Kigoma. Shahidi wa tano katika kesi ya uchaguzi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Clayton Chipando, maarufu Baba Levo, Husna Sungura ameieleza Mahakama alitekwa na kujeruhiwa tukio alilolihusisha na uchaguzi.

Shahidi huyo ametoa ushahidi huo leo Jumatano Julai 8, 2026 wakati akihojiwa na mawakili wa walalamikiwa, baada ya ushahidi wake wa maandishi kupokewa mahakamani na kuwa sehemu ya ushahidi wake.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Victoria Nongwa, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma.

Baba Levo alitangazwa mbunge wa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akimshinda mpinzani wake mkubwa kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Shahidi huyo Pendo na wenzake watatu, Johary Kabourou, Lumu Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali wamefungua kesi wakipinga ushindi wake.

Kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025 mbali na Baba Levo ambaye ni mlalamikiwa wa pili katika kesi hiyo walalamikiwa wengine ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Walalamikaji hao wanadai uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwa kuwa uligubikwa na kasoro nyingi za Sheria na Kanuni za Uchaguzi.

Wanabainisha kasoro hizo ni pamoja na ukiukwaji wa taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi, vitendo vya rushwa na udini vilivyooneshwa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.

Hivyo wanaiomba mahakama hiyo pamoja na mambo mengine iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.

Akiongozwa na wakili wa walalamikaji shahidi huyo ameieleza mahakama atatoa ushahidi wake kwa njia ya maandishi, ambao tayari ulishawasilishwa mahakamani na akaiomba mahakama iupokee.

Baada ya Mahakama kuyapokea maelezo yake hayo ya maandishi sehemu ya ushahidi wake ndipo mawakili wa walalamikiwa wakaanza kumhoji maswali ya dodoso kuhusiana na yale aliyoyaeleza katika ushahidi wake huo.

Kwa mujibu wa ushahidi wake huo wa maandishi na wakati akihojiwa na wakili wa Serikali, Erigh Rumisha na wakili wa Baba Levo, Thomas Msasa kwa nyakati tofauti ameeleza kuwa alitekwa saa sita usiku na akaende kutupwa maeneo ya Kiwanda cha Sementi.

Ameeleza baada ya kupatikana alikwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi (hakukitaja) na kwamba waliomteka wanafahamika na waliitwa kituoni hapo.

Wakati akihojiwa na wakili wa walalamikaji katika kufafanua majibu yake aliyoyatoa wakati akihojiwa maswali ya dodoso na mawakili wa walalamikaji, ameeleza kuwa alitekwa usiku alipotoka kwenda nyumba jirani kutafuta chumvi. Ambapo alipigwa na kujeruhiwa kwa marungu na vitu vyenye ncha kali na wakampora simu yake.

Amebainisha baada ya kuachwa eneo aliwasiliana na ndugu zake ambao walikwenda kumchukua kisha akaenda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi ambako aliwataja waliomteka ni viongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Abraham Makele na Emmanuel Chogero.

Shahidi huyo ameeleza watekaji wake hao waliitwa kituoni hapo wakampatia simu yake na licha kuwataja watekaji wake hao lakini Polisi hawakuwachukulia hatua zozote.

Shahidi wa sita kwa upande wake, Sheila Abdul Kilali aliyejitambulisha kama mama lishe ameieleza mahakama naye alitekwa na watu aliowaita mabaunsa wa Baba Leo na yeye ndiye aliyewaamuru wamtendee hivyo.

Amebainisha hayo katika ushahidi wake wa maandishi uliopokewa mahakamani na kuwa sehemu ya ushahidi wake.

Kwa mujibu wa ushahidi wake huo, baba yake ni mwenyekiti wa CCM na baada ya kutekwa na watu hao aliodai waliamrishwa na Baba Levo walimpeleka katika gari lake Baba Levo.

Amedai pamoja ya yeye kutekwa pia baba yake mlezi, Abdallah Kimenye ambaye ni mwana CCM na kiongozi anayeheshimika Kigoma naye alitekwa na Baba Levo na ndugu zake walifanyiwa vurugu.

Amedai katika tukio hilo alimsikia Baba Levo akisema baba yake, anamsaidia Zitto Kabwe kupiga kampeni.

Amedai kutokana na tukio hilo siku ya uchaguzi watu wengi hawakwenda kupiga kura kwani tukio hilo lilikuwa na lengo la kuwatia hofu watu wasiende kupiga kura hasa wa vyama vya upinzani.

Hata hivyo, wakati akihojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola amekiri kuwa hajui idadi ya wapiga kura katika jimbo hilo wala aliyeathirika na tukio hilo katika uchaguzi huo.

Pia amekiri uchunguzi wa jalada alilolifungua polisi bado haujatolewa majibu na akakiri kwamba si mtaalamu wa uchunguzi na kwa kuwa majibu ya uchunguzi huo hayajatoka hawezi kuthibitisha kuwa kitendo alichofanyiwa ni utekaji.

Akihojiwa na wakili wa Baba Levo, Thomas Msasa, ameeleza amefika mahakamani hapo kutoa ushahidi wa matendo haramu na ya kiuharamia yaliyofanywa na Baba Levo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *