Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf ameionya Marekani kwamba inalazimika kutimiza majukumu yake la sivyo italazimika kulipa gharama ya kukiuka ahadi na majukumu yake chini ya makubaliano ya kukomesha vita.

Qalibaf ametoa matamshi hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X leo Jumapili baada ya jeshi la kigaidi la Marekani kufanya mashambulizi ya anga ya duru ya tatu wiki hii dhidi ya Iran, jambo ambalo ni ukiukaji mkubwa wa Mkataba wa Maelewano (MoU) uliosimamiwa na Pakistan kati ya Tehran na Washington.

Ameashiria Kifungu cha 5 cha MoU, ambacho kinasisitiza kuwa Iran pekee ndiyo inayohusika na kusimamia mipango ya kufunguliwa tena Lango-Bahari la Hormuz, njia muhimu ya usafirishani wa nishati na kuandika: “Zama za mikataba ya upande mmoja zimekwisha. Tulikwambia: timiza majukumu yako la sivyo utalipa gharama. Hii ndiyo hali halisi.”

Vikosi vya Ulinzi vya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mapema leo vimetekeleza operesheni ya pamoja ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani katika nchi za Jordan, Kuwait, Qatar, Oman na Bahrain, ikiwa ni hatua ya kujibu mashambulizi endelevu ya Marekani dhidi ya maeneo ya kusini mwa Iran.

Wakati huo huo, Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza kufungwa Lango Bahari la Hormuz “hadi taarifa nyingine itakapotolewa,” likisisitiza kuwa njia hiyo muhimu ya majini itaendelea imefungwa hadi pale Marekani itakapokomesha uingiliaji wake wa kijeshi katika eneo hili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *