Shughuli maalumu ya kuuaga na kuusindikiza mwili wa kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei pamoja na mashahidi wa familia yake imefanyika leo katika mji mtakatufu wa Mash’had.
Mamilioni ya waombolezaji wamehudhuria mazishi hayo katika mji wa Mash’had ilipo Haram ya Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as).
Mazishi hayo yamehudhuriwa na raia wa kawaida, viongozi wa kisiasa kutoka zaidi ya nchi 45 duniani ambao wamejitokea leo katika mji huo kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huuyo shupavu aliyeuawa kidhulma Februari 28 mwaka huu kufuatia mashambulio ya kijeshi ya Marekani na utawala haramu wa Israel katika mji wa Tehran.
Aidha maombolezo hayo yamehudhuriwa na wanazuoni wa Kiislamu, viongozi wa dini mbalimbali na wasomi kutoka zaidi ya nchi 90 duniani.

Baada ya shughuli kubwa ya mazishi iliyofanyika jana katika miji mitakatifu ya nchi jirani ya Iraq, mwili wa hayati Imam Khamenei leo uko katika mji wa kaskazini mwa Iran wa Mash’had, na baada ya kuagwa na mamilioni ya wakazi wa mji huo na mikoa ya kandokando hatimaye kiongozi huyo atazikwa katika Haram ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Ali bin Musa Ridha (AS).
Kushiriki mamilioni ya watu katika mazishi haya kunatoa ujumbe muhimu sana. Mojawapo ya jumbe muhimu zaidi ni imani thabiti ya wananchi wa Iran kwamba kiongozi huyo aliyeuawa shahidi alijitolea maisha yake yote kwa ajili ya kulinda Uislamu, Mapinduzi na heshima ya Iran ya Kiislamu. Mahudhurio haya makubwa ya umma ni ishara ya shukrani kwa juhudi zisizo na kikomo zilizofanywa na kiongozi huyo kwa ajili ya Uislamu na Iran, juhudi alizozidhamini kwa maisha yake mwenyewe na ya wanafamilia wake. Ujumbe mwingine muhimu uliotolewa na mahudhurio ya mamilioni ya watu katika msafara wa mazishi ya kiongozi huyo adhimu wa Mapinduzi ni sisitizo linalotolewa kwa ajili ya kuendeleza njia na fikra zake katika awamu mpya.