Taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) iliyotolewa leo mjini London Uingereza inasema Katibu Mkuu wa shirika hilo, Arsenio Dominguez, ametoa wito wa hatua za haraka za kimataifa kuhakikisha mabaharia hao wanaachiliwa salama.

Kwa mujibu wa IMO, mabaharia hao wanazuiliwa ndani ya meli tatu, MT Honour 25, Eureka na Sward, zilizotekwa kati ya Aprili na Mei katika pwani ya Somalia na Ghuba ya Aden. Shirika hilo linaeleza kuwa mabaharia hao wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na maji pamoja na vitisho vya ukatili.

Dominguez ataka hatua za pamoja

Akihutubia kikao cha 137 cha Baraza la IMO mjini London Uingereza, Dominguez amesema, “Matukio haya ni ukumbusho wazi kwamba tishio la uharamia na ujambazi wa kutumia silaha dhidi ya mabaharia halijapungua, na linaendelea kuhitaji umakini pamoja na hatua za pamoja za kimataifa. Ninaomba muunge mkono juhudi za kuhakikisha wanaachiliwa salama.”

Amesema IMO itaendelea kushirikiana na nchi wanachama na wadau wa sekta ya usafirishaji wa baharini kuhakikisha mabaharia hao wanaachiwa huru, huku akiwataka waendeshaji wa meli kuzingatia kikamilifu hatua za usalama kabla ya kupitia maeneo hatarishi.

Mashambulizi yaongezeka

IMO imesema katika miezi mitatu iliyopita kumerekodiwa matukio 24 ya uharamia na ujambazi dhidi ya meli katika Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden. Aidha, matukio hayo duniani yaliongezeka kwa asilimia 17 kati ya mwaka 2024 na 2025, kutoka matukio 146 hadi 171.

Shirika hilo litaendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia Kanuni ya Mwenendo ya Djibouti, Marekebisho ya Jeddah na Mradi wa Bahari ya Shamu, ili kuboresha usalama wa baharini na kulinda njia muhimu za usafirishaji duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *