Dar es Salaam. Chama cha National League for Democracy (NLD) kimepongeza hatua ya ACT-Wazalendo na Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kuelekea kusaini tamko la maridhiano, kikisema inaweza kurejesha utulivu wa kisiasa na kuimarisha ushirikiano kwa maendeleo ya Zanzibar.

Tamko hilo lililosainiwa na Mwenyekiti Taifa wa chama hicho, Mwenyekiti wa NLD Taifa, Mfaume Hamis Hassan limetolewa leo Julai 8, 2026, siku moja kabla ya vyama hivyo kutangaza makubaliano yao Zanzibar.

NLD imesema maridhiano hayo yanaweza kumaliza mvutano wa kisiasa uliodumu kwa muda mrefu, hasa baada ya uchaguzi mkuu wa 2025 ambapo ACT-Wazalendo iligoma kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ikitaka mazungumzo zaidi na CCM Zanzibar.

Katika taarifa yake, chama hicho kimesema amani ndiyo msingi wa maendeleo na kutoa wito kwa vyama vya siasa kuacha siasa za chuki na kujenga ushirikiano.

Pia kimesisitiza kuwa maendeleo ya Zanzibar ni sehemu ya maendeleo ya Tanzania na kupongeza viongozi wa ACT-Wazalendo na CCM Zanzibar kwa kuweka masilahi ya Taifa mbele.

NLD imeeleza inatarajia makubaliano hayo yatafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kisiasa, kuimarisha SUK na kuongeza uaminifu miongoni mwa vyama vya siasa.

Chama hicho kimekitakia mafanikio ACT-Wazalendo, CCM Zanzibar na SUK katika utekelezaji wa makubaliano hayo, kikieleza kuwa kipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza amani, haki na maendeleo nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *