
Iringa. Bei ya mayai ya kisasa imeendelea kupanda katika masoko mbalimbali ya Mkoa wa Iringa, huku wafugaji wakieleza kuwa kupungua kwa uzalishaji kunakosababishwa na msimu wa baridi kumeathiri upatikanaji wa bidhaa hiyo na kuongeza bei sokoni.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Julai 15, 2026, mjini Iringa, wafugaji na wafanyabiashara wa mayai wamesema mabadiliko hayo yameanza kujitokeza katika masoko ya jumla na rejareja, huku kiwango cha mayai kinachoingia sokoni hakitoshelezi mahitaji ya wateja.
Hali hiyo imeongeza ushindani wa kupata bidhaa hiyo na kusababisha bei kupanda katika kipindi kifupi.
Mfugaji wa kuku, Judith Kipangula, amesema msimu wa baridi huathiri utagaji wa kuku, wakati mazingira ya ufugaji na lishe nayo hayajaboreshwa ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
“Katika kipindi hiki cha baridi, uzalishaji wa mayai umepungua ukilinganisha na kawaida. Kuku hawatagi kwa kiwango walichokuwa wakitaga awali, wakati gharama za chakula na matunzo zimeendelea kuwa juu. Hali hii imepunguza upatikanaji wa mayai na kuchangia kupanda kwa bei sokoni,” amesema.
Kutokana na kupungua kwa uzalishaji, wafanyabiashara wa jumla wanasema bei ya trei moja ya mayai imeongezeka kutoka kati ya Sh7,000 hadi kufikia Sh11,000.
Ongezeko hilo pia limeonekana katika biashara ya rejareja, ambako yai moja sasa linauzwa kati ya Sh450 na Sh500, hali inayowalazimu baadhi ya walaji kupunguza matumizi au kutafuta vyakula mbadala.
Mfanyabiashara wa mayai katika Soko la Semtema, Joseph Nzigilwa, ameiambia Mwananchi kuwa licha ya bei kupanda, faida kwa wafanyabiashara haijaongezeka kwa kiwango kikubwa kwa sababu wao pia wananunua mayai kwa gharama ya juu kutoka kwa wasambazaji.
“Biashara siyo nzuri kama ilivyokuwa miezi iliyopita. Tunauza kwa bei ya juu, lakini gharama za kununua mayai zimeongezeka na wateja wengi wameanza kupunguza ununuzi,” amesema.
Wananchi pia wameeleza kuwa ongezeko la bei ya mayai limeongeza gharama za maisha, hasa kwa familia zinazoyatumia kama chanzo muhimu cha lishe kutokana na urahisi wake wa kupatikana na thamani yake ya lishe.
Mkazi wa Manispaa ya Iringa, Agnesa Chota, amesema kupanda kwa bei kumebadili utaratibu wa matumizi katika baadhi ya familia.
“Awali tulikuwa tunanunua mayai mara kwa mara, lakini sasa bei imepanda. Wakati mwingine tunaamua tusinunue kabisa au tunanunua kwa siku chache tofauti na ilivyokuwa zamani,” amesema.
Kwa mujibu wa baadhi ya walaji, ongezeko hilo limewalazimu kupunguza idadi ya mayai wanayonunua kila wiki ili kuendana na uwezo wao wa kifedha.
Ofisa Mifugo wa Mkoa wa Iringa, Zakaria Mwanuke, amesema mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kuathiri uzalishaji wa mayai endapo wafugaji hawataendelea kuboresha mazingira ya mabanda, lishe na huduma za afya ya mifugo.
“Ni muhimu kuendelea kuwapatia wafugaji elimu kuhusu mbinu bora za ufugaji ili kupunguza athari za misimu mbalimbali na kuhakikisha uzalishaji wa mayai unabaki katika kiwango kinachokidhi mahitaji ya soko,” amesema.
Wadau wa sekta ya mifugo wanaeleza kuwa uzalishaji wa mayai una mchango mkubwa katika kipato cha wafugaji na upatikanaji wa lishe kwa jamii.
Hivyo, mabadiliko yoyote yanayoathiri uzalishaji hujitokeza moja kwa moja katika upatikanaji wa bidhaa hiyo na mwenendo wa bei sokoni.