Maridhiano mapya ya kisiasa kati ya vyama vikuu vya Zanzibar, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, yalifikiwa rasmi jana baada ya viongozi wa pande hizo mbili kusaini tamko la pamoja.

Tamko hilo lilisomwa Ikulu Zanzibar na Katibu Mkuu Kiongozi, Mansura Mossi Kassim, mbele ya viongozi wa serikali, viongozi wa dini na wawakilishi wa vyama vya siasa. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliyeshuhudia utiaji saini huo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, tamko hilo la pamoja linaambatana na ajenda zilizokubaliwa na kutiwa saini na pande zote mbili na kwamba ajenda hizo zitajadiliwa katika kamati ya pamoja itakayoshauri juu ya mfumo, utaratibu na upeo wa makubaliano ya pamoja katika kufanikisha hilo chombo maalumu kitaundwa chini ya sheria ili kuratibu na kusimamia utekelezaji wa makubaliano”

Maridhiano hayo yanaelezwa kuwa yanafungua fursa ya kujenga siasa za ushirikiano na mazungumzo, badala ya migogoro na mvutano wa kisiasa. Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza viongozi wa CCM na ACT-Wazalendo kwa kufanikisha hatua hiyo, akisisitiza kuwa tofauti za kisiasa zinapaswa kutatuliwa kwa mazungumzo na si kwa vurugu.

Kwa mujibu wa viongozi hao, makubaliano ya leo ni hatua muhimu katika kuimarisha umoja, mshikamano na ustawi wa taifa.

Naye Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema wananchi wa Zanzibar wamekuwa na matarajio ya muda mrefu ya kuona maridhiano ya kweli yanayoweka mbele maslahi ya wananchi.

 “Chama chetu kitasimamia yote yanayohitajika na kitaiendelea kuwafikia wananchi wote wa Zanzibar bila ya kujali itikadi zao ili kuwaelimisha juu ya umuhimu wa mchakato huu naomba niwaambie watanzania linapotokea jambo lolote muhimu kuzungumza”

Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuyasimamia maridhiano hayo ili yawe na matokeo chanya, akisema wananchi wengi wa Zanzibar wanatamani kuona siasa za maridhiano zikiendelea kuimarika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *