Nyota wa soka wa ndani na nje ya Tanzania Jumapili ya Julai 12, mwaka huu watakutana katika Tamasha la Hisani la “Clement Mzize Washike Mkono – Season One”, litakalofanyika Uwanja wa Samora mjini Iringa kwa lengo la kuunganisha nguvu za michezo na jamii kupitia misaada kwa makundi yenye mahitaji maalumu.
Pamoja na michezo mingine, tamasha hilo, linalotarajiwa kuvutia maelfu ya mashabiki kutoka mkoa wa Iringa na mikoa jirani, litazikutanisha Timu Mzize kwa upande mmoja na Timu Oscar Evaristo, mchezaji wa Port Fouad ya Misri. Mzize na Oscar wote ni wakazi wa Iringa.
Akizungumza na waandishi wa habari, mshambuliaji wa klabu ya Yanga na timu ya Taifa, Clement Mzize, amesema tamasha hilo lililoandaliwa na Mzize Foundation ni sehemu ya ndoto yake ya kurudisha kwa jamii mafanikio aliyoyapata kupitia soka.
Amesema jina la “Washike Mkono” linaakisi dhamira ya kuwafikia watu wenye uhitaji kwa vitendo, akisisitiza kuwa mafanikio ya mwanamichezo yanakuwa na maana zaidi yanapoboresha maisha ya wengine.

“Soka limenifikisha hapa nilipo. Sasa ni wakati wa kulitumia kuwashika mkono wale wanaohitaji msaada. Tunataka mashabiki wasije kutazama mpira pekee, bali wawe sehemu ya kubadilisha maisha ya watu,” amesema Mzize.
Amesema fedha zitakazokusanywa kupitia tamasha hilo zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya kijamii, ikiwemo ujenzi wa vyoo katika shule, na ununuzi wa vifaa tiba kwa hospitali ikiwemo mashine ya ultrasound.
Aidha zitasaidia kuwawezesha waendesha bodaboda 100( kazi aliyowahi kuifanya akiwa mjini Iringa) watakaopatiwa mafuta, helmeti na reflector kwa ajili ya kuongeza usalama wao barabarani.
Katika tamasha hilo mashabiki wanatarajiwa kushuhudia nyota wengi wa soka, huku Mzize akithibitisha ushiriki wa Feisal Salum, Maxi Nzengeli, Bakari Mwamnyeto, Denis Nkane, Kibwana Shomari na Lomalisa Mutambala, huku nyota wengine wa ndani na wa kimataifa wakitarajiwa kutangazwa kadri siku ya tamasha inavyokaribia.

Mbali na mchezo wa hisani, tamasha hilo litatoa burudani ya siku nzima kupitia maonyesho ya muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali, mechi za veterani, michezo ya watoto na fursa kwa mashabiki kukutana ana kwa ana na wachezaji wanaowafuatilia kila wiki kwenye ligi mbalimbali.
Mchezaji wa Port Fouad ya Misri, Oscar Evaristo, amesema kushiriki kwake ni ishara ya mshikamano wa wanasoka katika kutumia umaarufu wao kuleta mabadiliko ya kijamii.
Amesema baadhi ya nyota kutoka nje watakaoshiriki hatawata kwa sasa ili kuongeza hamasa ya tamasha hilo, huku akisisitiza kuwa vipaji vya soka kutoka Iringa vitapewa nafasi ya kuonyesha uwezo wao mbele ya makocha, mawakala na wadau wa mchezo huo.

“Tunataka tamasha hili liwe daraja la vipaji. Huenda kijana mmoja kutoka Iringa akaonekana hapa na kuanza safari yake ya soka la kulipwa,” amesema Oscar.
Afisa Utamaduni na Michezo Mkoa wa Iringa, Steven Sanga, amesema Serikali ya Mkoa imejipanga kuhakikisha tamasha hilo linafanyika kwa mafanikio, likiwa na maandalizi yote muhimu ya kiusalama na kiafya.
Alisema huduma za kwanza, uchangiaji damu, usalama wa mashabiki na uratibu wa taasisi mbalimbali tayari vimekamilika, huku akieleza kuwa tamasha hilo litaiweka Iringa katika ramani ya matukio makubwa ya michezo yanayochangia maendeleo ya jamii.

Mzize pia aliwashukuru wadhamini mbalimbali, akiwemo GSM, Asas, Master Lim, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Jeshi la Polisi na wadau wengine kwa kuwezesha kufanyika kwa tamasha hilo.