
Misafara ya mazishi ya mwili wa Ayatollah Khamenei, Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi, imefanyika kwa kishindo katika mji mkuu Tehran na katika miji mitakatifu ya Qom nchini Iran, na Najaf na Karbala nchini Iraq, ikihudhuriwa na mamilioni ya watu wa nchi mbili hizi na vile vile wa nchi nyingine za eneo.
Kushiriki mamilioni ya watu katika mazishi haya kunatoa ujumbe muhimu sana. Mojawapo ya jumbe muhimu zaidi ni imani thabiti ya wananchi wa Iran kwamba kiongozi huyo aliyeuawa shahidi alijitolea maisha yake yote kwa ajili ya kulinda Uislamu, Mapinduzi na heshima ya Iran ya Kiislamu. Mahudhurio haya makubwa ya umma ni ishara ya shukrani kwa juhudi zisizo na kikomo zilizofanywa na kiongozi huyo kwa ajili ya Uislamu na Iran, juhudi alizozidhamini kwa maisha yake mwenyewe na ya wanafamilia wake. Ujumbe mwingine muhimu uliotolewa na mahudhurio ya mamilioni ya watu katika msafara wa mazishi ya kiongozi huyo adhimu wa Mapinduzi ni sisitizo linalotolewa kwa ajili ya kuendeleza njia na fikra zake katika awamu mpya. Kwa hakika, uwepo huu mkubwa wa umma unaonyesha kwamba, licha ya mashinikizo na vitisho vyote vinavyotolewa na maadui, lakini taifa la Iran bado limesimama imara na liko thabiti katika kulinda maadili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Katika muktadha huu, Reuters imeelezea mazishi ya Imam Shahidi, Ayatollah Seyyed Ali Khamenei, kama tukio kubwa na muhimu kuliko mazishi ya kawaida ya kitaifa, ambalo linaashiria kuendelea mapambano ya Iran na kudhihiri nguvu yake mpya kieneo na kimataifa. Shirika la habari la Uingereza BBC, limesema kuwa “mafuriko ya waombolezaji” mjini Tehran yalituma ujumbe wa wazi kwa Marekani na Israeli kwamba juhudi zao za kutaka kuitokomeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimeshindwa. Reuters iliandika zaidi kuwa: “Badala ya kudaiwa kuwa dhaifu baada ya mashambulizi makali ya Marekani na Israel mnamo Februari 28, Iran imeonyesha kuwa ingali iko imara, imeungana na imeazimia kupanga vilivyo mkondo wake wa baadaye.”
Ujumbe mwingine muhimu uliotolewa na mahudhurio makubwa ya mamilioni ya watu katika misafara ya mazishi ya Kiongozi Shahidi ni thibitisho jipya la watawala wa Marekani na Israel kushindwa kuwaelewa watu wa Iran. Ingawa Marekani na utawala wa Kizayuni zilianzisha vita viwili vilivyodumu kwa siku 12 na 40, mtawalia, kwa dhana potofu kwamba watu wa Iran hawakuwa wanaiunga mkono serikali yao, misafara mikubwa ya mazishi iliyohudhuriwa na mamilioni ya watu haikubatilisha tu dhana hii bali imethibitisha hadharani kwamba wananchi wanabakia kuwa chanzo muhimu zaidi cha nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Idadi hii kubwa ya watu waliojitokeza kwa wingi inatuma ujumbe muhimu kwamba: Maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu, hasa Marekani na utawala wa Kizayuni, bado hawana uelewa sahihi wa watu wa Iran, kutokana na kutegeme kwao chambuzi za kichochezi, taarifa potofu na simulizi zinazoenezwa na makundi hasimu yanayopinga mfumo wa Kiislamu. Leo, wanapaswa kutazama kwa mazingatio mitaa ya Tehran, Qom, na miji mingine ili kupata simulizi sahihi kuhusu Iran.
Ujumbe mwingine muhimu ni kuhusu usalama mkubwa uliodhaminiwa katika kipindi chote cha mazishi. Ingawa Trump aliwahi kudai katika vita vya karibuni kwamba angeharibu na kuirudisha Iran katika Zama za Mawe, lakini mamilioni ya watu walijitokeza katika mitaa ya Tehran na Qom kwa ajili ya kushiriki mazishi ya Kiongozi Shahidi, bila kuripotiwa hata tukio moja la kuhatarishwa usalama. Uwepo wa mamilioni ya watu katika misafara ya mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulitimiza majukumu kadhaa muhimu. Jukumu mojawapo ni kuonyesha nguvu ya kuzuia hujuma ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ingawa uzuiaji hujuma kwa kawaida hufafanuliwa katika maneno ya kijeshi, akilini, na kiteknolojia, lakini mara hii “mitaa” na uwepo hai wa watu mitaani, umeongeza mwelekeo mpya katika ufafanuzi huu.
Umuhimu mwingine ulikuwa kuonyesha kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo mkubwa wa kudhamini usalama wa idadi kubwa ya watu waliojitokeza kumuaga kiongozi wao na wakati huo huo, kukabiliana vilivyo na vitisho vya maadui, ikiwa ni pamoja na kulinda mipaka yake dhidi ya hujuma ya makundi ya kigaidi na ya Marekani inayojaribu kuhatarisha usalama wa Lango-Bahari la Hormuz. Wakati wa msafara wa mazishi, vikosi vya kijeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilitoa jibu kali na la haraka kwa makundi ya kigaidi katika maeneo ya mpakani na vilevile dhidi ya uchokozi wa Marekani katika Lango-Bahari la Hormuz, na hivyo kuizuia Marekani kuanzisha njia mpya ya kupita meli katika eneo hilo.
Umuhimu mwingine ni mahudhurio makubwa ya mamilioni ya watu katika mazishi ya Kiongozi Shahidi, suala ambalo lina taathira kubwa kwenye meza ya mazungumzo na Marekani. Viongozi wa timu ya mazungumzo ya Iran sasa wanaweza kuketi kwenye meza hiyo wakiwa na msimamo thabiti zaidi kutokana na uungwaji mkono mkubwa wa wananchi, na hivyo kuwawezesha kupinga bila kusita matakwa ya kikandamizi yanayotolwa na upande wa pili na wakati huo huo kutetea kijasiri matakwa halali ya watu wa Iran, kukiwemo kulipizwa kisasi cha damu ya Kiongozi Shahidi dhidi ya Marekani.
Nukta ya mwisho ni kwamba, mahudhurio ya mamilioni ya watu katika misafara ya mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, yanaangazia enzi mpya ya nguvu ya Iran kieneo na kimataifa, Iran ambayo tangu mwanzo imekuwa ikifaidika kimsingi na uungaji mkono mkubwa wa raia wake, kinyume na simulizi na taswira bandia ambayo imekuwa ikienezwa kwa muda mrefu ulimwenguni na wapinzani na maadui wake sugu.