Dar es Salaam. Huduma ya kubadilisha mfumo wa gari kutoka kutumia mafuta kwenda gesi, hautagharimu tena malipo ya fedha kwa mkupuo, baada ya kuanzishwa utaratibu wa mkopo wa kubadilisha mfumo huo.

Mkopo huo utakaotolewa na Benki ya Equity, utagharimia ubadilishaji wa mfumo wa gari, kisha mmiliki wa chombo hicho cha usafiri atatakuwa kulipa kidogokidogo kwa Benki hiyo.

Katika kutimiza hilo, Benki ya Equity mwishoni mwa wiki imesaini mkataba wa ushirikiano na kampuni ya Energo Tanzania Limited inayohusika na ubadilishaji wa mifumo ya magari kutoka kutumia mafuta hadi gesi asilia.

Ushirikiano huo, unakuja wakati Tanzania ikiendelea kuhamasisha matumizi ya gesi asilia kama nishati mbadala iliyo safi zaidi na yenye gharama nafuu kwa sekta ya usafirishaji.

Makubaliano hayo ya ushirikiano yamesainiwa wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba.

Kupitia ushirikiano huo, Equity Bank Tanzania itatoa uwezeshaji wa kifedha kwa wateja watakaokidhi vigezo ili kubadilisha magari yao kutumia gesi ssilia, huku Energo Tanzania Limited ikitoa huduma ya usambazaji na ufungaji wa mifumo.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkuu wa Kitengo cha Uendelevu wa Equity Bank Tanzania, Hellen Dalali, amesema ushirikiano huo unaakisi dhamira ya benki  kutoa suluhisho za kifedha zinazogusa mahitaji halisi ya wateja, huku zikichangia katika ajenda ya uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi.

“Tunaamini kuwa upatikanaji wa huduma za kifedha unapaswa kuwawezesha watu na biashara kuboresha maisha yao, kupunguza gharama za uendeshaji na kujenga ustahimilivu wa muda mrefu,” amesema.

Amesema ushirikiano huo, una dhima ya kuwawezesha kifedha wamiliki wa vyombo vya usafiri na wafanyabiashara wadogo hususan vijana kuanza kutumia mifumo ya gesi asilia kuwa rahisi na nafuu zaidi.

“Kwa kufanya hivyo, tunawasaidia wateja kupunguza gharama za mafuta, kuboresha mzunguko wa fedha na kuchangia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa,” amesema.

Amesema ushirikiano huo unaendana na ajenda pana ya Equity Bank katika uendelevu na maendeleo ya biashara, inayolenga kuwasaidia wateja kukua.

Kupitia mpango huo, amesema wateja watakaokidhi vigezo watagharamiwa ubadilishaji wa magari yao kutoka matumizi ya petroli au dizeli kwenda matumizi ya gesi asilia.

“Huduma hii inalenga zaidi wateja wa sekta ya usafirishaji, wakiwemo madereva wa teksi, wamiliki wa magari mengi, pamoja na wateja wengine ambao shughuli zao za kila siku zimekuwa zikiathiriwa na gharama za mafuta,” amesema.

Amesema mpango huo, umebuniwa kupunguza mzigo wa kulipa gharama zote za ubadilishaji kwa mara moja, badala yake, wateja wanaostahili watapata mikopo ya mali kupitia Equity Bank na kurejesha kwa awamu kwa kipindi kitakachokubaliwa.

Amesema mkopo huo wa muda mfupi hadi miezi 12, unalenga kusaidia wamiliki wa teksi, wamiliki wa magari mengi na wafanyabiashara wanaostahili kufunga mifumo ya Gesi Asilia na kurejesha mkopo kupitia akaunti zao za uendeshaji.

“Bidhaa hii inatoa manufaa kadhaa ya moja kwa moja kwa wateja. Inawasaidia wamiliki wa magari kupunguza gharama za mafuta, kuboresha mtiririko wa fedha wa kila siku na kuhakikisha biashara zinaendelea bila kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na kupanda kwa gharama za uendeshaji,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Energo Tanzania Limited, Kahema Mziray, amesema ushirikiano huo utasaidia kuharakisha matumizi ya mifumo ya Gesi Asilia kwa kuunganisha utaalamu.

“Sisi tumejikita katika kuunga mkono safari ya Tanzania kuelekea matumizi ya nishati safi na yenye gharama nafuu. Kupitia ushirikiano huu na Benki ya Equity, wamiliki wengi zaidi wa magari wataweza kupata huduma bora za kubadilisha magari Kwenda Gesi Asilia zikiambatana na mkopo unaopunguza mzigo wa gharama za awali,” amesema.

Amesema ushirikiano huo unaunganisha teknolojia, fedha na huduma kwa wateja kwa namna inayoweza kuleta matokeo chanya kwa watoa huduma za usafiri na wafanyabiashara wadogo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *