Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza amesema vijana nchini wanakosa fursa ya kushiriki kikamilifu katika siasa kutokana na mazingira yanayowalazimu kujiunga na vyama vya siasa ili washiriki baadhi ya michakato ya kisiasa.

Amesema kutoakana na hilo vijana ambao si wanachama wa vyama vya siasa ni wengi kuliko wale waliojiunga na vyama.

Aidha, amesema changamoto zinazowakabili vijana haziwezi kutatuliwa kwa matumizi ya nguvu pekee, bali zinahitaji mjadala wa wazi, hoja zenye ushahidi na sera zinazojibu mahitaji yao.

Wakati Askofu Bagonza akieleza hayo, Profesa wa Uchumi, Abel Kinyondo amesema bado kuna mjadala kuhusu namna jamii inavyowaelewa vijana na mahitaji yao.

Amesema vijana wengi hujenga mifano ya maisha kupitia watu maarufu, jambo linaloonyesha umuhimu wa viongozi na taasisi mbalimbali kuendelea kujenga mazingira yatakayowawezesha kupata vielelezo vya uongozi vinavyowavutia.

Askofu Bagonza na Profesa Kinyondo wamesema hayo leo Alhamisi, Julai 9, 2026, kwenye kongamano la kisiasa na kisheria lililofanyika Zanzibar, likiwakutanisha viongozi wa vyama vya siasa, asasi za kiraia, wanaharakati na wananchi kujadili masuala ya demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.

Akichangia mada kuhusu elimu ya uraia, siasa na uongozi, Askofu Bagonza amesema baadhi ya vijana hujihisi kutengwa na michakato ya kisiasa kutokana na mtazamo kuwa nafasi za uongozi zinapatikana zaidi kupitia vyama vya siasa.

“Vijana wengi hawapo kwenye vyama vya siasa. Ni muhimu kujiuliza kama ushiriki wa kisiasa unapaswa kutegemea uanachama wa chama pekee, na wale ambao si wanachama wanashiriki vipi katika masuala ya kisiasa,” amehoji.

Aidha, amesema baadhi ya vijana hupoteza hamasa ya kushiriki katika uchaguzi kutokana na mitazamo tofauti kuhusu mazingira ya uchaguzi na uwezo wao wa kugombea nafasi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Askofu Bagonza, changamoto nyingine ni uwezo mdogo wa kifedha unaowakabili vijana, jambo linalowafanya washindwe kugharamia baadhi ya hatua za kutafuta haki au kushiriki kikamilifu katika michakato ya kisiasa.

Amesema hali hiyo huwafanya baadhi yao kutumika zaidi katika shughuli za kisiasa za wengine, badala ya wenyewe kujijengea nafasi za uongozi.

Askofu huyo pia amesema uwakilishi wa vijana katika nafasi mbalimbali za uongozi bado ni mdogo, na kuwa mara nyingi wanaopata nafasi hizo ni kundi dogo lenye uwezo wa kukidhi mahitaji na gharama zinazohusika.

Kwa upande wa malezi, amesema familia na taasisi mbalimbali zina nafasi muhimu katika kujenga kizazi chenye maadili na uwezo wa uongozi.

Hata hivyo, amesema mabadiliko ya teknolojia na matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii yamebadili namna vijana wanavyopata taarifa na kujenga mitazamo yao kuhusu maisha na uongozi.

“Mitandao ya kijamii imekuwa na ushawishi mkubwa kwa vijana. Hivyo, taasisi mbalimbali zinapaswa kubadilika na kutumia njia zinazowafikia vijana kwa ufanisi zaidi,” amesema.

Aidha, amesema changamoto zinazowakabili vijana haziwezi kutatuliwa kwa matumizi ya nguvu pekee, bali zinahitaji mjadala wa wazi, hoja zenye ushahidi na sera zinazojibu mahitaji yao.

Amesema vijana wa sasa wanahitaji kusikilizwa bila haraka ya kuwajibu, na si matamasha, kofia, fulana, baiskeli wala mikopo.

“Vijana wanahitaji kuruhusiwa kufanya makosa yao bila hulka ya kuwateka, kuwapiga wala kuwaumiza. Mfumo unahitaji kiwango cha juu cha uvumilivu kuliko mbinu za nyakuanyakua ninazoona zimetamalaki kila mahali,” amesema.

Kwa upande wake, Profesa Abel Kinyondo amesema bado kuna mjadala kuhusu namna jamii inavyowaelewa vijana na mahitaji yao.

Amesema vijana wengi hujenga mifano ya maisha kupitia watu maarufu, jambo linaloonyesha umuhimu wa viongozi na taasisi mbalimbali kuendelea kujenga mazingira yatakayowawezesha kupata vielelezo vya uongozi vinavyowavutia.

Akizungumzia maendeleo ya demokrasia, Profesa Kinyondo amesema kuna umuhimu wa kuendelea kujadili njia mbalimbali za kuongeza ushiriki wa wananchi katika uongozi, ikiwemo mjadala kuhusu mgombea binafsi.

Pia amependekeza kufanyika kwa tathmini ya utekelezaji wa falsafa ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya) ili kubaini mafanikio yaliyopatikana na maeneo yanayohitaji kuimarishwa katika muktadha wa maendeleo ya kidemokrasia nchini.

“Ni imani yangu kwamba katika mkutano huu tuweze kuwabainisha wanaonufaika na kero zilizopo na kujua namna tunavyoweza kushughulika nao. Ni jambo moja kuzungumza kuwa kuna watu wanatekwa, wengine wanafungwa, mikutano inazuiliwa na maandamano yanazuiwa.

“Lakini ukweli ni kwamba kuna kundi la watu linanufaika na hali hiyo. Ili wao wafaidike, watu wanatekwa na mikutano inazimwa. Sasa hali hiyo ikisimamishwa, faida wanayoipata haitakuwepo,” amesema.

Kwa upande wake, Rukiah Ibrahim, akichangia mjadala, amesema vyama vingi vya ukombozi havipo katika utawala sasa kutokana na kuwa karibu na dola.

Amesema hakuna chama chochote kilichoanzishwa kwa ajili ya ukombozi kwa kuwa waanzilishi wake walikuwa ndani ya dola tangu kilipoanzishwa.

“Vijana hatujui tunataka nini. Kama tunataka kitu, tunapaswa kutoka kudai haki. Haki haijawahi kupatikana kwa njia rahisi. Tuwe na misimamo ya kutaka mabadiliko ya Katiba,” amesema.

Naye Rukaiyah Nassir amezungumzia suala la watu kuwa machawa, akisema haliwahusu vijana pekee, bali hata watu wazima wamekithiri katika tabia hiyo ya kujipendekeza kwa watawala.

Kuhusu matumkizi ya mitandao, amesema: “Vijana wanatumia zaidi mitandao ya kijamii kwa sababu mikusanyiko hairuhusiwi. Mitandaoni tunapotaka kuzungumza, hakuna zuio tunaloweza kukumbana nalo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *