
Shirika la kutetea hazi za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limetangaza kuwa, mamlaka za kikanda katika eneo la kaskazini mwa Tigray nchini Ethiopia zimekuwa zikiwateka nyara na kuwaajiri raia kinyume cha sharia hasa watoto wenye umri wa miaka 15, tangu Aprili 2026.
Harakati ya kuajiri watu kwa kulazimisha inafuatia miezi kadhaa ya mvutano unaoongezeka kati ya serikali ya shirikisho ya Ethiopia na Tigray People’s Liberation Front (TPLF).
Katika taarifa iliyotolewa jana 6 Julai 2026, shirika hilo lilisema kwamba, jamii katika miji na vijiji zinasema vikosi vya jeshi na maafisa wa Tigray wanawakamata wapiganaji wa zamani, wanaume na wavulana kutoka mitaani, ofisini, majumbani wakati wa upekuzi wa usiku, na maeneo ya kuchimba dhahabu.
“Kampeni ya mamlaka ya Tigray ya kuwaajiri wanaume na wavulana kwa nguvu katika vikosi vyao inazusha hali ya hofu katika eneo lote,” anasema Laetitia Bader, naibu mkurugenzi wa Afrika wa HRW.
“Mamlaka inapaswa kukomesha kampeni yao mara moja na kuwaruhusu wale walioajiriwa kinyume cha sheria kurudi nyumbani.”
Human Rights Watch imesajili visa sita vya kulazimishwa kuajiriwa kupitia mahojiano ya mbali na watu 18 mwezi Juni, wakiwemo mashahidi, jamaa za wapiganaji walioandikishwa jeshini, na wale waliotoroka baada ya kutekwa nyara.
Waliohojiwa wamesema kuwa msako mkubwa uliongezeka mwishoni mwa Aprili, huku mamlaka za mitaa zikitumia orodha ya wapiganaji wa zamani na watoa taarifa wa maeneo ili kuwatambua wapiganaji walioandikishwa jeshini.
Inaripotiwa kwamba wapiganaji wapya walishikiliwa katika ofisi za utawala, magereza, au shule kabla ya kuhamishiwa kwenda kwenye kambi za kijeshi kaskazini magharibi na kusini mwa Tigray.