Raia wa Zimbabwe wanaokimbia vurugu na vitisho vya chuki dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini wamewasili katika kituo cha mapokezi katika mji wa mpakani wa Beitbridge, Zimbabwe.

Baadhi ya waliorejea Zimbabwe kutoka Afrika Kusini wamesema kuwa walishambuliwa, kuporwa na kulazimishwa kuondoka majumbani na katika sehemu zao za kazi.

Serikali ya Zimbabwe Jumanne iliyopita ilisema kuwa kwa zaidi ya wiki tano sasa imewasaidia takriban raia wake 21,300 kurejea nchini kutoka Afrika Kusini, huku mashinikizo yakiongezeka kwa wahamiaji wasio na vibali rasmi vya makazi kuondoka Afrika Kusini.

Raia wa nchi mbalimbali za Afrika, zikiwemo Ghana, Malawi, Msumbiji, Nigeria, Uganda na Zimbabwe wamekuwa wakiondoka Afrika Kusini kwa wiki kadhaa sasa kupitia programu zinazofadhiliwa na serikali.

Raia wa Kiafrika walianza kuondoka Afrika Kusini wiki kadhaa zilizopita kufuatia mashinikizo ya makundi ya wananchi wa Afrika Kusini wenye chuki dhidi ya wahamiaji ambao wanasema wahamiaji hao wasio na vibali rasmi vya kuishi nchini humo wanapasa kuondoka nchini humo ifikapo Juni 30; katika kampeni inayoandamana na maandamano ya vurugu na mapigano ambapo wahamiaji wasiopungua wanne wameuawa.

Waziri wa Habari wa Zimbabwe, Soda Zhemu amesema: Tangu tarehe 25 Mei hadi sasa takriban raia 21,291 wa nchi hiyo wamerejea nchini kupitia mkakati unaofadhiliwa na serikali. 

Zimbabwe na Afrika Kusini zina mpaka wa pamoja wenye shughuli nyingi ambapo idadi kubwa ya watu huvuka kwenda na kurudi kila siku. Aidha safari nyingi kati ya hizo hufanyika kwa siri na bila kusajiliwa rasmi na mamlaka husika za nchi mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *