
Dar es Salaam. Zawadi isiyo ya kawaida aliyotoa Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, kwa viongozi walioshiriki mkutano wa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (Nato) imezua mjadala barani Ulaya, baada ya kuwapatia kila mmoja bastola aina ya Gümüşay .357 Magnum iliyowekwa jina la mzawadiwa na risasi halisi.
Zawadi hiyo iliwalazimu maofisa wa usalama na itifaki wa nchi mbalimbali kuanza kushughulikia taratibu za kisheria za kusafirisha silaha hizo, huku baadhi ya viongozi wakiamua kuzikabidhi kwa vyombo vya usalama au makumbusho ya kijeshi.
Mkutano huo wa Nato uliofanyika Ankara uliwakutanisha viongozi wa nchi wanachama kujadili hali ya usalama duniani, hususan vita vinavyoendelea nchini Ukraine, mvutano unaoongezeka Mashariki ya Kati na kuimarika kwa uwezo wa kijeshi wa muungano huo.
Katika maazimio yake, viongozi wa Nato walisisitiza kuendelea kuimarisha ulinzi wa pamoja wa wanachama, kuongeza uwekezaji katika sekta ya ulinzi na uzalishaji wa silaha za kisasa, kuendelea kuisaidia Ukraine katika vita dhidi ya Russia na kusisitiza kuwa Iran haipaswi kumiliki silaha za nyuklia
Nato ina nchi wanachama 32; nchi 30 ziko Ulaya na nchi mbili ni Marekani na Canada.
Viongozi hao walipokea bastola aina ya Gümüşay 357 Magnum, ikiwa imewekwa ndani ya boksi la mbao lenye bendera ya Uturuki na nembo ya Nato, pamoja na vifaa vya kusafishia silaha na nyaraka maalumu za usafirishaji.
Lengo la Erdoğan, kwa mujibu wa maofisa wa Uturuki, lilikuwa kuonesha uwezo wa sekta ya ulinzi ya nchi hiyo, ambayo imeendelea kukua na kuwa miongoni mwa bidhaa muhimu za mauzo ya nje.
Hata hivyo, zawadi hiyo iliwakuta walinzi na maofisa wa itifaki wa mataifa mbalimbali katika wakati mgumu, wakilazimika kushughulikia taratibu za kisheria na kiusalama za kusafirisha silaha zinazofanya kazi pamoja na risasi zake.
Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Bart De Wever, alikabidhi bastola aliyopokea kwa polisi wa uwanja wa ndege mara tu alipowasili Brussels ili ihifadhiwe salama wakati taratibu za kisheria zikiendelea.
Ofisi yake ilisema hakufahamu mara moja kuwa zawadi hiyo ilikuwa bastola inayoweza kutumika hadi aliporejea nchini kwake.
Pia, Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, alimshukuru Erdoğan kwa zawadi hiyo, lakini msemaji wake alisema bastola hiyo itafanyiwa marekebisho ya kuondoa uwezo wa kufyatua risasi kabla ya kukabidhiwa kwenye makumbusho ya kijeshi.
Kwa upande wa Poland, bastola aliyokabidhiwa Rais Karol Nawrocki ilibaki kwenye taratibu za forodha katika Uwanja wa Ndege wa Warsaw, huku wasaidizi wake wakisisitiza kuwa haitatumika kufyatua risasi bali itahifadhiwa kama zawadi rasmi ya kidiplomasia.
Nchini Uingereza, Waziri Mkuu Keir Starmer alisema alipokea bastola iliyochongwa jina lake pamoja na risasi, huku vyanzo vya Downing Street vikieleza pia kulikuwa na vifaa vya kusafishia silaha hiyo.
Baadhi ya viongozi, akiwamo Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz na Waziri Mkuu wa Uholanzi, Rob Jetten, waliziacha bastola zao nchini Uturuki ili zikamilishiwe taratibu za kisheria kabla ya kusafirishwa.
Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, alitania kuwa zawadi yake ya sharubati ya maple aliyompa mwenyeji “haikulingana kabisa” na bastola alizowapa Erdoğan wageni wake, akisisitiza kuwa silaha aliyopokea itafanyiwa marekebisho ya kuondoa uwezo wa kufyatua risasi kabla ya kupelekwa kwenye makumbusho ya vita nchini humo.
Sekta ya silaha ya Uturuki
Bastola zilizotolewa ni aina ya Gümüşay .357 Magnum, mojawapo ya silaha adimu zilizotengenezwa nchini Uturuki miaka ya 1990 na Kampuni ya Mke.
Ingawa Uturuki kwa sasa huzalisha zaidi bastola za kisasa za nusu automatiki, Serikali imeendelea kutumia bidhaa za sekta ya ulinzi kama sehemu ya diplomasia na kuonesha uwezo wa viwanda vyake vya kijeshi.
Kwa mujibu wa taasisi ya Small Arms Survey yenye makao yake Geneva, nchini Uswisi, Uturuki ilikuwa miongoni mwa wauzaji wakubwa wa silaha ndogo duniani kati ya mwaka 2019 na 2024, ikishika nafasi ya tatu baada ya Marekani na Italia.
Trump abadilisha ndege Uturuki
Katika hatua nyingine, Rais wa Marekani, Donald Trump, alifanya mabadiliko ya ghafla katika safari yake ya kutoka Uturuki kwenda Uingereza baada ya kuamua kutumia Air Force One ya zamani badala ya ndege mpya aliyokabidhiwa na Qatar.
Trump alikuwa ametumia ndege hiyo mpya aina ya Boeing 747 kufika Ankara kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Nato, ikiwa ndiyo safari yake ya kwanza ya kimataifa tangu iingizwe katika matumizi ya Ikulu ya Marekani.
Hata hivyo, alipoondoka Uturuki kuelekea Kituo cha Jeshi la Anga cha RAF Mildenhall nchini Uingereza, alisafiri kwa Air Force One ya zamani yenye rangi ya buluu hafifu, huku ndege mpya ikipelekwa mapema katika kituo hicho kwa ajili ya kuonyeshwa wanajeshi wa Marekani.
Baadaye, Trump alipanda tena ndege hiyo mpya kwa safari ya kurejea Washington.
Kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump alisema alichagua kutumia ndege ya zamani “kwa kumbukumbu za zamani”, huku akieleza kuwa alitaka wanajeshi waliopo Mildenhall wapate nafasi ya kuitembelea ndege hiyo mpya.
Alisema wanajeshi hao walifurahia kuiona ndege hiyo ambayo ameisifu mara kwa mara kuwa ni ya kipekee na inayostahili hadhi ya Rais wa Marekani.
Katika matamshi yake ya awali, Trump amekuwa akiitaja ndege hiyo kama “ikulu inayotembea angani”, akisisitiza kuwa kiongozi wa Marekani anapaswa kusafiri kwa ndege inayoakisi hadhi na nguvu za taifa hilo.
“Ndege hii ni ya kuvutia sana. Rais wa Marekani anapaswa kuwa na ndege yenye hadhi kuliko nyingine yoyote duniani,” amekuwa akisema Trump katika nyakati tofauti akizungumzia ndege hiyo.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.