BAADA ya kipa wa Dodoma Jiji, Ally Salim kuonyesha kiwango kizuri akiwa na kikosi hicho cha ‘Walima Zabibu’, uongozi wa timu hiyo umeanza mazungumzo na menejimenti ya mchezaji huyo kwa ajili ya kumpa mkataba mpya wa miaka miwili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson amesema baada ya msimu wa 2025-2026 kumalizika, watapitia mikataba ya mchezaji mmoja baada ya mwingine, kisha kufanya uamuzi kabla ya msimu ujao wa 2026-2027 kuanza.

“Mazungumzo ya sasa ni ya kumuongezea mkataba mpya Kocha, Amani Josiah kisha baada ya hapo tutahamia kwa wachezaji ambao mikataba yao imefikia mwishoni, mazungumzo ya awali tumeanza na yapo katika hatua nzuri hadi sasa,” amesema Fortunatus.

SALI 01

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Dodoma Jiji imemwekea mkataba mpya kipa huyo kwa ajili ya kuendelea naye kwa msimu ujao wa 2026-2027, licha ya kukosekana uwanjani muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya bega.

Kipa huyo aliyejiunga na Dodoma Jiji, Septemba 7, 2025, akitokea Simba, alipata majeraha ya bega, wakati akiwa katika harakati za kuuokoa mpira kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City, Februari 3, 2026.

SALI 02

Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kuisha sare ya kufungana bao 1-1, Ally alipata majeraha hayo alipokuwa anauokoa mpira baada ya kukutana na mchezaji wa Mbeya City aliyempiga kichwa kwenye bega lake.

Tangu ajiunge na Dodoma Jiji, Ally Salim amekuwa kipa wa kikosi cha kwanza, ambapo kwa msimu wa 2025-2026 katika Ligi Kuu Bara alimaliza na clean sheets tano, akizidiwa na mwenzake wa timu hiyo, Daniel Mgore aliyemaliza na sita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *