- Jinamizi baya zaidi kwa familia moja lilibadilika kwa njia ya kushangaza baada ya mtoto wao, ambaye alikuwa ametangazwa kufariki na madaktari, kupatikana akipumua kwenye chumba cha kuhifadhi maiti hospitalini
- Vincent Lorenzo mwenye umri wa miezi 18 alipatikana akielea kifudifudi kwenye bwawa la kuogelea la familia yake
- Saa tano baadaye, wahudumu wa hospitali walipoenda kuchukua mwili wake kutoka kwenye chumba cha kuhifadhi maiti, walimkuta akiwa bado anapumua
Mtoto wa miezi 18 kutoka jimbo la Arizona, Vincent Lorenzo Fiordilino, ambaye alitangazwa kufariki baada ya tukio la karibu kuzama majini, aliwashangaza wahudumu wa hospitali na wachunguzi baada ya kupatikana akiwa bado anapumua kwenye mochari baada ya saa tano tangu kutangazwa kuwa amefariki.

Source: UGC
Kisa cha Vincent kimezua uchunguzi kuhusu mazingira yaliyosababisha karibu azame na maamuzi ya kitabibu yaliyofanywa baada ya kupelekwa hospitalini.
Ingawa mtoto huyo hatimaye alinusurika na tangu wakati huo ameruhusiwa kutoka hospitalini, bado kuna maswali kuhusu jinsi alivyotangazwa kufariki ilhali bado alikuwa anaonyesha dalili za uhai.
Jinamizi la familia
Tukio hilo lilitokea jioni ya siku ya Super Bowl Sunday, wakati Vincent alipatikana akielea kifudifudi kwenye bwawa la kuogelea la familia yao.
Simu ya dharura ilipigwa majira ya saa 5:38 jioni, baada ya ndugu zake kumkuta mtoto huyo na kujaribu kumfufua kwa kutumia huduma ya CPR kabla wahudumu wa dharura kufika.
Alipelekwa kwa haraka katika Mercy Gilbert Medical Centre, ambako wahudumu wa idara ya dharura waliendelea na juhudi za kuokoa maisha yake.
Hata hivyo, zaidi ya nusu saa baadaye, madaktari walihitimisha kuwa hawakuweza kumuokoa.
Majira ya saa 6:20 jioni, Vincent alitangazwa rasmi kuwa amefariki.
Kwa familia yake, ilionekana kuwa huo ulikuwa mwisho wa kusikitisha wa maisha ya mtoto wao mdogo.
Wasiwasi kuhusu dalili za uhai
Hata hivyo, karibu mara moja baadhi ya waliokuwepo walianza kuona kile walichoamini kuwa ni dalili kwamba mtoto huyo alikuwa bado anapumua.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, wanafamilia na maafisa waliokuwa hospitalini walimwona mtoto huyo akifanya mienendo iliyofanana na kuvuta pumzi hata baada ya kutangazwa kuwa amefariki.
Inadaiwa kuwa mpelelezi mmoja alisikia tena sauti ya mtoto akivuta pumzi majira ya saa 7:18 jioni, wakati wahudumu wa hospitali walipokuwa wakijiandaa kuhamisha mwili wake kwenda kwenye chumba cha baridi kinachotumika kuhifadhi maiti.
Wakati wasiwasi huo ulipoibuliwa, wahudumu wa hospitali walieleza kuwa harakati hizo zilikuwa “agonal breathing”, yaani kuvuta pumzi kusiko hiari kunakoweza kutokea baada ya mtu kufariki.
Baadaye, mpelelezi huyo alisema aliona harakati kama hizo tena alipokuwa akipiga picha za mwili.
Muda mfupi baadaye, mlango wa chumba cha kuhifadhi maiti ulifungwa.
Ugunduzi wa kushangaza kwenye chumba cha kuhifadhi maiti
Zaidi ya saa nne baadaye, majira ya saa 11:52 usiku, timu ya mchunguzi wa maiti ilifika kuchukua mwili wa mtoto huyo.
Kilichotokea baadaye kilimshangaza kila mtu.
Badala ya kuandaa usafirishaji wa mwili wa mtoto aliyefariki, walimkuta Vincent akiwa bado anapumua.
Familia yake iliarifiwa mara moja, na mtoto huyo akasafirishwa kwa ndege kwa matibabu ya dharura.
Ugunduzi huo wa ajabu ulibadilisha kile kilichoonekana kuwa janga na kuwa simulizi ya kuokoka.
Kwa mujibu wa ukurasa wa kuchangisha fedha ulioanzishwa na ndugu zake, Vincent amenusurika bila kupata uharibifu mkubwa wa ubongo, ingawa bado anahitaji tiba ya muda mrefu pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa kitabibu.
Inaripotiwa kuwa anaendelea kupumua kwa msaada wa mashine ya kumsaidia kupumua (ventilator).
Ripoti ya polisi inamtaja daktari wa idara ya dharura aliyemtangaza mtoto huyo kufariki kuwa ni Dkt. A. Toosi.
Maswali kuhusu hatua za hospitali
Afisa mmoja wa polisi alihoji uamuzi wa daktari huyo baada ya kuona kile kilichoonekana kuwa mtoto huyo alikuwa bado anapumua.
Daktari huyo alijibu:
“Tafadhali fanya kazi yako, nami niruhusu nifanye kazi yangu. Nilisoma udaktari kwa sababu.”
Mercy Gilbert Medical Center imethibitisha kuwa ilifanya uchunguzi wa ndani kuhusu kile ilichokiita “hali ya kuhuzunisha.”
Hata hivyo, hospitali hiyo haijaweka hadharani matokeo ya uchunguzi huo wala kutoa maoni kuhusu ikiwa daktari huyo bado anaendelea kufanya kazi hapo.
Wakili anayemwakilisha daktari huyo alisema:
“Kuna mengi zaidi kuhusu kesi hii, kwa upande wa ukweli na masuala ya kitabibu, kuliko yale yaliyoripotiwa hadi sasa,” lakini alikataa kutoa maelezo zaidi.
Wazazi nao wachunguzwa
Wakati hatua za hospitali zikichunguzwa, wachunguzi pia wanaangazia mazingira yaliyosababisha mtoto huyo karibu kuzama.
Wachunguzi wanaamini huenda wazazi hawakutambua kuwa mtoto wao alikuwa ametoka na kuelekea kwenye bwawa la kuogelea kwa sababu uwezo wao wa kufanya maamuzi huenda ulikuwa umeathirika.

Pia soma
Mwanamke adai aliteseka Jehanamu kwa siku 18, akafichua aliyoyaona kabla ya kuamka hospitalini
Kwa sasa, kunusurika kwa Vincent ndiko kunakoendelea kuwa kitovu cha kesi iliyovutia hisia za umma.
Kilichoanza kama tukio la kusikitisha la karibu kuzama kilibadilika na kuwa fumbo la ajabu la kitabibu baada ya mtoto aliyeaminika kufariki kupatikana akiwa hai kwenye chumba cha kuhifadhi maiti saa kadhaa baadaye.
Mtoto mchanga afariki ndani ya gari lililofungwa
Katika habari nyingine yenye mwisho wa kusikitisha, baba mmoja alivunjika moyo baada ya mwanawe wa miezi 18 kufariki ndani ya gari lililokuwa limefungwa.
Safari ya kawaida ya kwenda kumchukua mtoto kutoka kituo cha kulelea watoto iligeuka kuwa jinamizi kubwa baada ya mwanaume huyo kugundua kosa lake kubwa.
Yote yalianza alipomsahau mtoto huyo na kushindwa kumpeleka katika kituo cha kulelea watoto, kisha akamsahau ndani ya gari. Aliporudi kwenye gari, mtoto alikuwa tayari amefariki.
Read: ENGLISH VERSION
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.
Chanzo: TUKO.co.ke


