Zanzibar. Wakulima 200 wa mwani kutoka Shehia za Uzi na Muungoni, Mkoa wa Kusini Unguja, wamekabidhiwa vifaa muhimu vya kilimo, ikiwa ni juhudi za kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa zao hilo na kuwaongezea wakulima kipato.
Msaada huo ni kupitia Mradi wa Seaweed Social Enterprise (SESEP), unaotekelezwa na Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) kwa ufadhili wa The Big Heart Foundation
Mradi huo unatekelezwa kupitia mfumo wa Kilimo Mkataba na unalenga kukabiliana na changamoto zinazowakabili wakulima wa mwani, ikiwemo upatikanaji wa pembejeo, gharama za uzalishaji na uhaba wa masoko yenye uhakika.
Katika awamu ya majaribio, mradi huo unawanufaisha wakulima 200, wakiwemo wanawake 175 sawa na asilimia 88 na wanaume 25 sawa na asilimia 12. Aidha, vijana 51 wenye umri kati ya miaka 15 na 35 ni sehemu ya wanufaika wa mradi huo.
Wananchi wa Shehia za Uzi na Muungoni wakipokea vifaa vya kilimo cha mwani vilivyotolewa kupitia Mradi wa Seaweed Social Enterprise Project (SESEP), unaotekelezwa na Zanzibar Maisha Bora Foundation kwa ufadhili wa The Big Heart Foundation.
Mbali na kupokea vifaa vya kilimo, wakulima hao watapatiwa mafunzo ya vitendo kuhusu mbinu bora za uzalishaji wa mwani, udhibiti wa ubora, uchakataji na uongezaji thamani wa mazao pamoja na namna ya kupata masoko yenye ushindani ndani na nje ya Zanzibar.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Zanzibar Maisha Bora Foundation na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha sekta ya uchumi wa buluu na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza leo Alhamisi, Julai 9, 2026 kwa niaba ya wananchi wa Shehia ya Uzi, Othman Haji amesema vifaa hivyo vitawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
“Kupokea vifaa hivi ni hatua kubwa kwetu. Vitatusaidia kuongeza uzalishaji wa mwani na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Tunashukuru Zanzibar Maisha Bora Foundation na The Big Heart Foundation kwa kutuunga mkono na kutupa fursa ya kuboresha maisha yetu kupitia kilimo cha mwani,” amesema.
Naye Sheha wa Muungoni, Mussa Mbwato, amesema mradi huo unatoa matumaini mapya kwa wakulima wa eneo hilo, hususan wanawake na vijana ambao ndio nguvu kubwa katika shughuli za kilimo cha mwani.
Amesema vifaa hivyo vitachangia kuongeza ubora na kiwango cha uzalishaji wa mwani, hatua ambayo itawawezesha wakulima kupata mapato bora na kuboresha ustawi wa familia zao.
Wananchi wa Shehia za Uzi na Muungoni wakipokea vifaa vya kilimo cha mwani vilivyotolewa kupitia Mradi wa Seaweed Social Enterprise Project (SESEP), unaotekelezwa na Zanzibar Maisha Bora Foundation kwa ufadhili wa The Big Heart Foundation.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa SESEP kutoka Zanzibar Maisha Bora Foundation, Titus Lukurazo, amesema ugawaji wa vifaa hivyo ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha wakulima kupata rasilimali muhimu zitakazoongeza tija na kipato.
“Lengo letu ni kuhakikisha wakulima wanapata zana na maarifa yatakayowasaidia kuzalisha mwani wenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko. Tunathamini sana ufadhili wa The Big Heart Foundation na ushirikiano wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huu,” amesema.
Ameongeza kuwa pamoja na ugawaji wa vifaa, mradi utaendelea kuimarisha mfumo wa Kilimo Mkataba, kuboresha huduma za uchakataji na uongezaji thamani wa mwani, kuwaunganisha wakulima na masoko yenye ushindani na kuweka msingi wa maendeleo endelevu ya sekta ya mwani Zanzibar.
Kupitia utekelezaji wa SESEP, wadau wanatarajia kuongeza uzalishaji wa mwani, kuboresha kipato cha kaya, kuchochea ajira kwa wanawake na vijana, na kuimarisha mchango wa sekta ya uchumi wa buluu katika maendeleo ya Zanzibar.