• Askofu Hieronymus Emusugut Joya amewasimamisha kazi mapadri sita wa Jimbo Katoliki la Maralal kutokana na madai ya matumizi mabaya ya mamlaka
  • Askofu huyo ametoa masharti mapya makali yanayowazuia mapadri kunywa pombe katika baa, kuishi na wapenzi, kumiliki biashara binafsi na kulala nje ya makazi yao bila ruhusa
  • Askofu Joya pia ametangaza uteuzi wa mapadri watano wapya kama sehemu ya juhudi za kuimarisha uongozi wa kichungaji katika jimbo hilo

Askofu wa Jimbo Katoliki la Maralal, Rt. Rev. Hieronymus Emusugut Joya, IMC, amewasimamisha kazi mapadri sita na kutangaza hatua kali za kinidhamu zinazolenga kukabiliana na usimamizi mbaya wa fedha, utovu wa maadili na mapungufu ya kiutawala ndani ya jimbo hilo.

Askofu Joya amewasimamisha kazi mapadre sita wa Jimbo Katoliki la Maralal.
Askofu Hieronymus Emusugut Joya atangaza kusimamishwa kazi kwa makasisi sita ili kuimarisha nidhamu ya kipadre. Picha: Radio Mchungaji.
Source: Facebook

Askofu Joya alitoa tangazo hilo Jumapili, Julai 12, wakati wa Misa Takatifu ya Jumapili ya 15 ya Kipindi cha Kawaida katika Parokia ya Watakatifu Petro na Paulo mjini Maralal.

Kwa mujibu wa Radio Mchungaji, askofu huyo alitafakari karibu miaka minne ya huduma yake katika jimbo hilo, akisema alilikuta likikabiliwa na changamoto kubwa za kifedha na kiutawala alipowasili.

Pia soma

Majina ya wanaume 3 walioteketea kwenye ajali ya Mbagathi yafichuliwa

“Inasikitisha kusema kwamba nililikuta jimbo hili likiwa na matatizo mengi, lakini hakuna aliyekuwa tayari kuniambia chanzo cha matatizo hayo na namna ya kuyatatua,” alisema katika taarifa yake.

Ni kina nani mapadri waliosimamishwa kazi Maralal?

Mapadri sita waliosimamishwa kazi wakisubiri kushughulikiwa kwa kesi zao ni:

  • Padri Paul Maina
  • Padri Peter Musau
  • Padri Stephen Lekasuyan
  • Padri Peter Nderitu
  • Padri Christopher Letikirich
  • Padri John Dida

Askofu alisema hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na madai ya matumizi mabaya ya mamlaka ya Kanisa, uzembe katika utawala na usimamizi mbaya wa mali za Kanisa.

Askofu Joya alisisitiza kuwa hatua hiyo haikuchukuliwa bila ushahidi.

“Simshtaki padri yeyote bila kuwa na ushahidi wa kuaminika,” ilisema taarifa hiyo, ikiongeza kuwa baada ya kupokea taarifa za kuaminika kuhusu utovu wa nidhamu, alichukua hatua kwa mujibu wa Sheria za Kanisa (Code of Canon Law) ili kulinda hadhi ya ukuhani na usimamizi sahihi wa mali za Kanisa.

Askofu Joy ametoa sheria kali kwa mapadri, ikiwa ni pamoja na kuwazuia kunywa pombe.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Maralal atangaza sheria mpya kwa mapadre wote. Picha: SN Lenduda.
Source: Facebook

Askofu Joya atoa masharti mapya kwa mapadri wote

Pamoja na kuwasimamisha kazi mapadri hao, Askofu Joya alitoa maelekezo mapya yatakayowahusu mapadri wote wa jimbo hilo kuanzia mara moja.

Mapadri wote wanatakiwa kurejea katika makazi yao ya kipadri ifikapo saa moja jioni (7:00 pm) kwa ajili ya sala za jioni, na hawataruhusiwa kulala nje ya makazi hayo bila kibali cha moja kwa moja kutoka kwa askofu.

Pia soma

Basi la shule lililokuwa na wanafunzi 56 lahusika katika ajali barabara ya Kabarnet-Marigat

Hakuna raia wa kawaida atakayekubaliwa kulala katika nyumba ya padri au nyumba ya watawa bila idhini ya askofu.

Askofu huyo pia amewakataza mapadri kunywa pombe katika baa au ndani ya makazi ya parokia na taasisi za Kanisa, na amepiga marufuku padri yeyote kuongoza ibada akiwa amelewa.

Aidha, mapadri hawataruhusiwa kumiliki au kuendesha biashara binafsi zisizohusiana na Kanisa wala kununua mali zilizosajiliwa kwa majina ya ndugu zao bila kueleza chanzo halali cha fedha zilizotumika.

Kuishi pamoja kama mume na mke au kuwa katika mahusiano ya kimapenzi, iwe na mtu wa jinsia tofauti au wa jinsia moja, nako kumepigwa marufuku kabisa.

Magari na pikipiki za jimbo zitatumika tu na watu walioteuliwa rasmi, huku gharama zote za matengenezo zikibebwa na parokia au taasisi husika.

Kuhusu usimamizi wa fedha, Askofu Joya aliamuru fedha zote za Kanisa zisimamiwe kwa uwazi, kamati za fedha ziwezeshwe kutekeleza majukumu yao ya usimamizi, na bajeti pamoja na ukaguzi wa hesabu ufanyike kila mwaka katika parokia na taasisi zote.

Askofu Joya atangaza uteuzi mpya wa mapadri

Pamoja na hatua hizo za kinidhamu, Askofu Joya alitangaza uteuzi wa mapadri watano wapya ili kuimarisha huduma ya kichungaji.

Pia soma

Mudavadi awaambia upinzani kushinda urais si rahisi kama wanavyofikiria: “Ni ngumu”

  • Padri Dominic Lesayon ameteuliwa kuwa padri msaidizi wa Parokia ya Kanisa Kuu la Maralal.
  • Padri Albert Letaon ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa St. Joseph Allamano Pastoral Centre na Radio Mchungaji.
  • Padri Solomon Ebei ameteuliwa kuwa padri wa Parokia ya St. Matthew Lodokejek.
  • Padri Ambrose Lepartingat ameteuliwa kuwa padri wa Parokia ya Christ the Risen Lord Morijo.
  • Padri Marko Lopetet ameteuliwa kuwa padri msaidizi wa Parokia ya St. Matthew Lodokejek.

Askofu huyo alihitimisha kwa kuwasihi waumini kuwaombea mapadri waliosimamishwa kazi wanapoanza kipindi cha kutafakari kuhusu wito wao wa ukuhani.

“Waombeeni mapadri wetu hawa. Kwa wakati huu wanaanza maisha ya kutafakari kwa kina kuhusu thamani ya wito wao na umuhimu wa kulitumikia Kanisa kwa manufaa ya wote,” alisema.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *