
Dar es Salaam. Muungano wa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani (Organization of the Petroleum Exporting Countries Plus -OPEC+) umeafikiana kuongeza uzalishaji wa mafuta kwa mapipa 188,000 kwa siku kuanzia mwezi Agosti 2026, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa mafuta na kushuka kwa bei katika soko la kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya OPEC na ripoti za mashirika ya habari ya kimataifa ikiwemo Reuters, Deutsche Welle (DW) na Associated Press (AP), uamuzi huo umefikiwa katika mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao jana Jumapili, Julai 5, 2026, ukihusisha nchi wanachama wakuu wa muungano huo.
Nchi zilizoshiriki katika uamuzi huo ni pamoja na Saudi Arabia, Russia, Iraq, Kuwait, Kazakhstan, Algeria na Oman, ambazo kwa pamoja zimeendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika kusimamia mwelekeo wa uzalishaji wa mafuta duniani.
OPEC ni muungano wa nchi wazalishaji wa mafuta ulioanzishwa mwaka 1960 kwa lengo la kuratibu sera za uzalishaji na kuhakikisha bei ya mafuta inabaki katika kiwango kinachoweza kutabirika.
Baadaye, muungano huo uliungana na washirika wake wakubwa na kuunda mfumo wa OPEC+, unaoratibu uzalishaji kwa njia ya mgawo wa kila nchi mwanachama ili kuleta uwiano wa soko la dunia.
Kwa mujibu wa taarifa ya OPEC, ongezeko hili la uzalishaji ni mwendelezo wa hatua za muda mrefu zilizoanza Juni 2026, ambapo muungano huo ulianza kurekebisha baadhi ya vikwazo vya uzalishaji vilivyowekwa mwaka 2023.
Lengo kuu ni kurejesha usawa wa soko baada ya kipindi cha bei kupanda kwa kasi kutokana na upungufu wa mafuta katika soko la dunia.
Katika miaka ya hivi karibuni, soko la mafuta limeathiriwa kwa kiasi kikubwa na vita vya Ukraine, vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi, pamoja na machafuko ya kisiasa Mashariki ya Kati.
Migogoro hiyo imesababisha usumbufu katika minyororo ya usambazaji wa nishati duniani na kusababisha bei ya mafuta kupanda kwa kasi katika masoko ya Ulaya, Asia na Afrika.
Hali ya usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayopitisha takribani theluthi moja ya mafuta ya dunia, ilifungwa na sasa imeanza kurejea katika hali ya utulivu, jambo ambalo limeongeza matarajio ya kushuka kwa bei ya mafuta katika miezi ijayo.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwezi Juni ya Mamlaka ya Kimataifa ya Nishati (IEA), uzalishaji wa mafuta duniani kwa sasa ni mapipa milioni 102.4 kwa siku.
Ongezeko la mapipa 188,000 lililopendekezwa na OPEC+ litafanya uzalishaji kufikia mapipa milioni 102.588 kwa siku, sawa na ongezeko la asilimia 0.184.
Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Prince Abdulaziz bin Salman, amenukuliwa akieleza msimamo wa nchi yake kuhusu mwelekeo wa soko la mafuta, akisisitiza kuwa OPEC+ inaendelea kuchukua tahadhari katika kurekebisha uzalishaji ili kuepuka mshtuko wa bei katika soko la dunia.
“Hatua hii ni ya kurejesha usawa wa soko bila kuvuruga uthabiti wa bei,” amesema Prince Abdulaziz bin Salman, akisisitiza muungano huo utaendelea kufuatilia hali ya mahitaji ya mafuta duniani kabla ya hatua nyingine kubwa kuchukuliwa.
Kwa upande wa Urusi, mamlaka zake za nishati zimeeleza kuwa soko la mafuta linaanza kuonyesha utulivu baada ya kipindi cha misukosuko ya kijiopolitiki na kiuchumi iliyochochea kupanda kwa bei katika miaka ya hivi karibuni.
“Soko linaonyesha dalili za utulivu, na ongezeko la uzalishaji halilengi kushusha bei kwa kasi bali kuzuia upungufu wa ghafla wa mafuta duniani,” amesema Alexander Novak, Naibu Waziri Mkuu wa Urusi anayehusika na nishati, akifafanua msimamo wa Moscow ndani ya OPEC+.
Wakati huohuo, wachambuzi wa masoko ya nishati wamesema hatua ya kuongeza uzalishaji inaweza kuongeza shinikizo la kushuka kwa bei ikiwa mahitaji ya mafuta katika masoko makubwa ya Asia na Ulaya yatabaki tulivu katika miezi ijayo.
Wanasema ongezeko la mapipa 188,000 kwa siku linaweza kuonekana dogo lakini lina athari kubwa katika soko ambalo linategemea uwiano kati ya mahitaji na uzalishaji.
Hata hivyo, wataalamu wa masoko ya nishati wanasema mwelekeo wa bei utaendelea kutegemea mambo kadhaa ikiwemo kasi ya mahitaji ya mafuta kutoka China na Marekani, hali ya kisiasa Mashariki ya Kati, pamoja na utekelezaji wa sera za uzalishaji ndani ya OPEC+.
Kwa upande mwingine, baadhi ya nchi ikiwemo Iraq zimeendelea kushinikiza kuongezewa kiwango cha uzalishaji, huku baadhi ya wanachama ikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wakionyesha mabadiliko ya sera katika mfumo wa mgawo wa uzalishaji, hali inayoashiria mwelekeo mpya wa OPEC+ kuelekea soko lenye ushindani zaidi hatua inayoweza kuongeza shinikizo kushuka kwa gharama za nishati hiyo.