
Mamlaka nchini Tanzania zimewakamata watu kadhaa wanaodaiwa ni wahusika wa kuandaa maandamano yanayotarajiwa hivi leo.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Tangu baadhi ya wanaharakati watangaze kutakuwa na maandamano siku ya sikukuu ya Saba Saba, mamlaka zimekuwa zikitekeleza operesheni dhidi ya wakosoaji wa Serikali wanaodai mabadiliko ya mfumo wa demokrasia na haki nchini humo.
Tayari maandamano ya hivi leo yalipigwa marufuku na Serikali, ambapo jeshi la polisi nchini humo lilionya dhidi ya wale wanaopanga kuandamana na kufanya vurugu, watu kadhaa wakiripotiwa kukamatwa kwa tuhuma za kupanga vurugu.
Kwa mujibu wa vipeperushi vilivyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii nchini humo, maandamano ya hivi leo ikiwa yatafanyika, yanalenga kupinga vitendo vya utekaji na mauji pamoja na kuminywa kwa demokrasia.
Kwa zaidi ya majuma mawili, ulinzi mkali ulikuwa umewekwa kwenye miji mikubwa, ambapo polisi wenye silaha wamekuwa wakifanya doria, huku pia juma lililopita Serikali kupitia kwa waziri wa mambo ya ndani, alitangaza kupiga marufuku mikutano ya kisiasa.
Baadhi ya raia waliozungumza na vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa, wameeleza kuwa na hofu ya kujitokeza barabarani kutokana na kilichotokea wakati wa maandamano ya Octoba 29 mwaka jana, ambapo watu zaidi ya 500 waliuawa.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya ndani na nje ya nchi ya Tanzania, yametoa wito kwa mamlaka kuheshimu uhuru wa watu kutoa maoni, wakiukosoa utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan kushindwa kulinda haki za binadamu, madai ambayo mamlaka nchini humo zimeendelea kukanusha.