Wakati Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye akianza mchakato wa kuanzisha chama chake cha siasa kuelekea uchaguzi mdogo, Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) nchini Kenya kimetangaza kumuunga mkono Rais William Ruto kwenye uchaguzi wa mwaka 2027.

Joto la kisiasa katika mataifa hayo mawili linazidi kupanda kila siku kufuatia viongozi wa mataifa hayo kutafuta uungwaji mkono katika chaguzi zilizo mbele yao ili kujitengenezea nafasi ya ushindi katika chaguzi hizo zenye ushindani mkali.

Licha ya kuwa na mazingira tofauti ya kisiasa, Senegal na Kenya zina mifumo ambayo haiwafungi wanasiasa na vyama vyao, jambo linalowawezesha kubadilisha vyama au kuungana na vyama vingine bila kupoteza nafasi zao serikalini.

Hata hivyo, Tanzania ina nafasi ya kujifunza katika siasa za mataifa hayo hasa katika kuruhusu mgombea binafsi, muungano wa vyama na kutofungwa na sheria kwamba chama ndiyo mdhamini wa mgombea, akifukuzwa au kujiondoa unapoteza nafasi yake serikalini.

Hali ilivyo Senegal

Huko Senegal, Rais Faye ameanza maandalizi ya kuanzisha chama chake cha siasa, hatua inayodhihirisha wazi kuvunjika kwa uhusiano wake wa kisiasa na aliyekuwa mshirika wake wa karibu, Waziri Mkuu wa zamani, Ousmane Sonko.

Hatua hiyo imekuja wakati mvutano wa uongozi kati ya viongozi hao wawili ukiendelea kuongezeka huku Senegal ikielekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na mchakato wa kufanya marekebisho ya katiba.

Muungano wa kisiasa unaomuunga mkono Rais Faye ulisema katika taarifa iliyotolewa wiki iliyopita kuwa rais huyo amemteua mshauri wake mkuu, Aminata Touré kuongoza kikosi kazi kitakachohusika na kuanzisha vuguvugu jipya la kisiasa.

Uamuzi huo umeelezwa kuwa ishara kubwa zaidi hadi sasa ya kuwapo kwa mpasuko wa kudumu kati ya Faye na Sonko, ambao walikuwa washirika wakuu katika harakati zilizowaingiza madarakani.

Tangu alipoingia madarakani, Rais Faye amekuwa mwanachama wa chama tawala cha Pastef, lakini uhusiano wake na Sonko ulianza kudhoofika miezi kadhaa kabla ya kumfuta kazi Sonko kama Waziri Mkuu, Mei.

Baada ya kuondolewa katika nafasi hiyo, Sonko alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Senegal, ambako ameendelea kusukuma ajenda ya marekebisho ya katiba yanayolenga kubadilisha mfumo wa siasa nchini humo.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kifungu kinachozuia rais aliyepo madarakani kuendelea kuwa kiongozi wa chama cha siasa kwa wakati mmoja.

Wiki iliyopita, wabunge waliidhinisha marekebisho hayo ya katiba, lakini Rais Faye ameamua kuyapeleka kwa wananchi kupitia kura ya maoni badala ya kuyatia saini na kuwa sheria.

Serikali bado haijatangaza tarehe ya kufanyika kwa kura hiyo.

Kura hiyo ya maoni inatarajiwa kuwa kipimo muhimu cha umaarufu na uungwaji mkono wa kisiasa kwa pande zote mbili, Faye na Sonko, huku ushindani wao ukiendelea kushika kasi.

Mgawanyiko unaoongezeka kisiasa unatokea wakati Senegal ikikabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi baada ya kubainika kuwa serikali iliyopita ilitoa taarifa zisizo sahihi kuhusu kiwango cha deni la taifa.

Mvutano huo pia unajitokeza kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2027, ambao unatarajiwa kuwa jaribio la kwanza kubwa la kupima nguvu za kisiasa za makundi mawili yanayoongozwa na Faye na Sonko.

Kuanzishwa kwa chama kipya kinachoungwa mkono na rais kunaweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa sura ya siasa za Senegal na kuunda upya muungano wa vyama ndani ya serikali inayotawala.

ODM kutembea na Ruto 2027

Huko Kenya, chama cha ODM kimetangaza kuwa hakitasimamisha mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa Kenya wa mwaka 2027, badala yake kitamuunga mkono Rais Ruto kuwania muhula wa pili madarakani.

Kauli hiyo ilitolewa jana, Julai 12, 2026, na kiongozi mwandamizi wa ODM, Oburu Oginga, ambaye alisema uamuzi huo umetokana na mazungumzo ya kisiasa yanayoendelea kati ya chama hicho na viongozi wa serikali.

“Katika mazungumzo ya muungano tunayofanya, tunajua safari hii ODM haitasimamisha mgombea wa urais. Kwa hiyo, tutamuunga mkono Rais William Ruto kuwania muhula wa pili,” alisema Oburu.

Akizungumza katika harambee iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la St. Pascal’s Chiga, Kaunti ya Homa Bay, Oburu alisema ushirikiano huo unalenga kuimarisha mshikamano wa kisiasa, huku ukiihakikishia ODM nafasi ya kushiriki katika utekelezaji wa ajenda za serikali.

Alisema chama hicho kitaingia katika muungano huo kwa masharti yatakayohakikisha sera na vipaumbele vyake vinazingatiwa, pamoja na kuwapo kwa mfumo unaobainisha nafasi na ushiriki wa ODM ndani ya serikali.

Msimamo huo ni ushindi wa Rais Ruto ambaye hata kabla kifo cha aliyekuwa kiongozi wa chama hicho, Raila Odinga, alifanikiwa kumshawishi kuwa upande wake, jambo ambalo lilipunguza joto la kisiasa nchini humo.

Licha ya kwamba kuna mgawanyiko ndani ya ODM, bado msimamo huo utambeba Ruto ambaye amepoteza mvuto nchini humo kutokana na kinachoelezwa kuwa ni kutotekeleza ahadi nyingi alizozitoa kwa Wakenya.

Wakati huohuo, Rais Ruto anaongoza orodha ya wanasiasa wanaotajwa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 kwa kupata uungwaji mkono wa asilimia 32, kulingana na utafiti mpya wa maoni ya wananchi uliotolewa na kampuni ya Infotrak.

Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa Ruto anaungwa mkono zaidi na wanaume kwa asilimia 34 ikilinganishwa na asilimia 30 miongoni mwa wanawake.

Anafuatiwa na kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, aliyepata asilimia 13 huku aliyekuwa Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Fred Matiang’i, wakipata asilimia 12 kila mmoja.

Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua alipata asilimia nne, wakati Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino akipata asilimia tatu na aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga, akipata asilimia mbili.

Kwa upande wake, kiongozi wa chama cha PLP, Martha Karua, alipata asilimia moja ya uungwaji mkono.

Hata hivyo, utafiti huo umeonyesha kuwa asilimia 18 ya waliohojiwa bado hawajafanya uamuzi kuhusu mgombea watakayemuunga mkono. Idadi hiyo ni kubwa zaidi kwa wanawake, ambapo asilimia 20 walisema hawajaamua, ikilinganishwa na asilimia 15 ya wanaume. Aidha, asilimia tatu ya washiriki wa utafiti walikataa kueleza mgombea wanayempenda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *