
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4
Ugumba huathiri takribani mtu mmoja kati ya wanandoa sita, huku wanaume wakichangia karibu nusu ya visa vya ugumba. Ni tatizo ambalo lipo kwa wanaume pia kwa kiwango kikubwa.
Licha ya miongozo ya kimatibabu kutoka Taasisi ya Kitaifa ya Afya na Hudu (NICE) ya Uingereza, ikishauri kwamba wanandoa wanaokosa kupata mimba baada ya miezi 12 wanapaswa kupimwa pamoja kwa wakati mmoja, lakini wanaume mara nyingi hutengwa na mfumo wa huduma ya afya.
Kwa sababu matibabu ya uzazi kama upandikizaji wa mimba ama IVF ni kwa ajili ya mwanamke, matibabu ya ugumba mara nyingi yamekuwa yakiwalenga wanawake.
Wagonjwa kama Luke kutoka Uingereza, ambaye amehangaika kutafuta mtoto yeye na mke wake anasema kwamba miadi, mawasiliano, na makaratasi huwa zaidi yanamuhusu mwanamke.
Upendeleo huu wa kimuundo husababisha ucheleweshaji mkubwa wa utambuzi wa tatizo kwa wanaume.
Ilichukua mwaka mmoja kwa Luke kupimwa baada ya upandikizaji kushindwa, kabla ya manii yake kufanyiwa vipimio.
Vile vile, mgonjwa anayeitwa James alipata ucheleweshaji wa miaka miwili kabla ya kufanyiwa uchunguzi kamili wa kimwili na upimwaji wa wa homoni.
Wanaume wanahisi kutengwa

Utafiti wa 2019 ulioongozwa na Profesa Bola Grace kutoka chuo kikuu cha London unaonyesha kwamba wanaume wengi wanataka kuhusika lakini wanahisi kutengwa na huduma. Kutengwa huku husababisha wanaume kutojihusisha sana, na hivyo kuimarisha dhana potofu kwamba hawana nia ya kushiriki matibabu.
Kulingana na Profesa Allan Pacey, mtaalamu wa masuala ya uzazi kwa wanaume kutoka chuo kikuu cha Manchester, anasema kliniki za uzazi kwa kawaida huongozwa na wataalamu wa magonjwa ya wanawake, ikimaanisha kuwa afya ya uzazi ya wanaume (andrology) mara nyingi huchukuliwa kama jambo la pili au wazo la baadaye.
Tofauti hii pia inaonekana katika ngazi ya sera ya serikali. Mkakati wa huduma ya afya wa miaka 10 wa Wizara ya Afya kwa Uingereza unataja uzazi mara 20 katika hati yake ya wanawake, na kuweka ukurasa mzima wa mwongozo wa kliniki.
Kinyume chake, hati ya wanaume inataja uzazi mara tano tu, ikiielezea hasa masuala ya mtindo wa maisha kama vile athari za unywaji wa pombe na unene kupita kiasi.
Utasa wa wanaume umeunganishwa na mitazamo ya kijamii kuhusu uanaume, na hivyo kusababisha mzigo mzito wa kisaikolojia.
Wanaume mara nyingi hupata upweke mkubwa na kujihisi kuwa na hatia. James 34 kutoka North Yorkshire, anasema alijiona kama chanzo pekee cha maumivu ya mwenzi wake.
Mamlaka ya Utungishaji wa Mbegu na Kiinitete cha Binadamu (HFEA) inabainisha kuwa kuna vikundi vichache sana vya usaidizi mtandaoni au vya ulimwengu kwa ajili ya wanaume ikilinganishwa na wanawake.
Ili kupambana na kutengwa huku, watu kama Shaun Greenaway, ambaye aligunduliwa na azoospermia, yaani hakuna mbegu kwenye manii yake, walianzisha Podikasti ya Uzazi wa Mwanaume na mtandao wa usaidizi unaoojitolea ili kuhimiza mazungumzo ya wazi.
Mtindo wa maisha na usita kupima
Chanzo cha picha, Getty Images
Ubora wa manii ni jambo nyeti sana, na manii yanaweza kuathirika kutokana na msongo wa mawazo, usingizi duni, uvutaji sigara, lishe duni, na pombe. Wataalamu wanasisitiza kwamba mtindo mzuri wa wa maisha ji jambo muhimu. Kwa sababu inachukua miezi mitatu kutoa manii kuanzia mwanzo hadi mwisho. Kwahyo mabadiliko ya muda mfupi, kama vile kujiepusha na pombe kwa wikiendi tu, hayatatoa matokeo ya haraka.
Licha ya hatari kubwa, wataalamu wa matibabu bado wanakabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya wanaume. Utafiti wa 2022 uligundua kuwa mmoja kati ya wataalamu sita wa uzazi wa Ulaya wanajitahidi mara kwa mara kuwashawishi wanaume kufanya kipimo cha manii.
Baadhi ya wanaume wanakataa kubadilisha tabia hasi, huku wengine wakidhani kwamba wana uwezo wa kuzaa kwa sababu tu wanafanya ngono au wamewahi kuwa baba wa mtoto hapo awali.
“[Uzazi wa wanaume] sio mazungumzo ya kando. Ni kutambua kwamba uzazi wa wanaume ni mada muhimu. Ni sehemu ya msingi ya afya ya uzazi.” Anasema Sophie Sulehria, Mkurugenzi wa Maudhui wa Kipindi cha Uzazi
Mitaala ya shule kupitia mpango mpya ya masomo ya PSHE nchini Uingereza sasa inawapa wanaume masomo kuhusu hatari za kuathiri uzazi, kama vile matumizi ya steroidi, uvutaji sigara, na lishe duni, sawa na hatari kwa wanawake.
Madaktari kama Profesa Hussain Alnajjar wanaelezea kwamba utasa wa wanaume mara nyingi ni kiashiria cha mapema cha matatizo mapana ya kiafya, ikiwa ni pamoja na kasoro za homoni, unene kupita kiasi, na hatari za moyo na mishipa. Kwa hivyo, kupima ubora wa manii hutoa fursa muhimu kwa uingiliaji kati wa matibabu mapema katika afya ya wanaume kwa ujumla.