.

Chanzo cha picha, AFP

Jumuiya ya madola imeitaka serikali ya Tanzania kutafuta ufumbuzi wa kisiasa na kisheria kumaliza kesi inayomkabili kiongozi wa upinzani nchni humo Tundu Lissu

Haya ni kwa mujibu wa mapendekezo yaliowasilishwa kwa jumuiya hiyo na aliyekuwa rais wa zamani wa Malawi na mjumbe maalum wa jumuiya hiyo Lazariaus Chakwera.

Chakwera aliteuliwa kupatanisha mivutano ya kisiasa na kuwezesha mazungumzo ya kitaifa kufuatia uchaguzi mkuu wenye utata wa Oktoba 2025, ambao ulisababisha maandamano makubwa.

Tundu Lissu alikamatwa kufuatia mkutano wa hadhara wa kisiasa huko Mbinga, Tanzania, ambapo alitoa wito wa kufanyika marekebisho makubwa ya uchaguzi na katiba.

Serikali ilimshtaki kwa uhaini na kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni, kwa madai kuwa kampeni yake ya “Hakuna Marekebisho, Hakuna Uchaguzi” ilichochea uasi wa umma.

Katika kesi yake inayoendelea ambayo imeahirishwa mara nyingi , Lissu aliomba kujiwakilisha mwenyewe baada ya jopo lake la mawakili kudai kuwa walinyimwa fursa ya kuwasiliana naye kwa faragha na hivyo kujiondoa kwenye kesi hiyo.

Hatahivyo serikali ya Tanzania imekuwa ikisisitiza kuwa kesi inayomkabili lissu haijachochewa kisiasa na mahakama ipo huru katika kuisikiliza.

Waliokamatwa waachiwe huru

Aidha mapendekezo ya Jumuiya hiyo yametoa wito kwa serikiali kuwaachilia wale wote waliokamatwa wakati wa ghasia hizo kwa kupigania haki zao kwa amani.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu na wanasheria waliripoti kuwa idadi kubwa ya watu walifikishwa mahakamani mapema mwezi wa Novemba na wakati wa uchaguzi wakikabiliwa na mashtaka mazito.

Vilevile ripoti hiyo ya Chakwera imeitaka serikali ya rais Samia Suluhu Hassan ndani ya siku sitini kurejesha mifumo yote ya kidijitali na kusita kutoa vitisho kwa Watetezi wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza.

Wakati wa uchaguzi uliopingwa wa Oktoba 2025, serikali ya Tanzania ilituma wanajeshi na polisi kukandamiza maandamano kwa nguvu, kufunga mtandao, na kuweka amri ya kutotoka nje katika miji mikubwa.

.

Chanzo cha picha, Jacob Nankhonya

Viongozi wa upinzani

Mamlaka iliwakamata mamia ya watu—wakiwemo watu muhimu wa upinzani—wakiwashtaki kwa uhaini, huku uchunguzi rasmi baadaye ukiripoti mamia ya vifo.

Jumuiya ya kimataifa ililaani uchaguzi huo, ikitaja mchakato wa kidemokrasia wenye kasoro na vurugu kali zilizofuatia uchaguzi huo.

Ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa AU ulitangaza kwamba kura hiyo haikuzingatia viwango vya kidemokrasia, kujazwa kwa kura katika masanduku ya kupigia kura, kuzimwa kwa mtandao, na utekaji nyara uliochochewa kisiasa ambao uliathiri uadilifu wa uchaguzi.

Mabadiliko ya mfumo wa Uchaguzi

Vilevile mapendekezo hayo yameitaka serikali ya Tanzania ndani ya siku tisini kuanzisha jukwaa la vyama vya kisiasa lisilopendelea upande wowote ili kuangazia mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi, ushindani wa kisiasa, waliokamatwa na uwajibikaji.

Jumuiya hiyo imeitaka serikali ya Tanzania kuanzisha bila kuchelewa , Uchunguzi huru wa uhalifu uliofanyika kama ilivyopendekezwa na Tume ya uchunguzi , ikiwemo masuala kama vile ulipaji fidia kwa waathiriwa.

Imeongezea kwamba itaitisha kikao kisicho cha kawaida mwezi Septemba 2026 ambapo Tanzania itaalikwa ili kutoa ripoti kuhusu hatua ilizopiga kabla ya mkutano huo kufanyika.

Aidha mapendekezo hayo yanamtaka katibu mkuu kuendelea kuwasiliana na serikali ya Tanzania ili kutoa ripoti za hatua zaidi zilizoafikiwa.

.

Ghasia wakati wa uchaguzi

Machafuko makali yaliyohusiana na uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba 2025 yalisababishwa hasa na kuondolewa kwa vyama vikuu vya upinzani na wagombea wao kushirki katika uchaguzi huo.

Maandamano yalizuka Dar es Salaam na baadaye yakaenea hadi miji mingine, kufuatia madai ya ukiukwaji wa sheria za uchaguzi, kukandamiza vyama vya upinzani, na vitisho vya polisi.

Vikosi vya usalama vilijibu kwa risasi, gesi ya machozi, na amri ya kutotoka nje, pamoja na mauaji yaliyolenga watu, na kusababisha wasiwasi wa kimataifa na maonyo ya usafiri kutoka kwa serikali kadhaa za kigeni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *