
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limesema kuwa vikosi vyote vya ulinzi viko tayari kulinda haki za taifa na kuweka mfumo unaokusudiwa na Iran katika Lango -Bahari la Hormuz.
Msemaji wa Jeshi la Iran, Brigedia Jenerali Mohammad Akraminia ameeleza haya kupitia televisheni ya taifa huku kukiwa na mvutano mpya katika Mlango-Bahari wa Hormuz uliosababishwa na mashambulizi ya kichokozi ya anga ya Marekani dhidi ya Iran, jambo ambalo ni ukiukaji mkubwa wa makubaliano ya mwezi uliopita ya kusitisha vita kati ya pande mbili.
Brigedia Jenerali Akramiania amesema: Marekani inajaribu kuhalalisha njia isiyofaa ya usafirishaji wa meli ya kusini mwa Lango-Bahari hilo, ambayo haiendani na masharti ya Hati ya Maelewano (MoU) kati ya Tehran na Washington.
“Kwa mujibu wa masharti ya hati hiyo, Iran ndiyo inayopaswa kusimamia mipango yote ya usafirishaji katika Lango-Bahari la Hormuz. Jamhuri ya Kiislamu inafanya kazi kwa ushirikiano na Oman ili kuanzisha mipango ya pamoja katika njia hiyo ya baharini katia fremu ya kidemokrasia na ya amani,” ameongeza kusema msemaji wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
“Tuna jukumu la kulinda usalama wa Lango–Bahari la Hormuz na usafirishaji wa meli za mafuta kupitia eneo hilo kama Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tumesimama imara kuhakikisha utekelezaji wa makubaliano yanayoendana na Hati ya Maelewano (MoU) na sambamba na msimamo wa Iran,” ameeleza Brigedia Jenerali Mohammad Akraminia.