Serikali ya Sudan na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) zimeonya kuhusu mgogoro mbaya wa utapiamlo miongoni mwa watoto nchini Sudan, huku vita na mapigano ya ndani yakiendelea kwa mwaka wa nne sasa.

Pande hizo mbili zimesisitiza kwamba mgogoro unaoongezeka na uhaba wa chakula na huduma za afya vinawasukuma mamilioni ya watoto katika hatari, katika kipindi hiki ambapo ukosefu wa ufadhili wa misaada ya kibinadamu unaendelea kushuhudiwa.

Waziri wa Afya wa Sudan, Haitham Mohamed Ibrahim, ameviambia vyombo vya habari kwamba utapiamlo miongoni mwa watoto ni mojawapo ya athari mbaya zaidi za kiafya za vita ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa zaidi ya miaka mitatu, akieleza kuwa athari za mzozo huo kwenye mfumo wa afya zinatofautiana kutoka jimbo hadi jingine. Amesema majimbo ya kaskazini na mashariki yenye utulivu wa kiwango fulani, yanabeba mzigo wa kupokea idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao, na kwamba majimbo ya Darfur na Kordofan yanaendelea kuteseka kutokana na hali ngumu sana ya kibinadamu na kiafya kutokana na kuendelea mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Waziri Haitham Mohamed Ibrahim ameeleza kwamba wafanyakazi wa huduma za afya katika maeneo yenye migogoro wanafanya kazi katika mazingira na hali ngumu sana na kuongeza kuwa, tafiti zilizofanywa na Wizara ya Afya kwa ushirikiano na washirika wa kimataifa zinaonyesha kuwa kiwango cha utapiamlo mkali miongoni mwa watoto kimefikia takriban 15% katika ngazi ya kitaifa, huku kikiongezeka hadi takriban 30% katika baadhi ya maeneo ya Darfur na Kordofan.

Haitham Mohamed Ibrahim amesisitiza kwamba mgogoro huo hautokani na uhaba wa chakula nchini Sudan, bali ni kutokana na ugumu wa kufikisha chakula kwa raia walioathiriwa na vita kutokana na kuzuiwa na kufungwa njia za usambazaji.

Kwa upande wake, mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan, Sheldon Yett, amesema kwamba viwango vya utapiamlo miongoni mwa watoto vimeongezeka kwa kiasi kikubwa tangu kuzuka kwa vita vya ndani nchini humo, akisisitiza kwamba mgogoro wa sasa hausababishwi na ukame au mabadiliko ya hali ya hewa, bali ni kutokana na kuendelea mgogoro huo na athari zake za kuporomoka masoko, kuvurugika minyororo ya usambazaji na ugumu wa kufikisha chakula kwa familia zilizoathiriwa.

Mwakilishi huyo wa UNICEF ameonya kwamba shirika hilo, kama mashirika mengine ya misaada ya kibinadamu, linakabiliwa na ugumu unaoongezeka katika kukidhi mahitaji kutokana na ufadhili mdogo, akielezea kwamba limepokea robo tu ya ufadhili unaohitajika, jambo ambalo linalazimisha kufanya “maamuzi machungu” na kuzuia misaada kuwafikia watoto wote wanaohitaji, licha ya mgogoro huo kuongezeka siku hadi siku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *