Wakati fulani huwa naikumbuka kauli ya mwenyekiti wa zamani wa chama cha siasa, na aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kambi ya upinzani.

Alipohojiwa na kituo cha habari, mgombea huyo alisema: “Yaani Watanzania kama wameazimwa nchi yao…” Nilimwelewa vema Mheshimiwa huyo nilipoitazama methali ya Kiswahili: “Nguo ya kuazima haisitiri matako.”

Kama mama alivyo tayari kufa kwa ajili ya mwanaye, mwananchi huwa tayari kupoteza uhai kwa ajili ya kuipambania nchi yake. Ni kwa sababu nchi inapokumbwa na vurugu, raia wa nje wanaikimbia au wanakuja kuchukuliwa na kurudishwa makwao. Lakini raia wa nchi iliyovurugwa hukosa pa kukimbilia.

Wanabaki na shida yao mpaka mwisho. Matokeo yaweza kuwa kupoteza maisha, kupoteza familia, kupoteza mali au kupoteza vyote kwa pamoja.

Nilivyoielewa kauli ya mgombea huyo, baadhi ya wananchi wamepoteza uzalendo kwa nchi yao. Wanaiona nchi yao kuwa sawa na ng’ombe asiye na mwenyewe, kila mmoja anajikamulia kwa faida yake mwenyewe. Mara kadhaa Watanzania wamekuwa wakiwalalamikia wahamiaji haramu, lakini nyuma ya pazia ni wao wenyewe wanaowaleta kwa njia za panya. Hii inamaanisha kuwa wapo tayari mgeni aibe iwapo wao watafaidika binafsi.

Sababu za wananchi kufanya mambo hayo ni mtambuka. Lakini msingi wa sababu hizo unaweza kuwa mmoja tu: ukosefu wa uzalendo. Hapa namaanisha uzalendo kwa wananchi na viongozi wao.

Hawa wawili ni sawa na samaki na maji, kwani kiongozi huchaguliwa na wananchi kama ambavyo mwananchi alivyo na haki ya kugombea uongozi. Na ikumbukwe kuwa mahitaji na madhaifu yao ni yaleyale kwani hapa tunamzungumzia mwanadamu.

Wanadamu hatuna budi kumchagua binadamu miongoni mwetu ili awe kiongozi wetu. Tunategemea huyu awe mfano kwetu sote, na tumfuate kwenye njia za kujenga nchi. Pamoja na kuwa madhaifu yake ni sawa na ya kwetu, tutamwezesha kuona kule kuzuri tusikokuona ili atufikishe. Kama kichwa cha twiga kingekuwa miguuni asingeyafikia malisho kwenye matawi, tena asingemwona simba anayemnyatia.

Lakini kwa nini Watanzania wanajitoa ufahamu? Juzi kati Waziri Mkuu alikemea wauguzi na madaktari wanaokwenda kinyume na taratibu. Wamekuwa wakidai fedha za nauli kwa wagonjwa wanaosafirishwa kwa magari ya wagonjwa (ambulance).

Haijalishi mgonjwa anahudumiwa kupitia Bima ya Afya au unalipia taslimu, akibebwa na gari lao hugeuka kuwa abiria. Tena si wakutozwa nauli ya daladala.

Niliwahi kusikia kuhusu mtu maarufu aliyekuwa rafiki yangu sana. Huyu jamaa alikuwa kapuku kama mimi, akatoweka kwa muda mfupi na kurudi akiwa tajiri mkubwa.

Alimiliki malori yaliyosafiri nchi jirani, nyumba za kupangisha na kadhalika. Binafsi nilishangazwa na sikusita kumtembelea ili anipe siri ya mafanikio yake. Lakini yeye alisisitiza kufanya kazi kwa bidii na kujituma bila kuchoka ndio kulimfikisha hapo.

Baada ya muda siri ilifichuka. Kumbe jamaa alikimbilia katika mikoa ya jirani akijifanya mganga wa kienyeji.

Inaeleweka kuwa wagonjwa huwa tayari kufilisika wakati wakitetea uhai wao. Hivyo waganga feki wanaitumia hiyo kama fursa kwao. Wanaweza kumfilisi mtu anayetetea maisha yake kwa urahisi sana hata kama hawaijui tiba yake. Hilo ndio naliona kwa madaktari na wauguzi wanaomdai mgonjwa mahututi kabla hawajampa tiba.

Ndivyo wanavyoweza kukausha dawa katika Hospitali za Serikali, wakazijaza kwenye vituo vyao binafsi vya afya. Kisha wakawaelekeza wagonjwa kununua dawa kwa bei ghali huko kwenye maduka yao.

Wanayafanya hayo wakijua kuwa wanadhulumu haki na maisha ya wanyonge wasio na hatia. Wahanga wakubwa kwenye maumivu hayo ni kinamama, watoto na walio na mahitaji maalumu.

Pata picha ya mama mjamzito anayegaragara nje ya wodi ya wazazi baada ya kukosa laki mbili za kufanyiwa upasuaji. Kando yake wauguzi wanamsisitiza atangulize japo laki-unusu ili aingizwe wodini.

Lakini isivyo bahati, uchungu unamzidi mama yule hadi anakata roho. Mbaya zaidi kichanga kilichomtegemea mama apate huduma ili kiianze safari yake duniani, nacho kinashindwa kuvuta pumzi yake ya kwanza hapa duniani.

Katika nchi kama hii ya kwetu ambapo udugu unatangulia, dhambi hii inakuwa kubwa zaidi. Kila siku wanamichezo, wanajeshi na makundi ya raia wa kawaida hupanga foleni kutoa misaada kwenye hospitali zetu.

Misaada ni hiyari, lakini ni lazima Serikali iweke usimamizi thabiti kwenye mapato ya nchi na kudhibiti matumizi yake, vipaumbele vikiwa katika mambo ya msingi kama elimu, afya, usalama na kadhalika.

Tukiambiwa kuwa huduma za afya zimefika hadi vijijini, tuone wanakijiji wakifaidika na huduma hizo. Haiingii akilini kuona hospitali zisizo na dawa au wauguzi. Haina tofauti na kujenga jiko la kisasa wakati hakuna chakula. Kodi ya mwananchi inayojenga hospitali ikanunue vifaa vya kinamama wanaojifungua. Ulinzi mkali uwekwe ili dawa na vifaa hivyo visichepushwe, na adhabu kali kwa watakaobainika kuvihujumu.

Napongeza sana mwamko wa makundi yanayochangia huduma za afya. Hata hivyo hizi Bonanza na Marathon ziwe zikichangia kwa ziada, kamwe Serikali isishindwe kutimiza wajibu wake kwa kukosa misaada.

Hayo yakifanyika kama inavyopasa, nina uhakika tiba itawatafuta wagonjwa badala ya wagonjwa kutafuta tiba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *