
Kigoma. Wakati kesi ya uchaguzi inayomkabili nbunge wa Kigoma mjini, Clayton Revocatus Chipando, maarufu Baba Levo ikitarajiwa kuanza kusikilizwa ushahidi leo Jumatatu, Julai 6, 2026, Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, imekumbana tena na mapingamizi.
Mapingamizi hayo yameibuliwa na mawakili wa walalamikiwa. Walalamikaji katika kesi hiyo wameanza kutoa ushahidi asubuhi unaolenga kuthibitisha madai yao dhidi ya mbunge huyo.
Baba Levo alitangazwa mbunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akimshinda mpinzani wake mkubwa kutoka ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Hata hivyo, wananchi wanne- Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali walifungua kesi dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), mbunge huyo Chipando na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wakipinga uchaguzi huo.
Katika kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025 wadai hao waliojitambulisha kuwa wapiga kura katika jimbo hilo wanadai uchaguzi huo uligubikwa na kasoro nyingi.
Wanabainisha kasoro hizo ni pamoja na ukiukwaji wa taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi, vitendo vya rushwa na udini vilivyooneshwa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.
Hivyo wanaiomba mahakama hiyo pamoja na mambo mengine iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.
Mapingamizi
Wakili wa Serikali, Erigh Rumisha kwa niaba ya jopo la mawakili sita wa Serikali wanaowawakilisha mlalamikiwa wa kwanza, AG na wa wa tatu, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini amedai walalamikiwa wameshindwa kutekeleza matakwa ya kanuni na amri ya Mahakama.
Wakili Rumisha amedai mara ya mwisho kesi hiyo ilipoitwa walalamikiwa walikuwa wameshindwa kuwasilisha mahakamani maelezo ya maandishi ya mashahidi, hivyo wakaiomba mahakama ikawaamuru wawasilishe mahakamani maelezo hayo kwa mujibu wa sheria na ikapanga kesi kusikilizwa leo.
Hata hivyo, Wakili Rumisha amedai hata leo walalamikiwa wameshindwa kuwasilisha mahakamani maelezo hayo ya maandishi ya mashahidi, kwani hawajafuata utaratibu uliowekwa badala yake wametumia utaratibu wa kwao.
Akirejea uamuzi wa Mahakama hiyo katika baadhi ya mashauri, amedai amri za mahakama lazima zitimizwe.
Hata hivyo, amesema kanumi ya 20 (1) na 24 za Kanuni za Uwasilishaji wa Mashauri Kielektroniki katika Mfumo wa Mahakama zimeweka utaratibu mbadala nje ya utatstibu huo.
Wakili Rumisha amedai hata utaratibu huo pia haukufuatwa.
“Hivyo amri ya mahakama haikufuatwa na utaratibu wa mahakama haukufuatwa,” amesema walili Rumisha.
Amefafanua kwa mujibu wa amri ya Mahakama ya Juni 18, 2026 maelezo hayo yalipaswa kuwasilishwa mahakaamani si zaidi ya Julai 4, 2026 kabla ya saa 3:00 asubuhi, lakini mpaka muda huo wao walikuwa hawajazipata nyaraka hizo kwa mujibu wa utaratibu.
Amedai badala yake alipokea barua pepe ya mawasiliano baina ya wakili wa walalamikaji na msajili akimweleza alikuwa amepata changamoto na kwamba msajili alimwelekeza ajitahidi kuwasilisha kama amri ya mahakama ilivyoelekeza.
Wakili Rumisha amedai hata kama kuna exemption, lazima isiwe nje ya sheria ambayo ni Kanuni ya 24(5) ya Uwasilishaji wa Mashauri kwa Kielektroniki, ambayo inasema isizidi saa za kazi.
Wakili Rumisha amedai siku hiyohiyo ambayo wakili wa walalamikaji amedai kulikuwa na changamoto ya mfumo, wao waliwasilisha nyaraka na mapingamizi.
“Kwa hiyo, tunasisitiza walalamikaji wameshindwa kutekeleza amri ya mahakama na kanuni. Hivyo tunaomba nyaraka hizo zisipokewe na na shauri hili litupiliwe mbali,” amesema.
Hoja hiyo imeungwa mkono na mmoja wa mawakili wa Baba Levo, Thomas Msasa aliyeongeza kuwa nyaraka hizo za maelezo ya mashahidi zinaonesha kuwa zimewasilishwa Julai 6, 2026, hivyo ni nje ya muda na kinyume cha Kanuni ya 21(2), inayotaka maelezo hayo yawasilishwe saa 48, kabla ya tarehe na muda wa usikilizwaji kesi.
Wakili Msasa amedai kwa mujibu wa barua pepe waliyoipata walijaribu kuwasilisha nyaraka hizo Julai 4 ambayo si siku ya kazi na kwamba katika barua pepe hiyo msajili alisisitiza ajitahidi kutekeleza amri ya Mahakama.
Amedai badala yake waliwasilisha nyaraka hizo kwa njia ya barua pepe ambayo pia licha ya kwamba ziliwasilishwa nje ya utaratibu, lakini pia ilikuwa nje ya muda kwani ilitarajiwa ziwasikishwe kabla ya saa tatu, lakini ziliwasilishwa baada ya muda huo.
Amedai kwa msingi huo, maelezo ya mashahidi yamewasilishwa nje ya kanuni na kwamba mawasiliano ya barua pepe kati ya walalamikaji na msajili haziko ndani ya Kanuni za Mahakama za Uwasilishaji Mashauri Kielektroniki.
“Kwa hiyo, Mheshimiwa tunaomba ionekane walalamikaji wameshindwa kuwasilisha maelezo ya maandishi ya mashahidi wao kwa mujibu wa kanuni. Kwa hiyo ni maombi yetu maelezo ya mashahidi wote 16 yamewasikishwa nje ya kanuni na kesi itupiliwe mbali,” amedai.
Katika kesi hiyo upande wa walalamikaji unatarajiwa kuwa na mashahidi wasiopungua 20 na kuwasilisha vielelezo vya nyaraka ngumu vyenye kurasa 180 na vielelezo vya kielektroniki yaani picha jongefu (video) 60.
Kabla ya kufikia hatua ya usikilizwaji ushahidi, kesi hiyo ilipitia katika mvutano mkali kutokana na mapingamizi ya mara kwa mara yaliyokuwa yakiibuliwa na Serikali na Baba Levo wakitaka iitupilie mbali wakidai kuwa imegubikwa na kasoro mbalimbali za kisheria.
Hata hivyo, jitihada za wadaiwa hao kutaka kuimaliza kesi hiyo kwa mbinu za kiufundi, kupitia mapingamizi ya awali ya hoja za kisheria zimegonga mwamba, kwani mara kadhaa mahakama imekuwa ikiyakataa.
Kutokana na mvutano huo, muda wa awali wa usikilizwaji wa kesi za uchaguzi yaani ndani ya miezi sita uliisha kabla haijaanza kusikilizwa.
Hivyo imemlazimu Jaji Mkuu, George Masaju kwa mamlaka aliyo nayoi kisheria kuongeza muda wa miezi sita ya usikilizwaji wa kesi hiyo.
Baada ya kupenya katika mapingamizi hayo, hatimaye Jumatatu, Juni 15, 2026 kesi hiyo iliingia katika hatua ya usikilizwaji wa awali ikiwa ni maandalizi ya usikilizwaji kamili.
Katika hatua hiyo, wadaiwa walisomewa muhtasari wa madai ya kesi hiyo na kisha wakatakiwa kubainisha mambo au hoja wanazokubaliana nazo na zile wasizokubaliana nazo katika maelezo hayo, ambazo hizo ndizo upande wa wadai watakuwa na wajibu wa kuzithibitisha.
Wakili alivyojibu Mapingamizi
Akijibu hoja hizo wakili John Seka amedai ni kweli nyaraka hizo zilipaswa kuwasilishwa kabla ya saa 3:00 Jumamosi, Julai 4, 2026 na kwamba hoja ya Wakili Msasa kuwa tarehe hiyo haikuwa siku ya kazi haina msingi, kwani mahakama ndio ilielekeza nyaraka hizo ziwasikishwe tarehe hiyo.
“Kwa hiyo hakukuwa na kosa lolote endapo nyaraka hizo zingewasilishwa siku ya Jumamosi kwani ilikuwa ni kwa mujibu wa amri ya mahakama hii,” amesema wakili Seka.
Wakili Seka amedai baada ya kukamilisha kuandaa maelezo ya mashahidi hao alianza kuzipakia katika mfumo wa mahakama, lakini siku hiyo ya Ijumaa Mfumo wa Mahakama ulikuwa haufanyi kazi.
Amedai baada ya kufika Jumamosi na Mfumo wa Mahakama ukiwa haufanyi kazi aliwasiliana na Naibu Msajili aliyedai naye ana taarifa za changamoto za mfumo na kwamba changamoto hiyo haiko katika masjala ya Kigomanpekee, bali ni tatizo la kitaifa.
Wakili Seka amesema Naibu Msajili alimwelekeza afanye mawasiliano na makao makuu naye akawasiliana na Desdery Kamugisha, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri aliyemweleza wanalifahamu tatizo hilo na akaomba dakika 20 na kwamba zikiisha watatoa maelekezo kwa Msajili.
Wakili Seka amesema baada ya dakika 20, Kamugisha alimpigia akamwambia tatizo lililopo haliwezi kuisha kabla ya saa 3:00 na kwamba awasiliane na Naibu Msajili Kigoma kwa barua pepe rasmi za mahakama, kwani ameshamtaarifu.
Hivyo saa 2:26 Julai 4, 2026 alituma barua pepe kwa Naibu Masjala ya Kigoma akieleza changamoto anayoipitia na watu wote aliwasiliana nao na maelekezo aliyopewa.
Pia kwa kuongozwa na busara alituma barua pepe hiyo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na kwa wakili Msasa ili nao wawe na taarifa ya kinachoendelea.
Amedai saa 2:36 Naibu Msajili alimjibu maombi kwa kuwasilisha nyaraka hizo nje ya utaratibu wa kawaida yamekubalika na katika barua pepe hiyo alikiri kuna tatizo la mfumo na kwamba ameelezwa na Kamugisha na hawezi kumhakikishia kuwa litatatuliwa lini.
Wakili Seka amedai barua pepe hiyo alimtumia yeye Seka pekee, lakini baada ya kugundua hilo alituma barua pepe nyingine saa 4:56 Julai 4, 2026 ambapo pia aliwanakilisha Wakili Mkuu wa Serikali na wakili Msasa.
Amesema katika barua hiyo alimwelekeza atume nyaraka hizo kwa barua pepe na kwamba mfumo utakapotengamaa aziwasilishe.
“Saa 2:58 Julai 4,2026 mimi wakili wa walalamikaji nilituma kwa njia ya barua pepe maelezo ya mashahidi 16,” amesema nyaraka hizo pia zilikwenda Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na kwa wakili Msasa na pia kwa Jaji, huku akiahidi kuwa mfumo utakaporejea atawasilisha kama alivyoelekezwa.
Amesema Naibu Msajili alimjibu saa 3:02 kuwa amezipokea ndani ya muda.
Wakili Seka amesema baada ya kuwasilisha nyaraka hizo alipopata taarifa kuwa mfumo umerejea siku hiyohiyo aliwasilisha kwenye mfumo Julai 4, 2026 kama mahakama ilivyoelekeza na si Julai 6, 2026 kama Wakili Msasa alivyodai.
Amedai sheria inayosimamia uwasilishaji mashauri kwa kielektroniki kwa maombi ya mdomo Msajili anaweza kusamehe uwasilishaji kwa mfumo panapokuwa na changamoto kama vile upatikanaji wa mfumo.
“Kwa hiyo mheshimiwa Jaji nitakushawishi ukubaliane nami kuwa nilikidhi matakwa ya kanuni ya 20 (1,” amedai wakili Seka na kusisitiza kanuni hizo zinasema muda ambao mfumo ulikuwa haupatikani hautahesabika.
Hata hivyo, wakili Rumisha amedai bado wanasisitiza pingamizi lao, kwani hata huo msamaha wa Naibu Msajili aliousema haupo na unatakiwa uwe kwa mujibu wa kanuni ya 20, maandishi lakini kinachoonekana Msajili alimsisitiza afanye kila analoweza atekeleze amri ya mahakama.
Pia amedai wakili Seka hajaeleza nini alikifanya tangu alipopewa nyongeza ya muda mpaka akaja kufukuzana siku hiyo ya changamoto ya mfumo.
Amesisitiza siku hiyohiyo ambayo wakili Seka alisema kulikuwa na tatizo la mfumo, wao waliwasilisha nyaraka na mapingamizi yao.
Wakili Msasa amesisitiza kuwa kanuni zinaelekeza kunapokuwa na changamoto kuwasilisha maombi kwa njia ya mdomo na si kwa barua pepe na kwamba maombi hayo yanapaswa kufanyika ndani ya muda wa kazi.
Pia wakili Msasa amesema licha ya wakili Seka kudai aliwasiliana na kina Desdery, lakini hakuna kiapo chao kinachoonesha kuwa kweli kulikuwa na tatizo la mfumo na lilianza lini.
Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea katika kesi hii