DAR ES SALAAM: MRATIBU wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema Tanzania inatarajia kuingia katika hatua muhimu ya maandalizi ya Mapitio ya Nne ya Haki za Binadamu (Universal Periodic Review), yanayotarajiwa kufanyika kati ya Oktoba na Novemba mwaka huu mjini Geneva, Uswisi.
Olengurumwa ameyasema hayo katika mkutano wa maandalizi ya mapitio hayo uliowakutanisha baadhi ya asasi za kiraia, wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa pamoja na wadau wa maendeleo, kwa lengo la kujadili masuala muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele katika tathmini hiyo ya kimataifa.
Amesema lengo la mkutano huo ni kuhakikisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zitakazoshiriki katika mapitio ya Tanzania zinapata taarifa sahihi kuhusu hali halisi ya haki za binadamu nchini, ili ziweze kuuliza maswali yanayozingatia mazingira ya Tanzania na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kukabiliana na changamoto zilizopo.
Akifafanua kuhusu UPR, Olengurumwa amesema ni utaratibu wa Umoja wa Mataifa ulioanzishwa mwaka 2006 unaozihusisha nchi zote wanachama katika kutathminiana kuhusu utekelezaji wa wajibu wao wa kulinda, kuheshimu na kuendeleza haki za binadamu. Kupitia mchakato huo, nchi huulizana maswali na kutoa mapendekezo ya kuboresha hali ya haki za binadamu.

Akizungumzia utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa katika mzunguko uliopita wa UPR, amesema Tanzania ilikubali mapendekezo 108. Hata hivyo, tathmini iliyofanywa inaonesha kuwa zaidi ya nusu ya mapendekezo hayo hayakutekelezwa ipasavyo, mengine yalitekelezwa kwa kiwango cha sehemu, huku yaliyotekelezwa kikamilifu yakiwa chini ya asilimia 10.
Amesisitiza kuwa UPR ni mchakato muhimu wa uwajibikaji wa kimataifa kwa kuwa nchi hulazimika kueleza hatua zilizochukuliwa katika kutekeleza ahadi na mapendekezo iliyokubali katika mapitio yaliyopita.
Kwa mujibu wa Olengurumwa, zaidi ya asasi za kiraia 300 zilishiriki kuandaa ripoti ya pamoja ya asasi za kiraia kuhusu hali ya haki za binadamu nchini, ambayo tayari imewasilishwa kwa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuzingatiwa wakati wa mapitio hayo.
Ameongeza kuwa ushiriki wa asasi za kiraia katika maandalizi ya mzunguko wa nne wa UPR umeongezeka ikilinganishwa na mizunguko iliyopita, jambo linaloonesha kuimarika kwa ushiriki wa wadau katika masuala ya haki za binadamu. Ameeleza matumaini kuwa Tanzania itakubali mapendekezo mengi zaidi yatakayotolewa katika mzunguko huu kuliko ilivyofanya katika mapitio yaliyopita.
Mkutano huo umehudhuriwa na wawakilishi kutoka sekta mbalimbali, zikiwemo zinazojihusisha na haki za watoto, wanawake, wafugaji, mazingira, uhuru wa kujieleza pamoja na makundi mengine ya watetezi wa haki za binadamu.
