
Malalamiko kuhusu utendaji wa askari wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe Zanzibar si jambo jipya.
Kwa muda mrefu, wananchi wamekuwa wakieleza kutoridhishwa na namna sheria zinavyotekelezwa katika eneo hilo, huku wakidai baadhi ya watendaji wanatumia nguvu kupita kiasi na kukosa utu wanapowashughulikia wanaodaiwa kukiuka taratibu.
Hakuna ubishi kwamba Mji Mkongwe ni urithi wa dunia unaostahili kulindwa. Serikali kupitia mamlaka husika ina wajibu wa kuhakikisha hadhi yake inalindwa na mazingira yake yanabaki safi na yenye kuvutia.
Kutokana na dhamira hiyo, takribani miaka mitatu iliyopita mamlaka ilianza operesheni za kuwaondoa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika maeneo yanayozunguka Mji Mkongwe.
Operesheni hizo ziliwahusisha pia waendesha bodaboda, mama lishe na wajasiriamali wengine wadogo waliokuwa wakipanga bidhaa zao pembezoni mwa barabara.
Lengo la mpango huo lilikuwa zuri. Hata hivyo, changamoto imekuwa namna ya utekelezaji wake. Malalamiko mengi yamekuwa yakieleza kuwa baadhi ya askari wamekuwa wakitumia nguvu kupita kiasi, kuharibu bidhaa za wananchi na wakati mwingine kuwachukulia hatua hata watu ambao hawakuwa wanauza bidhaa katika maeneo yaliyopigwa marufuku.
Wananchi wamekuwa wakidai kuwa hata mtu anayepita akiwa amebeba bidhaa zake kwa ajili ya kuzipeleka sehemu nyingine huweza kukamatwa kana kwamba alikuwa akifanya biashara. Katika mazingira hayo, bidhaa hukamatwa bila tahadhari ya kuzihifadhi salama, jambo ambalo limezua hisia za uonevu na kuibua chuki dhidi ya mamlaka hiyo. Kwa kawaida, bidhaa zinazokamatwa hupelekwa kuhifadhiwa na wahusika kutakiwa kulipa faini ili kuzichukua. Hata hivyo, kumekuwapo tuhuma kwamba baadhi ya bidhaa hupotea au hurudishwa zikiwa pungufu tofauti na zilivyokamatwa.
Kwa upande wa mama lishe, baadhi yao wamedai vyakula vyao humwagwa au kuliwa baada ya kukamatwa, hali inayowasababishia hasara kubwa kutokana na mtaji wao kuwa mdogo.
Hoja hizi zimewahi kufikishwa hata katika Baraza la Wawakilishi, ambako baadhi ya wajumbe, akiwamo Mwakilishi wa Paje, Jaku Hashimu Ayoub, walihoji mwenendo wa operesheni hizo. Pamoja na maswali hayo, majibu yaliyokuwa yakitolewa mara nyingi yalisisitiza kuwa mamlaka ilikuwa inatekeleza sheria.
Pia kulikuwa na malalamiko kuhusu utozwaji wa faini hata katika maeneo yanayoruhusiwa kwa maegesho, huku changamoto ya mashine za kutoa risiti za maegesho katika eneo la Darajani ikitajwa kusababisha wananchi kuadhibiwa isivyo halali. Serikali ilikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuahidi kuifanyia kazi.
Hata hivyo, tukio lililotokea Juni 29, 2026 lilionesha namna malalamiko hayo yalivyokuwa yamejenga hasira kwa baadhi ya wananchi.
Siku hiyo kundi la waendesha bodaboda lilivamia ofisi za Mamlaka ya Mji Mkongwe, likavunja geti na kuondoka na baadhi ya pikipiki pamoja na mali nyingine zilizokuwa zimekamatwa.
Inadaiwa kuwa kabla ya tukio hilo, askari wa mamlaka walimkamata mama mmoja aliyekuwa akiuza chakula eneo la Darajani akiwa amembeba mtoto mgongoni, wakamnyang’anya chakula chake na kukimwaga. Kitendo hicho kilisambaa kwa haraka na kuzua hisia kali miongoni mwa wananchi, hususan vijana waendesha bodaboda.
Hakuna anayeweza kuhalalisha uamuzi wa kuvamia ofisi za serikali na kujichukulia sheria mkononi.
Hatua hiyo ilikuwa ni kosa na haipaswi kupewa nafasi katika jamii inayozingatia utawala wa sheria. Endapo wananchi wanaona wanaonewa, zipo njia za kisheria za kuwasilisha malalamiko yao kwa viongozi na mamlaka husika.
Hata hivyo, tukio hilo linapaswa kuwa fundisho kwa viongozi na watendaji wote wenye mamlaka ya kusimamia sheria.
Utekelezaji wa sheria unahitaji busara, mawasiliano mazuri na heshima kwa utu wa binadamu. Sheria inapotekelezwa kwa ukali usiozingatia ubinadamu, huweza kujenga chuki na migogoro isiyo ya lazima.
Ni muhimu mamlaka zikajiuliza kama kweli kuna sheria inayoruhusu kuharibu bidhaa za mwananchi au kumwaga chakula kilichokamatwa.
lengo ni kuhakikisha sheria inafuatwa, basi hatua zinazochukuliwa zinapaswa kulinda pia haki na mali za wananchi.
Kwa upande mwingine, hatua zinazochukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Moh’d Ali Abdalla, zinaonyesha kuwa changamoto zinaweza kutatuliwa kwa mazungumzo na elimu. Badala ya kuanza na nguvu, amekuwa akikutana na wafanyabiashara, kusikiliza hoja zao na kuwaelimisha kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa.
Huo ndio uongozi unaojenga ushirikiano kati ya serikali na wananchi. Sheria ni muhimu, lakini utekelezaji wake unapaswa kwenda sambamba na busara, utu na haki. Hapo ndipo mamlaka zitapata ushirikiano wa wananchi badala ya kujenga mazingira ya migogoro ambayo mwisho wake huathiri pande zote.