GAIRO: Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Japhari Kubecha, ametatua changamoto ya muda mrefu iliyokuwa kati ya Serikali ya Kijiji cha Ikwamba na wananchi juu ya miradi mbalimbali ya kijiji.

DC Kubecha amefanya ziara katika Kata ya Mandege, Kijiji cha Ikwamba huku akiendelea kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali za wananchi, ambapo katika ziara yake ameongozana na wajumbe baadhi wa Kamati ya Usalama pamoja na Wataalamu mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.

Mara baada ya kufanya ukaguzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ikwamba pamoja na kuona utekelezaji wa Mradi wa Maji ya Mseleleko, Mkuu wa Wilaya alifanya Mkutano wa Hadhara wa kusikiliza kero na changamoto za wananchi ndipo alipotatua changamoto hiyo ya muda mrefu kati ya Serikali ya Kijiji pamoja na wananchi juu ya miradi mbalimbali ya kijiji.

Mara baada ya makubaliano mbalimbali, DC Kubecha alielekeza baadhi ya mambo kufanywa ndani ya muda wa wiki mbili, huku akisisitiza kuhakikisha wananchi pamoja na Serikali ya Kijiji wanashirikiana kwa pamoja kuhakikisha wanaleta agenda ya maendeleo ndani ya kijiji hicho.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ameahidi mara baada ya mwezi mmoja kurudi tena Ikwamba kujionea utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa.