezaji aliyetolewa kwa kadi nyekundu kwenye Kombe la Dunia kucheza mechi inayofuata.

Balogun alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 64 wakati Marekani ilipoibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Bosnia na Herzegovina kwenye hatua ya 32 bora mnamo Julai 1, baada ya kumkanyaga vibaya beki wa Bosnia, Tarik Muharemovic, kwa nyuma wakati wakigombea mpira uliokuwa unadunda.

Mshambuliaji huyo wa Marekani ameshafunga mabao matatu kwenye mashindano haya, huku Marekani ikisaka nafasi yake ya kwanza ya kutinga robo fainali ya Kombe la Dunia tangu mwaka 2002.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *