
Dar es Salaam. Malalamiko ya wananchi kuhusu kubambikiwa malipo ya maegesho ya magari huenda yakapungua baada ya kubuniwa kwa teknolojia ya Rafiki Parking and Car Wash, mfumo unaotumia akili bandia (AI) kujiendesha.
Mfumo huo utakuwa ukiweka rekodi zote za magari yanayoingia katika eneo la maegesho husika na kubainisha kiwango cha pesa kinachopaswa kulipwa kwa ajili ya maegesho kulingana na muda ambao mmiliki wa gari ametumia.
Kwa wenye biashara za kuosha magari pia utakuwa na uwezo wa kuweka rekodi ya magari yote yaliyoingia na huduma iliyofanywa.
Hili linakuja wakati hivi karibuni baadhi ya wamiliki wa magari wamekuwa wakilalamikia kutozwa fedha za ziada au kubambikiwa muda wa maegesho ambao hawakutumia kutokana na mifumo ya usimamizi inayotegemea rekodi za mikono.
Akizungumza katika Maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) jana Julai 9, 2026, mbunifu wa mfumo huo, Joshua Gilbert amesema katika uendeshaji wake, unatumia teknolojia ya kutambua namba za usajili wa magari, kurekodi kila gari linaloingia na kutoka katika eneo la maegesho.
Amesema mfumo huo huanza kufanya kazi mara tu gari linapoingia katika eneo la maegesho kwa kusoma namba zake na kuhifadhi taarifa zote, ikiwamo muda wa kuingia na kutoka, jambo linalosaidia kuondoa makosa ya kibinadamu na kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato.
“Mfumo huu unarekodi kila gari linaloingia na kutoka. Ikiwa gari litazidisha muda wa maegesho uliolipiwa, mfumo unakokotoa moja kwa moja gharama za ziada, hivyo kusaidia kupunguza upotevu wa mapato na kuondoa migogoro kati ya mteja na mtoa huduma,” amesema Gilbert.
Amesema matumizi ya teknolojia hiyo yanaweza kusaidia pia kuondoa changamoto ya ubambikaji wa malipo kwa sababu taarifa zote huhifadhiwa kidijitali na zinaweza kufuatiliwa wakati wowote.
Mbali na usimamizi wa maegesho, mfumo huo pia umetengenezwa kusaidia kusimamia biashara za kuosha magari, kila huduma inayotolewa kwa mteja huingizwa kwenye mfumo pamoja na taarifa za gari na aina ya huduma iliyotolewa.
Gilbert ambaye anatoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), amesema mfumo huo unasaidia kuongeza uwajibikaji, kurahisisha utoaji wa taarifa za biashara na kupunguza mianya ya upotevu wa fedha ambayo imekuwa ikijitokeza katika biashara zinazosimamiwa kwa njia za kawaida.
“Kuna biashara nyingi zinazofanya miamala ya fedha kila siku, lakini bado zinategemea mifumo ya karatasi au kumbukumbu za mikono. Hali hiyo huongeza uwezekano wa makosa, upotevu wa mapato na wakati mwingine migogoro na wateja,” amesema.
Kampuni hiyo pia imezindua msaidizi wa kidijitali AI Employee, kazi yake ni hujibu maswali ya wateja kupitia tovuti za kampuni au mtandao wa WhatsApp bila kuhitaji mfanyakazi wa huduma kwa wateja.
Gilbert amesema teknolojia hiyo inaziwezesha taasisi na biashara kutoa huduma saa 24 kwa siku huku ikipunguza mzigo kwa watumishi wa huduma kwa wateja.
“Lengo letu ni kusaidia biashara za Kitanzania kukumbatia mabadiliko ya kidijitali kwa kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi, kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato na kuboresha huduma kwa wateja,” amesema.
Wakati mahitaji ya teknolojia za kidijitali yakiendelea kuongezeka nchini, majukwaa yanayotengenezwa na wabunifu wa ndani yanatarajiwa kusaidia biashara ndogo na za kati kupata suluhisho nafuu za teknolojia zinazoweza kuongeza ufanisi, kuimarisha usimamizi wa fedha na kupunguza malalamiko ya wateja yanayotokana na mifumo isiyo na uwazi.
Akizungumzia mfumo wa kusaidia kukokotoa fedha za maegesho ya magari, Shadrack Chagua amesema ni vyema halmashauri, hususan za Jiji la Dar es Salaam, zikauchangamkie ili kupunguza upotevu wa mapato na kuondoa malalamiko ya wananchi.
“Nadhani hili ni suluhisho la kudumu ambalo linapaswa kufanyiwa uwekezaji. Hii si tu itasaidia kuongeza mapato, bali pia kupunguza ubambikaji wa fedha za maegesho,” amesema.