
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali jinai na mashambulizi yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Iran katika saa 24 zilizopita.
Wizara hiyo ilitoa taarifa Jumapili usiku ikiyataja mashambulizi ya Marekani kuwa “ya kikatili” na ukiukaji wa wazi wa Hati ya Umoja wa Mataifa, hasa Kifungu cha 2(4) cha hati hiyo.
Imeonya kwamba mashambulizi haya sio tu kwamba yanatishia amani na usalama wa kimataifa lakini pia yamevuruga juhudi za miezi kadhaa za kupunguza mivutano na kurejesha utulivu kote Asia Magharibi.
Taarifa hiyo imesema kuwa siku 25 tu baada ya kusainiwa makubaliano ya kusitisha vita, utawala wa Marekani umekiuka waziwazi karibu kila kipengele cha makubaliano hayo.
Vikosi vya jeshi la Marekani vimelenga kwa makusudi miundombinu ya usafiri ya Iran, boti za uvuvi, meli za mizigo, na vifaa na majengo ya hali ya hewa, na kufanya baadhi ya uhalifu mbaya zaidi wa kivita.
Utawala wa Washington pia umeingilia waziwazi mamlaka halali ya Iran ya kusimamia Lango-Bahari la Hormuz, kuvuruga kwa makusudi usalama kwenye njia hiyo muhimu ya majini na usafirishaji wa meli za kibiashara za kimataifa.
Wakati huo huo, hatua ya jeshi la kigaidi la Marekani ya kutumia ardhi na zana zinazomilikiwa na nchi za Kiarabu za pwani ya kusini ya Ghuba ya Uajemi imeyageuza mataifa hayo kuwa viwanja vya vita vyake haramu na vya kijinai dhidi ya watu wa Iran.
Ikisisitiza tena azma yake ya kutetea mamlaka na ardhi ya Iran dhidi ya uchokozi wa Marekani na mchokozi mwingine yeyote, Wizara ya Mambo ya Nje imetoa onyo kali dhidi ya ushiriki au ushirikiano wa aina yoyote na wachokozi.
Imezikumbusha nchi jirani kuhusu wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa wa kuzuia ardhi na zana zao kutumiwa kwa ajili ya mashambulizi dhidi ya Iran, ikisisitiza kwamba vyanzo na asili ya uchokozi wowote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu vitakuwa shabaha halali za mashambulizi ya kujihami ya vikosi vya Jeshi vya Iran.
Wizara hiyo pia imefichua kampeni ya uongo inayoendelea kufanywa na Marekani na kueneza taarifa zisizo sahihi zinazolenga kupotosha ukweli na kuhalalisha uhalifu wake.
Ikielezea masikitiko yake kuhusu msimamo usiojenga wa Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kuhusu uvunjaji sheria wa wazi wa Marekani, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kutimiza majukumu yao kuhusu uvunjifu wa amani na usalama wa kimataifa.