Dar es Salaam. Kuna habari njema kwa Yanga na Simba ambazo msimu ujao zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao wakati huu zikisubiria kufahamu wapinzani wao wa hatua za awali.

Timu hizo mbili zitaanza mashindano hayo msimu ujao zikiwa zimeporomoka katika chati ya viwango vya ubora wa soka kwa klabu vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lakini zimepata kitonga ya kutoangua katika chungu cha tatu ama cha nne katika upangaji wa droo ya hatua ya makundi iwapo zitafanikiwa kuingia katika hatua hiyo.

Hiyo inafuatia klabu nne zilizo juu ya Simba na Yanga katika chati hiyo ya ubora ya klabu ya CAF, kushindwa kujihakikishia kushiriki mashindano hayo baada ya kufanya vibaya katika ligi zao.

Hilo linafanya Simba na Yanga kila moja kuwa na uhakika wa kuwa miongoni mwa timu nane za juu ambazo zitawekwa katika vyungu viwili vya mwanzo katika upangaji wa droo ya hatua ya makundi.

Katika chati hiyo ya ubora wa klabu ya CAF, timu zilizo nafasi za juu ambazo hazitokuwemo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ni Al Ahly, USM Alger, AS FAR na CR Belouizdad.

Kama timu hizo zingefanikiwa kushiriki na kisha zingetinga katika hatua ya makundi kama ilivyo kwa Yanga na Simba, maana yake wawakilishi hao wa Tanzania wangepangwa katika chungu cha tatu.

Kwa sasa, Simba ipo katika nafasi ya 11 na Yanga ipo katika nafasi ya 12 kwenye chati hiyo ya ubora wa klabu ya CAF.

Kutokuwepo kwa Al Ahly, USM Alger, Belouizdad na AS FAR, kunazisogeza Simba na Yanga hadi katika nafasi nane za juu katika upangaji wa hatua ya makundi.

Na hilo likitokea, itakuwa ni mara ya pili mfululizo kwa Yanga na Simba kuwekwa katika chungu cha pili kwenye upangaji wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Faida ya timu kupangwa katika chungu cha kwanza au cha pili kwenye upangaji wa hatua ya makund ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ni timu kuanzia na kumalizia mechi za hatua hiyo katika uwanja wa nyumbani.

Nyingine ni timu kutokutana na wapinzani wagumu au wenye uzoefu zaidi. Katika chati ya ubora wa klabu ya CAF hivi sasa, kinara ni Mamelodi Sundowns yenye pointi 73 ikifuatiwa na Al Ahly iliyo na pointi 66.

Esperance inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 58, RS Berkane iko nafasi ya nne na pointi zake 57 huku USM Alger iko nafasi ya tano ikiwa na pointi 52.

Nafasi ya sita inashikiliwa na Zamalek iliyo na pointi 49, Pyramids FC ina pointi 48 ikiwa namba saba, AS FAR inashika nafasi ya nane na pointi 41 huku Al Hilal ikiwa nafasi ya tisa na pointi 39.

CR Belouizdad ipo nafasi ya 10 na pointi 38 sawa na Simba iliyo katikanafasi ya 11 na Yanga iliyo katika nafasi ya 12 ina pointi 25.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *